Skip navigation.
Home kabah

Taratibu Za Hajj Na Umrah


SHAYKH MUHAMMAD BIN SWAALIH AL-'UTHAYMIYN

Imefasiriwa na  ALHIDAAYA

 

Alhamdulillah, Sifa na shukurani zote Anastahiki Mola wa ulimwengu.  Swalah na salaam zimfikie Muhammadصلى الله عليه وآله وسلم Mtume wa mwisho pamoja na Ahli zake na Maswahaaba zake. 

Hajj ni mojawapo ya aina ya ibada bora kabisa na ni amali tukufu kabisa kwani ni mojawapo ya Fardhi za Kiislamu ambazo Allaah سبحانه وتعالى Amemtuma Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kutuongoza. Dini ya mja wa Kiislamu haikamiliki bila ya Hajj. Ni ibada inayokubaliwa pindi yafuatayo yatahakikishwa:


Mtu ataifanyia bidii ya dhati kuwa ni kwa ajili ya Allaah سبحانه وتعالى Pekee na kwa kutamani Akhera na haitowezekana kufanyika kwa ajili ya kumuonyesha mtu au kwa ajili ya maslahi ya mambo ya dunia.

Inampasa mtu anapotenda ibada yake afuate mfano wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa maneno na vitendo na hii haiwezekani kutimia ila kwa kujifunza na kupata elimu ya mafundisho ya Sunnah.

       

AINA ZA HAJJ

Kuna aina tatu za Hajj; Tamattu'u, Ifraad na Qiraan.

TAMATTU'U

Hujaji anavaa Ihraam ya 'Umrah tu wakati wa miezi ya Hajj (anapokwenda Makkah mapema) ambayo inamaanisha kwamba anapofika Makkah atafanya twawwaaf na Sa'ayi ya 'Umrah. Kisha atanyoa au kukata nywele. Siku ya Tarwiyyah ambayo ni siku ya nane Dhul-Hijjah, atavaa nguo zake za Ihraam kwa ajili ya Hajj tu na atatekeleza yote yanayompasa kufanya.

 

IFRAAD

Hujaji atavaa Ihraam kwa ajili ya Hajj pekee. Atakapofika Makkah atafanya twawwaaf pamoja na Sa'ayi ya Hajj. Hana haja kunyoa au kukata nywele zake kwani hatoki kwenye Ihraam yake. Bali atabakia katika Ihraam mpaka amalize kupiga mawe katika Jamrah Al-'Aqabah siku ya 'Iyd. Anaruhusiwa kuchelewesha Sa'yi yake ya Hajj mpaka amalize twawwaaf ya Hajj.

 

QIRAAN

Hujaji anavaa Ihraam ya zote mbili; 'Umrah na Hajj au anavaa kwanza Ihraam ya 'Umrah, kisha anatia Nia ya Hajj kabla ya twawwaaf ya Hajj. Wajibu wa anayefanya Ifraad ni sawa sawa na anayefanya Qiraan, isipokuwa tu mwenye kufanya Qiraan inampasa achinje na mwenye kufanya Ifraad haimpasi kuchinja. 



Aina ya Hajj iliyo bora kabisa katika hizi ni ya Tamattu'u ambayo ndio Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisisitiza wafuasi wake waitekeleze.

Hata kama Hujaji akitia Nia ya kufanya Qiraan au Ifraad, anaruhusiwa kubadilisha Nia yake kuingia katika Hajj ya Tamattu'u. Na anaweza kufanya hivi hata kama baada ya kufanya twawwaaf na Sa'ayi kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipofanya Twawwaaf na Sa'ayi mwaka wa Hijjah ya Widaa' (Hajj ya kuaga) pamoja na Maswahaba zake, aliamrisha wote ambao hawakuleta mnyama kwa ajili ya kuchinja, wabadilishe nia zao za Hajj na kutia Nia ya 'Umrah, wakate nywele zao, na wavue Ihraam mpaka Hajj. Akasema:

(("لولا أني سقت الهدي لفعلت مثل الذي أمرتكم به))   البخاري

"Ingelikuwa sikuleta mnyama ningelifanya hivyo nilivyokuamrisheni mfanye" [Al-Bukhaariy]   

 

'UMRAH

Akipenda Hujaji kuwa katika Twahaara ya 'Umrah, akoge kama josho la janaba. Mwanamume atie manukato mazuri kabisa na apake mafuta mazuri kichwani. Hakuna ubaya harufu ikibakia baada ya Ihraam.

Kukoga ili kuingia katika Ihraam ni Sunnah kwa mwanamume na mwanamke pamoja na wanawake wenye hedhi na wale wenye Nifaas (Damu ya uzazi).  

Baada ya kukoga na kujitayarisha, Mahujjaaj wote isipokuwa wanawake wenye hedhi au nifaas wataswali Swalah za fardhi inapowadia wakati wake kama kawaida. Na ikiwa sio wakati wa Swalah ya fardhi basi ataswali Raka'ah mbili ambazo ni vizuri mtu kuswali kila anapotia wudhuu.

Atakapomaliza kuswali atasema Talbiyah hii:

لبيك عمرة، لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك.

Labbayka 'Umrah, Labbayka-Llaahumma Labbayk.  Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk. Innal-Hamda Wan-Ni'imata Laka Wal-Mulk Laa Shariyka Lak.

"Nimekuitikia Ewe Mwenyeezi Mungu 'Umrah, Nimekuitika Ewe Mwenyezi Mungu nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika Wako nimekuitika, hakika Sifa njema na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshrika"

Mwanamume atasema kwa sauti na mwanamke atasema kiasi cha kumsikia wa pembezoni mwake. (Wanawake wenzake).

Anatakiwa mtu kusema Talbiyah kila mara khaswa anapofika na kubadilisha kituo. Mfano anapopanda na kushuka kipando wakati wa safari au wakati wa usiku unapoingia na asubuhi kunapopambazuka. Pia Amuombe Allaah سبحانه وتعالى Ridhaa Yake ya kupata Pepo na aombe kujikinga kwa Rahma ya Allaah سبحانه وتعالى kutokana na moto. 

Anatakiwa mtu aseme Talbiyah wakati wa 'Umrah tokea anapovaa Ihraam yake hadi anapoanza Twawwaaf. Wakati wa Hajj aseme Talbiyah kutokea mwanzo wakati anapovaa Ihraam yake mpaka anapoanza kupiga mawe Jamarah ya 'Aqaba siku ya 'Iyd.

Hujaji anapoingia msikitini atangulize mguu wake wa kulia na kusema:

(( أعوذ بالله العَظيـم وَبِوَجْهِـهِ الكَََرِِيـمِ وَسُلْطـانِهِ القََدِيـمِ مِنَ الشّيْـطانِ الرَّجِـيمِ، [ بِسْـمِ الله، وَالصَّلاةُ] [وَالسَّلامُ عَلى رَسولِ الله]، اللّهُـمَّ افْتَـحْ لي أَبْوابَ رَحْمَتـِكَ))

((A'uudhu BiLLahil-'Adhwiym, Wa Biwajhihil-Kariym Wa Sultwaanihil-Qadiym Minash-shaytwaanir-rajiym, Bismillah Was-Swalaatu Was-salaam 'Alaa Rasuli-Llah, Allaahuumaf-tah-liy Abwaaba Rahmatik))

 “Najilinda na Mwenyezi Mungu  Aliye Mtukufu, na kwa uso Wake, mtakatifu, na kwa utawala Wake wa kale, kutokana na shetani aliyeepushwa na Rahma za Mwenyezi Mungu, (kwa Jina la Mwenyezi Mungu, na Rahma) (Na amani zimfikie Mtume wa Mwenyezi Mungu ) Ewe Mwenyezi Mungu  nifungulie milango ya Rahma Zako"

Anakaribia Hajar Al-Aswad (jiwe jeusi) na kuligusa kwa mkono wake wa kulia na kulibusu. Ikiwa hii haiwezekani, basi aelekeze tu uso wake kuelekea kwenye Hajar Al-Aswad na kuashiria kwa mkono wake (na kubusu mkono wake) Haifai kusukuma na kusababisha madhara kwake na kwa watu.  

Anapoligusa Hajar Al-Aswad anatakiwa aseme hivi:

  بسم الله والله أكبر، اللهم إيماناً بك، وتصديقاً بكتابك، ووفاء بعهدك، واتباعاً لسنة نبيك محمد صلى الله عليه وآله وسلم

Bismillahi Wa-Allaahu Akbar, Allaahumma Iymaanam-Bik,  Wa Taswdiyqam-Bikitaabik, Wa Wafaa-am-Bi'ahdik, Wat-tibaa'al-lisunnati Nabiyyika Muhammad Swalla Allaahu 'Alayhi Wasallam.

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ni Mkubwa, Ewe Allaah kwa iymani Kwako, na kwa kuamini kitabu Chako, na kwa kutekeleza ahadi yako, na kufuata Sunnah ya Nabii Wako Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم.

Hujaji lazima atembee huku Ka'abah liko kushotoni mwake. Anapofika Rukn Al-Yamaani aiguse lakini asibusu bali atakapokuwa baina yake na Hajar Al-Aswad aseme:

 رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الاَخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ 

((Rabbanaa Aatinaa Fid-Duniyaa Hasanataw-Wafil- Aakiharati Hasanataw-Waqinaa 'Adhaaban-Naar)).

"Mola wetu Mlezi, Tupe duniani mema, na Akhera mema, na Utulinde na adhabu ya Moto"

((اللهم إني أسألك العفو والعافية في الدنيا والآخرة))

Allaahumma Inni As-alukal-'afuw Wal-'aafiyata Fid-Duniyaa Wal-Aakhirah)

"Ewe Allaah Nakuomba msamaha na 'afya duniani na Akherah".

Kila mara akilipita Hajar Al-Aswad anatakiwa aseme "Allaahu Akbar" (Mungu Mkubwa).

Katika kufanya Twawwaaf zilizobakia anaweza kusema anachopenda katika Du'aa, kumtaja Allaah سبحانه وتعالى, kusoma Qur'aan. Hii kwa sababu twawwaaf, Sa'ayi na kupiga mawe Jamrah imekhusiwa kwa ajili ya kumtaja Allaah سبحانه وتعالى .  

Katika Twawwaaf hii anahitajika mwanamume afanye vitu viwili: 

Aweke Al-Idhwtwiba'a kutoka mwanzo wa Twawwaaf mpaka mwisho. Al-Idhwtwiba'a ina maana kwamba ni kuweka sehemu ya katikati ya vazi (ridaa) chini ya kwapa lake la kulia na kipande cha ridaa akipitishe juu ya bega la mkono wa kushoto. Anapomaliza kufanya Twawwaaf anaweza kurudisha ridaa yake katika hali yake ya mwanzo kwa sababu wakati wa Idhwtwiba'a ni wakati wa Twawwaaf tu.

Kufanya Ar-Raml katika Twawwaaf tatu za mwanzo. Ar-Raml ina maana kwamba kuzunguka kwa mwendo wa haraka kwa  hatua ndogo ndogo. Kisha anatakiwa atembee mwendo wa kawaida katika Twawwaaf zake nne za mwisho. 

Atakapomaliza mizunguko saba ya Twawwaaf, atakaribia Maqaamu Ibrahyim na atasoma:

((وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى))

((Na alipokuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kuswalia)) [Al-Baqarah: 125]

Ataswali Raka'ah mbili fupi, akiwa karibu kiasi iwezekanavyo na nyuma ya Maqaamu Ibrahiym. Katika Raka'ah ya mwanzo atasoma Suratul-Kaafiruun na Raka'ah ya pili atasoma Suratul-Ikhlaas. Atakapomaliza Raka'ah mbili atarudi kuligusa Hajar Al-Aswad kama itawezekana.   Atakwenda Al-Mas'aa, atakapofika karibu na As-Swafaa atasoma:

((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ اللّهِ))

((Hakika vilima vya Swafaa na Marwah ni katika alama za Mwenyezi Mungu)) [Al-Baqarah: 158]

 Atapanda (mlima wa) Swafaa mpaka aweze kuona Ka'abah. Aelekee Ka'abah na anyanyue mikono yake, amtukuze Allaah سبحانه وتعالى na aombe Du'aa apendayo. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliomba:

 لا إِلهَ إلاَّ  اللهُ وَحْدَهُ  لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لا إِلَهَ إلا اللهُ وَحْدَهُ أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ

Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu Laa Shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr.  Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu, Anjaza Wa'dahu Wanaswara 'Abdahu Wahazamal-Ahzaaba Wahdahu))

 “Hapana Mola Apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa peke Yake, wala Hana mshirika Wake, ni Wake Ufalme na ni Zake sifa njema Naye juu ya kila kitu ni Muweza.  Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke Yake, Ametekeleza ahadi Yake, na Amemnusuru mja Wake, na Amevishinda vikosi peke Yake”

Atasema mara tatu akiomba Du'aa baina yake.

Atateremeka As-Swafaa na kuelekea Al-Marwah kwa mwendo wa kawaida mpaka anapofika katika alama ya kijani, hapo atakimbia mpaka alama ya kijani nyingine.  Ataendelea kuelekea Al-Marwah kwa mwendo wa kawaida. Atakapofikia ataupanda (mlima) na kuelekea Qiblah, atanyanyua mikono na kurudia kusema kama alivyosema alipokuwa As-Swafaa. Atateremka Al-Marwah kuelekea As-Swafaa, akihakikisha anatembea sehemu zinazohusika na kukimbia katika sehemu zinazohusika.

Ataendelea kufanya hivyo hivyo mpaka amalize mizunguko saba. Kutoka As-Swafaa kwenda Al-Marwah ni mzunguko mmoja na kurudi ni mzunguko mwingine. Wakati wa Sa'ayi anaweza kusoma anachotaka kama Du'aa, Qur'aan na kumtaja Allaah سبحانه وتعالى.

Anapomaliza Sa'ayi atanyoa nywele. Mwanamke atakata nywele kiasi cha urefu wa ncha ya kidole. Inapendekezeka kunyoa nywele zote, na kunyoa ni bora kuliko kukata kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaombea du’aa walionyoa mara tatu na waliokata mara moja. Isipokuwa ikiwa Hajj iko karibu na hakuna wakati wa kutosha kwa nywele kurudi kukua, basi ni bora kukata ili nywele zibakie kwa ajili ya kunyoa wakati wa Hajj, kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaamrisha Maswahaba kukata nywele katika 'Umrah kwani walifanya asubuhi ya tarehe nne ya Dhul-Hijjah.

Baada ya hapo 'Umrah itakuwa imemalizika na Hujaji atakuwa huru kuvaa nguo nyingine, kutia manukato (mwanamume) na kurudia hali ya ndoa (kujimai na mkewe) na kadhalika.

 ***************************

 

HAJJ

 

SIKU YA TARWIYYAH, TAREHE 8 DHUL-HIJJAH 

 

Siku ya tarehe 8 Dhul-Hijjah, Hujaji atajitoharisha tena kwa kukoga kama alivyofanya kabla ya 'Umrah mahali hapo anapokaa.  Atavaa Ihraam yake na kusema:

 لَبَّيْكَ حَجّاً  لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ ، لا شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ ،إنَّ الْحَمْدَ ،وَالنِّعْمَةَ ،لَكَ وَالْمُلْكُ ، لا شَرِيكَ لَكَ  

Labbayka Hajja  Labbayka-Allaahumma Labbayk, Labbayka, Laa Shariyka Laka Labbayk, Innal-Hamda Wan-Ni'mata Laka Wal-Mulk, Laa Shariyka Lak

"Nimekuitikia Ewe Mwenyeezi Mungu Hajj, Nimekuitika Ewe Mwenyezi Mungu nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika Wako nimekuitika, hakika Sifa njema na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshirika Wako"

Ikiwa atakhofu kuwa jambo litamzuia kukamilisha Hajj yake basi atie Nia kwa kusema:

 وإن حبسني حابس فمحلي حيث حبستني

"Ikiwa nitazuiliwa na kizuizi chochote sehemu yangu ni popote nilipozuiliwa" 

Ikiwa hana khofu kama hiyo basi hana haja kujishurutisha hivyo.  

Kisha Hujaji atakwenda Mina na huko ataswali Swalah ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, 'Ishaa na Al-Fajiri na kufupisha Swalah za Raka'h nne kuwa mbili mbili kila moja bila ya kuziunganisha. (Yaani kuswali kila moja vile kwa wakati wake ila ziwe fupi tu) kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiswali Qaswran (kufupisha) na sio Jam'an (kujumuisha). 

 

TARERHE 9 DHUL-HIJJAH – SIKU YA 'ARAFAH

Jua litakapochomoza  siku ya pili ambayo ni tarehe 9 Dhul-Hijjah, atakwenda 'Arafah na huko ataswali Adhuhuri na Alasiri kwa kuunganisha wakati wa Adhuhuri na kufupisha mbili mbili. Atabakia katika msikiti wa Namirah mpaka jua litakapokuchwa. Atamkumbuka Allaah سبحانه وتعالى  hapo 'Arafah na kuomba Du'aa nyingi sana awezavyo huku akielekea Qiblah na sio kuelekea Mlima wa 'Arafah.

Ikiwa atakuwa hakujaaliwa kuweko katika msikiti wa Namirah karibu na Jabali la 'Arafah basi popote alipokuweko kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisimama katika jabali la 'Arafah na akasema:

((وقفت هاهنا وعرفة كلها موقف، وارفعوا عن بطن عرنة))

((Nimesimama hapa na 'Arafah yote ni kisimamo (cha 'Arafah) na msisimame katika bonde la 'Uranah))

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiomba:

 لا إِلَهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَريكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ ولَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَديرٌ.

 Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu Laa Shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr))

 “Hapana Mola Apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke Yake, Hana mshirika Wake, ni Wake Ufalme na ni Zake sifa njema, Naye juu ya kila kitu ni Muweza”

Atakapochoka anaruhusiwa kuzungumza na wenzake au kusoma vitabu vyenye faida khaswa vile kuhusu Ukarimu na zawadi kubwa za Allaah سبحانه وتعالى kwetu ili apate kuzidi kupata matumaini kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى. Kisha arudi kuendelea kuomba Du'aa na kuhakikisha kuwa anatumia wakati wake wa mwisho wa siku hiyo katika Du'aa nyingi na nzito kwa sababu Du'aa zilizo bora kabisa ni Du'aa za siku ya 'Arafah. 

 

 MUZDALIFAH

Jua litakapozama ataondoka 'Arafah kwenda Muzdalifah na huko ataswali Magharibi, 'Ishaa na Al-Fajiri Ikiwa atachoka au ana uchache wa maji, anaruhusiwa kuunganisha Magharibi na 'Ishaa.  Ikiwa atakhofu kuwa hatofika Muzdalifah mpaka baada ya usiku wa manane, basi aswali kabla ya kufika huko kwani hairuhusiwi kuchelewesha Swalah mpaka usiku wa manane. 

Atabakia huko Muzdalifah akiomba Du'aa na kumtaja Allaah سبحانه وتعالى mpaka Alfajiri, ataswali Alfajiri mapema kwa adhaan na Iqaamah, kisha ataelekea Mash'aril-Haraam (sehemu tukufu) na atafanya tahliyl, yaani atasema "Laa Ilaaha Illah Allaah"  pia "Allaahu Akbar" na ataomba Du'aa mpaka kupambazuke vizuri. Ikiwa hakujaaliwa kwenda Mash'aril-Haraam, ataomba hapo hapo alipo kutokana na kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

((وقفت هاهنا وجمع كلها موقف)) 

((Nimesimama hapa na kote hapa ni kisimamo (cha Muzdalifah)) [Muslim]

Na atakuwa akiomba Du'aa kwa kuelekea Qiblah na huku akinyanyua mikono. 

      

MINAA - AR-RAMIY (KUPIGA MAWE) KATIKA JAMRAH 

 

Ikiwa ni mtu dhaifu na hawezi kustahamili  zahma za watu wakati wa Ar-Ramiy (kupiga mawe), (kama mwanamke na mtu mzima), basi anaruhusiwa kwenda Mina mwisho wa usiku huo kupiga Jamrah kabla ya zahma ya watu kuwa kubwa.  

 

TAREHE 10 DHUL-HIJJAH

 

Karibu na jua kuchomoza Hujaji ataondoka Muzdalifah kuelekea Mina. Atakapofika atafanya yafuatayo:

Atatupa mawe saba moja moja katika Jamrah ya 'Aqabah ambayo iko karibu na mnara wa Makkah na kusema :

الله أَكْبَر

Allaahu Akbar

Kwa kila jiwe analotupa.

Atachinja mnyama, na kula baadhi ya nyama na atatoa nyingine kuwapa masikini. Kuchinja ni fardhi kwa wale wanaofanya Hajj ya Tamattu'u na Qiraan. (Kwa hali ilivyo sasa huwa haiwezekani kufanya hivi, hivyo anaweza kutekeleza kama anavyoamrishwa yaani kulipa na kuacha jukumu hili kwa serikali ifanye kazi ya kuchinja)   

Atanyoa au kukata nywele. Inapendekezwa kunyoa kuliko kukata (kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika maelezo ya 'Umrah hapo juu). Mwanamke atakata nywele zake urefu wa ncha ya kidole.

Mambo matatu hayo yafanywe kama ilivyo taratibu yake ikiwezekana, lakini hakuna kikwazo au sharti ikiwa mtu atatanguliza kitendo chochote kabla ya chengine.

Akimaliza hayo mambo matatu anaruhusiwa kujitoa katika Ihraam. Na anaweza kuvaa nguo zake za kawaida na kufanya kila jambo la halali ila kuingia katika kitendo cha ndoa.    

Atakwenda Makkah kufanya Twawwaaful-Ifaadhwah na Sa'ayi kwa ajili ya Hajj. Ni Sunnah kujitia manukato kabla ya kwenda Makkah (kwa wanaume) kutokana na kauli ya Bibi 'Aishah رضي الله عنها kwamba:

((كنت أطيب النبي صلى الله عليه وسلم لإحرامه قبل أن يحرم، ولحله قبل أن يطوف بالبيت )) البخاري و مسلم

((Nilikuwa nikimpaka manukato Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kabla ya kuingia katika Ihraam na na baada ya kutoka katika Ihraam kabla ya kutufu Ka'aba)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Atakapomaliza Twawwaaf na Sa'ayi, Hujaji anaruhusiwa kufanya kila kitu kilicho halali hata tendo la ndoa. 

 

TAREHE 11 na 12 DHUL- HIJJAH

 

Baada ya kufanya Twawwaaf na Sa'ayi atarudi Mina kulala huko usiku wa tarehe kumi na moja na wa kumi na mbili Dhul-Hijjah.

Atarusha mawe Jamrah tatu jioni zote za siku ya tarehe kumi na moja na kumi na mbili Dhul-Hijjah. Ataanza kwanza Jamrah ya kwanza ambayo iko mbali na Makkah, kisha ya katikati, kisha ya mwisho Jamrah Al-Aqabah. 

Katika kila moja ya Jamrah atarusha mawe saba moja moja na huku atasema Takbiyr kwa kila jiwe analorusha.

Atasimama baada ya kurusha mawe Jamrah ya kwanza na ya katikati kufanya Du'aa akielekea Qiblah akiwa amenyanyua mikono na kuomba Du'aa ndefu akiweza kufanya hivyo, au asimame kadiri atakavyoweza. Wala haimpasi kuacha kuomba Du'aa kwani ni Sunnah na watu wengi sana hawatekelezi hivi aidha kwa kutokujua au kupuuza. Na kila inapokuwa Sunnah haitekelezwi huwa kutangazika kwake kwa watu na kutendeka huenda ikaachwa kabisa na kupotea.   

Hairuhusiwi kurusha mawe kabla ya Adhuhuri katika siku mbili hizi. 

Ni bora kabisa kutembea kwenda kurusha mawe, ingawa kipando kinaruhusiwa. 

Ikiwa mtu ana haraka baada ya kurusha mawe siku ya kumi na mbili Dhul-Hijjah, anaweza kuondoka Mina lakini iwe kabla ya jua kuzama. Lakini akipenda kuzidisha makazi yake, ambayo ni bora zaidi, basi alale Mina usiku wa kumi na tatu na arushe mawe jioni kama alivyofanya siku ya kumi na mbili.

 

TWAWWAAFUL-WIDAA'I (TWAWWAAF YA KUAGA)

 

Atakapokuwa tayari kurudi kwao, atafanya twawwaaful-Widaa' ambayo ni mizunguko saba katika Ka'abah kutokana na kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم:

((لا ينفر أحد حتى يكون آخر عهده بالبيت ((مسلم

((Asikimbie mtu (asiondoke zake) mpaka iwe shughuli yake (kitendo chake cha mwisho) katika Nyumba (Ka'abah)) [Muslim]

Wanawake wenye hedhi na nifaas hawana lazima kufanya Twawwaaful-Widaa'i kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

((أمر الناس أن يكون آخر عهدهم بالبيت إلا أنه خفف عن الحائض)) البخاري و مسلم  

((Aliamrisha watu iwe shughuli zao za mwisho ni Ka'abah isipokuwa waliruhusiwa (wanawake) wenye hedhi)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ikiwa baada ya twawwaaful-Widaa'i umebakia wakati wa kusubiri wenzake au kipando chake au kununua kitu njiani hakuna neno juu yake, wala hana haja ya kurudia kufanya twawwaaful-Widaa'i isipokuwa akitia Nia ya kuchelewesha safari yake, mfano akitaka kuondoka mwanzo wa siku akatufu Ka'abah, kisha akachelewesha safari yake hadi mwisho wa siku, basi itamlazimu arudie kufanya Twawwaaf ili kiwe kitendo chake cha mwisho ni Ka'abah.

 

  **************************

 

KUTEMBELEA MSIKITI WA MTUME صلى الله عليه وآله وسلم

 

Hujaji atakwenda Madiynah kabla au baada ya Hajj kwa Nia ya kutembelea msikiti wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na kuswali humo na sio  kwa nia ya kutembelea kaburi kutokana na Hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم:

((لا تشد الرحال إلا إلى ثلاثة مساجد: المسجد الحرام، ومسجدي هذا، والمسجد الأقصى)) البخاري ومسلم

((Msifanye ziara ila kwa misikiti mitatu; Masjidul-Haraam [wa Makkah], na msikiti wangu [wa Madiynah], na Masjidul-Aqswaa [wa Palestina])) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Swalah moja humo ni bora kuliko Swalah elfu mahali pengine isipokuwa msikiti wa Makkah.

 

Anapofika msikitini atatanguliza mguu wa kulia na kusema:

 أعوذ بالله العَظيـم وَبِوَجْهِـهِ الكَََرِِيـمِ وَسُلْطـانِهِ القََدِيـمِ مِنَ الشّيْـطانِ الرَّجِـيمِ،[ بِسْـمِ الله، وَالصَّلاةُ] [وَالسَّلامُ عَلى رَسولِ الله]، اللّهُـمَّ افْتَـحْ لي أَبْوابَ رَحْمَتـِكَ

A'uudhu BiLLahil-'Adhwiym, Wa Biwajhihil-Kariym Wa Swultwaanihil-Qadiym Minash-shaytwaanir-rajiym, Bismillah Was-Swalaatu Was-Salaam 'Alaa Rasuli-Llah, Allaahuumaf-tah-liy Abwaaba Rahmatik.

 “Najilinda na Mwenyezi Mungu  Aliye Mtukufu, na kwa uso Wake, mtakatifu, na kwa utawala Wake wa kale, kutokana na shetani aliyeepushwa na Rahma za Mwenyezi Mungu, (kwa Jina la Mwenyezi Mungu na Rahma) (Na amani zimfikie Mtume wa Mwenyezi Mungu ) Ewe Mwenyezi Mungu  nifungulie milango ya Rahma Zako"

Anatakiwa aswali Raka'ah mbili za Sunnah ya kuamkia msikiti au aswali Swalah za fardhi ikiwa ameingia katika wakati wake.

Atakwenda katika kaburi la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na atasimama mbele yake, atamsalimia kwa kusema:

 السَّلاَمُ عَلَيْكَ أَيُّها النَّبِيُّ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُه  

 Amani zishuke juu yako Ewe Mtume na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka Zake

 اللّهُـمَّ صَلِّ عَلـى مُحمَّـدٍ  وَعَلـى آلِ مُحَمَّد كَمـا صَلَّيْـتَ عَلـى آلِ إبْراهـيم  وَعَلـى آلِ إبْراهـيم إِنَّكَ حَمـيدٌ مَجـيد

   اللّهُـمَّ  َبارِكْ عَلـى مُحمَّـدٍ  وَعَلـى آلِ مُحَمَّد  كَمـا بارِكْتَ عَلـى    إبْراهـيم وَعَلـى آلِ إبْراهـيم  إِنَّكَ حَمـيدٌ مَجـيد

Allaahumma Swalliy 'Alaa Muhammad Wa 'Alaa Aal Muhammad Kamaa Swallayta 'Alaa Ibraahiym Wa 'Alaa Aal Ibraahiym Innaka Hamiydum-Majiyd. 

Allaahumma Baarik 'Alaa Muhammad Wa 'Alaa Aali Muhammad Kamaa Baarakta 'Alaa Ibraahiyma Wa 'Alaa Aal Ibrahiym Innaka Hamiydum-Majiyd.

“Ewe Mwenyezi Mungu  Mrehemu Muhammad,  na aila ya Muhammad  kama Ulivyomrehemu Ibraahiym na aila ya Ibrahiym hakika Wewe Umesifika na Umetukuka"

"Ewe Mwenyezi Mungu Mbariki  Muhammad, na aila ya Muhammad,  kama ulivyombariki Ibraahiym na aila ya Ibraahiym, hakika Wewe Umesifika na Umetukuka.

أشْهَد أنَّكَ رَسُولُ الله حَقاً، وَأنَّكَ قَدْ بَلَّغْتَ الرِّسَالَةَ، وَأدَّيْتَ الأَمَانَةَ، وَنَصَحْتَ الأُمَّةَ، وَجَاهَدْتَ فِي اللهِ حَقَّ جِهَادِه، فَجَزاكَ اللهُ عَنْ أُمَّتك أَفْضَل ما جَزَى نَبِيَّا عَنْ أُمَّتِه.

Ash-hadu Annaka Rasuulu-Allaah Haqqan, Wa Annaka Qad Ballaghtar-Risaalat, Wa Addaytal-Amaanah, Wa Naswahtal-Ummah, Wa Jaahadta Fiy-Llahi Haqqa Jihaadih, Fa-Jazaaka-Llahu 'An Ummatika Afdhwal Maa Jazaa Nabiyyan 'An Ummatih

"Nashuhudia kwamba wewe hakika ni Mjumbe wa Allaah, Na kwamba umefikisha ujumbe, na umefikisha amana. Na umenasihi Ummah, na umefanya jihaad kwa njia ya Allaah ipasavyo hakika, basi Allaah Akulipe kwa Ummah wako bora kuliko Alivyomlipa Mtume (yeyote) kwa Ummah wake"

Kisha atasogea hatua moja au mbili upande wa kulia kujiweka mbele ya Abu Bakar na kumsalimia kwa kusema :

 السَّلاَمُ عَلَيْكَ

Assalaamu 'Alayka

"Amani zishuke juu yako"

Na akipenda amuombee Du'aa munaasib kama kusema:

رَضِيَ اللَّهُ عَنْكَ وَجَزَاكَ اللَّهُ  عَنْ أُمَّة مُحَمَّد  أَفْضَل جَزَاء

Radhiya-Llahu 'Anka Wa Jazaaka-Llahu 'An Ummati Muhammad Afdhwal Jazaa

"Allaah Aridhike na wewe na  Akulipe malipo bora kwa niaba ya Ummah Wa Muhammad" 

Kisha asogee hatua moja au mbili upande wa kulia kidogo na kuelekea kwa 'Umar na kumsalimia kwa kusema:

السَّلاَمُ عَلَيْكَ

Assalaamu 'Alayka

"Amani zishuke juu yako"

رَضِيَ اللَّهُ عَنْكَ وَجَزَاكَ اللَّهُ  عَنْ أُمَّةَ مُحَمَّد  أَفْضَل جَزَاء

Radhiya-Llahu 'Anka Wa Jazaaka-Llahu 'An Ummati Muhammad Afdhwal Jazaa

"Allaah Aridhike na wewe na  Akulipe malipo bora kwa niaba ya Ummah Wa Muhammad"

 

Haifai mtu kujikurubisha kwa Allaah سبحانه وتعالى kwa kugusa ukuta wa chumba cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  au kufanya twawwaaf (kuzunguka). Pia haelekei mtu huko bali anaelekea Qiblah wakati wa kuomba Du'aa.  Kwa sababu kujikurubisha kwa Allaah سبحانه وتعالى  haiwi ila kama Alivyotuwekea sheria Yeye pamoja na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم, na ibada zinatakiwa zifuatwe sio zianzishwe.

Na mwanamke haimpasi kuzuru kaburi la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wala kaburi la yeyote mwingine kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amelaani wanawake wanaozuru makaburi. Lakini aswali na kumsalimia mahali hapo hapo alipo kwani zinamfikia salamu kama alivyosema:

)) صلوا علي فإن صلاتكم تبلغني حيث كنتم" وقال: "إن لله ملائكة سياحين في الأرض يبلغوني من أمتي السلام((  النسائي و أحمد

((Niswalieni kwani Swalah zenu zinanifikia popote mlipo. Na akasema: ''Hakika Allaah Anao Malaika wanazunguka katika ardhi na kunitumia salamu kutoka kwa ummah wangu'')) [An-Nasaaiy na Ahmad]

Akiwa Katika hali ya Twahaarah atakwenda kuswali katika msikiti wa Qubaa.

Atakwenda Al-Baaqiy'i kutembelea kaburi la 'Uthmaan رضي الله عنه atasimama mbele yake na kumsalimia kwa kusema:

السَّلاَمُ عَلَيْكَ

Assalaamu 'Alayka

"Amani zishuke juu yako"

رَضِيَ اللَّهُ عَنْكَ وَجَزَاكَ اللَّهُ  عَنْ أُمَّةَ مُحَمَّد  أَفْضَل جَزَاء

Radhiya-Llahu 'Anka Wa Jazaaka-Llahu 'An Ummati Muhammad Afdhwal Jazaa

"Allaah Aridhike na wewe na  Akulipe malipo bora kwa niaba ya Ummah Wa Muhammad" 

Kisha atawasalimia Waislamu wengine waliofariki waliopo hapo makaburini Al-Baaqiy'i kwa kusema:

السَّلامُ عَلَـيْكُمْ أَهْلَ الدِّيارِ مِنَ المؤْمِنيـنَ وَالْمُسْلِمينَ، وَإِنّا إِنْ شاءَ اللهُ بِكُـمْ لاحقون، ( وَ يَرْحَمُ اللَّهُ الْمُسْتَقْدِمِينَ مِنَّا وَالْمُسْتَأْخِرِينَ) نَسْـاَلُ اللهَ لَنَـا وَلَكُـمُ العَـافِيَةَ.

Assalaamu 'Alaykum Ahlad-Diyaari Minal-Muuminiyna Wal-Muslimiyn, Wa Insha-Allaah Bikum Laahiquun, Wayarhamu-Llahul-Mustaqdimiyna Minnaa Walmusta-akhiriyn) Nas-alu-Llah Lanaa Wa Lakumul-'Aafiyah

“Amani ishuke juu yenu watu wa nyumba za waumini na Waislamu, nasi Apendapo Mwenyezi Mungu tutakutana nanyi, tunamuomba Mwenyezi Mungu Atusamehe, sisi na nyinyi.  [Na Mwenyezi Mungu Awarehemu wa mwanzo na wa mwisho] namuomba Mwenyezi Mungu  Atupe sisi nanyi afya njema.”

 

Atakwenda Uhud na kutembelea kaburi la Hamzah رضي الله عنه,  pamoja na mashahidi waliozikwa hapo.  Atawatolea salamu na kuwaombea hivyo hivyo Du'aa ya kuzuru makaburi.

 

TANBIHI MUHIMU

Zifuatazo ni Tanbihi muhimu kwa mwenye kufanya Hajj au 'Umrah

1

Ajishurutishe katika fardhi za Allaah سبحانه وتعالى za dini zinazompasa kama kuswali kwa wakati wake na kuswali Jama'ah

2

Ajiepusha na yote yaliyoharamishwa kama uchafu, dhulma, utovu wa adabu kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى  :

((الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلاَ رَفَثَ وَلاَ فُسُوقَ وَلاَ جِدَالَ فِي الْحَجِّ))

((Hija ni miezi maalumu. Na anayekusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija)) [Al-Baqarah: 197]

3

Ajiepushe na kuwadhuru Waislamu wenziwe kwa maneno au vitendo katika sehemu tukufu na kwengine kote.

 

4

Ajiepushe na  yote aliyozuiliwa kufanya katika  Ihraam kama yafuatayo:

Kwa Hujaji wa kiume na wa kike

a) Asikate nywele Hapana ubaya kukuna kichwa au kuchana nywele na ikiwa zitatoka kwa ajili hiyo hakuna ubaya. 

b) Asikate kucha. Ikikatika kucha na ikiwa inamuudhi hakuna ubaya kuikata.

c) Asijitie manukato mwilini, au katika nguo zake baada ya kuingia katika Ihraam. Ama kabla ya Ihraam inafaa (kama ilivyoelezwa mwanzo). Vile vile katika chakula kama kutia zaafarani kwani zaafarani ni katika harufu nzuri. Vilevile ajiepushe na kuoga sabuni iliyo na manukato. Hakuna ubaya ikiwa manukato aliyotia kabla ya Ihraam yamebakia katika nguo zake.

d)  Asimguse na kumbusu mke/mume wake kwa hamu na baya zaidi asifanye naye jimai (kitendo cha ndoa).

e) Asifunge Nikaah (Ndoa) au kupeleka posa kwa mwanamke kwa ajili yake au mwenzake.

f)  Asivae glavu, lakini hakuna ubaya kufunika mikono yake kwa nguo yake.

 

Tanbihi kwa mwanamume pekee:

 

a) Asivae nguo zilizoshonwa kama fulana, shati, suruwali, soksi, viatu na kadhalika ila tu ikiwa hakuweza kupata Izaar na makubadhi au malapa ndio anaweza  kuvaa suruwali na viatu.   Anaruhusiwa kuvaa saa, miwani visaidizi vya kusikia au kuzungumzia.

b) Haifai kujifunika kichwa kama kuvaa kofia, kilemba, ghutra na kadhalika. Ama kujifunika mwavuli kwa ajili ya kujihifadhi jua hakuna ubaya. Pia hakuna ubaya akibeba begi lake kichwani.

 

Tanbihi kwa mwanamke pekee:

 

a) Asivae niqaab na glavu. Kuna Maulamaa waliosema kuwa haifai kujifunika uso wake kwa niqaab au chochote kingine ila kama kuna wanaume karibu yake, basi inambidi ajifunike uso wake (kuepusha fitna) na hatakiwi kulipa fidia akifanya hivyo.

 

Rahma na Amani Zimshukie Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Na Ahli Zake  na Maswahaba Zake.

 

 

FAHARASA

 

Al-Baaqiy'i

Sehemu Madiynah ambako kuna makaburi ya Maswahaba

 

Al-Idhwtiba'a

Kuweka sehemu ya katikati ya shuka (Ridaa) Chini ya kwapa ya mkono wa kulia na ncha zake juu ya bega la mkono wa kushoto katika twawwaaf

Al-Ikhlaas

Surah Namba 112 katika Qur'aan yaani 'Qul-Huwa-Llahu Ahad'

 

Al-Kaafiruun

Surah Namba 109 katika Qur'aan yaani 'Qul Yaa Ayyuhal-Kaafiruun'

 

Al-Marwah