Kumpenda Nabiy ﷺ Ni Kumtii Na Kumfuata

 

Kumpenda Nabiy Ni Kumtii Na Kumfuata

 

Abu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Sifa zote njema anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Swalah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na watu  wema baada yao mpaka siku ya Malipo.

 

Nawausia kaka na dada zangu pamoja na kuiusia nafsi yangu katika kumcha na kumpenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Ndugu zangu wapenzi, Waislam wengi wamejenga ada ya kumkumbuka Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumsherehekea mazazi (Mawlid) yake, na kutenga siku maalum kwa sherehe hiyo na kukesha kwa kuzitaja sifa zake na kuimba na wengine kucheza na kuandaa vyakula kwa kuiadhimisha siku hiyo. Ingawa ushahidi wa kuzaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku hiyo iliyozoeleka kusherehekewa, ina utata! Vitabu mbalimbali vya kihistoria vinataja tarehe mbalimbali na hata mwaka tofauti wa kuzaliwa kwake.

 

Kinachokubaliwa ni siku ambayo ni ya Jumatatu kama alivyosema mwenyewe wakati Swahaba zake watukufu walipomuuliza kwanini hufunga Swawm katika siku hiyo.

 

Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba aliulizwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kufunga Jumatatu akasema: “Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku ulioteremshwa kwangu [Unabii]”.  [Imaam Muslim]

 

Lengo letu hapa si kueleza yafanywayo katika siku hiyo na kwanini yanafanywa, bali ni kueleza njia sahihi zilizothibiti zinazopaswa kudhihirisha mapenzi ya umpendaye. Na mapenzi ya kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanayotakikana na ambayo yanamridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni kutekeleza yale aliyotuamrisha kuyafanya, na kuyaacha yale aliyotukataza kuyatenda. Pia kujipamba na yote aliyokuja nayo na aliyokuwa amepambika nayo.

 

Iweje usome Barzanji na kuimba kwa madaha na umsifie Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uzuri na urefu wa ndevu zake na hali wewe wanyoa au kuzichonga mistari kama ramani kwa kuwaiga wanamuziki na wacheza mipira?

 

Iweje utaje na kuimba sifa za uaminifu, ukweli, uadilifu wake kwa wake zake (Radhwiya Allaahu ‘anhunna), na hali wewe ni khaini, muongo na mwenye kunyanyasa wake zako au kutoa mapenzi zaidi na haki zaidi kwa mmoja na wengine huwajali?

 

Iweje Mawlid kwako ni ‘Ibaadah na Swalah huzitekelezi kwa wakati au huziswali kabisa?

 

Iweje wayatukuza mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na unazibeza na kuzipuuza Sunnah zake?

 

Hayo hayawezi kuwa mapenzi. Na mifano ni mingi tunayoiona kwa wenye kusherehekea hayo Mawlid na kuyaadhimisha.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

  

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٢﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi (mmeshakuwa) ni Waislamu kamili. [Aal ‘Imraan: 102]

 

Tuitazame vizuri qadhiyah hii muhimu sana nayo ni “Kumtii na Kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

 

Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemchagua Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumpatia Unabii na Utume na Akateremshiwa Kitabu (Qur-aan) na Hikma (Sunnah) na Akaamrishwa kufuata aliyoteremshiwa na kufikisha ujumbe kutoka kwa Allaah. Alisimama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufikisha ujumbe na kutekeleza amana. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

كَمَا أَرْسَلْنَا فِيكُمْ رَسُولًا مِّنكُمْ يَتْلُو عَلَيْكُمْ آيَاتِنَا وَيُزَكِّيكُمْ وَيُعَلِّمُكُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُعَلِّمُكُم مَّا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ ﴿١٥١﴾

Kama Tulivyomtuma kwenu Rasuli anayetokana na nyinyi, anawasomea Aayaat Zetu na anakutakaseni na anakufunzeni Kitabu na Hikmah (Sunnah), na anakufundisheni mambo ambayo hamkuwa mkiyajua. [Al-Baqarah: 151]

 

Kitabu hapa ina maana ya Qur-aan na Hikma ni mafunzo yake Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Allaah Amemshuhudia yeye kuwa ni mkweli na ameshikamana vilivyo kwa amri Zake (Allaah) kama Alivyomshuhudilia kwa uongofu katika nafsi Yake na kuwa yeye Anawaongoza wanaomfuata. Allaah Anasema:

 

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا ۚ مَا كُنتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿٥٢﴾صِرَاطِ اللَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِلَى اللَّـهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ﴿٥٣﴾

Na hivyo ndivyo Tulivyokuletea Ruwh (Qur-aan) kutoka amri Yetu. Hukuwa unajua nini Kitabu wala iymaan, lakini Tumeifanya ni Nuru, Tunaongoa kwayo Tumtakaye miongoni mwa waja Wetu. Na hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka. Njia ya Allaah Ambaye ni Vyake Pekee vyote vilivyomo mbinguni na vyote vilivyomo ardhini. Tanabahi! Kwa Allaah Pekee yanaishia mambo yote. [Ash-Shuwraa: 52-53]

 

Na hiki ni cheo na daraja ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Dini. Yeyote atakayemuamini, hivyo amemuamini Allaah na yeyote atakayemtii basi amemtii Allaah. Kwa ajili ya hili, Allaah Amewaamrisha waja wake kumtii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Akawalazimisha wao kufuata amri Zake na kusadikisha habari Anazotupasha, na Akatutahadharisha kutomhalifu wala kumuasi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

لَّا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُم بَعْضًا ۚ قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا ۚ فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

Msifanye wito wa Rasuli baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Kwa yakini Allaah Anawajua miongoni mwenu wale wanaoondoka kwa kunyemelea. Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo. [An-Nuwr: 63]

 

Allaah Akajaalia kuwa kumtii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni faradhi ya lazima kwa kila anayemuamini Allaah, wala hakujaalia kwa muumini khiyari kwa amri yoyote baada ya kuwa Allaah na Nabiy Wake wamepitisha. Allaah Anasema:

 

 وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab: 36]

 

Anasema Allaah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَوَلَّوْا عَنْهُ وَأَنتُمْ تَسْمَعُونَ﴿٢٠﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na Rasuli Wake; na wala msijiepushe nazo (amri za Rasuli) na hali nyinyi mnasikia.  [Al-Anfaal: 20]

 

Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) :

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَلَا تُبْطِلُوا أَعْمَالَكُمْ﴿٣٣﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wala msibatilishe ‘amali zenu. [ Muhammad: 33]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾

Sema: Mtiini Allaah na mtiini Rasuli. Mkigeukilia mbali, basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa tu nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa. Na mkimtii mtaongoka; na hapana juu ya Rasuli isipokuwa ubalighisho bayana. [An-Nuwr: 54]

 

Na Anasema tena Allaah kwa yule mwenye kumuasi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 

 وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٤﴾

Na yeyote atakayemuasi Allaah na Rasuli Wake na akataadi mipaka Yake Atamuingiza motoni, ni mwenye kudumu humo na atapata adhabu ya kudhalilisha. [An-Nisaa: 14]

 

Amebainisha Allaah baada hii amri ya kumtii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni sababu ya uongofu na rehma, kama alivyobainisha Aliyetukuka ya kwamba hakuna kufaulu kwa waja na wala 'kunali saada' (kupata furaha) kwao wao katika ahadi isipokuwa kwa kufuata maagizo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtii.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na semeni kauli nyofu ya haki. Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakughufurieni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu. [Al-Ahzaab: 70-71]

 

Na Anasema Allaah:

 

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٣﴾

Hiyo ni mipaka ya Allaah. Na yeyote atakayemtii Allaah na Rasuli Wake Atamuingiza Jannaat zipitazo chini yake mito, watadumu humo, na huko ndiko kufuzu kukubwa. [An-Nisaa: 13]

 

Allaah Amefanya wajibu juu ya waumini kurudisha mambo na mizozano yao kwa Allaah na Nabiy Wake. Na Akajaalia Aliyetukuka kuwa hilo ni katika Imani na ulazima wake. Na Akasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa: 59]

 

Kama hivyo hivyo Alivyowajibisha Allaah kwa Waumini kurudi kwa Kitabu chake na Sunnah za Nabiy Wake. Ameifanya hukumu ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wajibu kufuatwa na kuisalimisha nafsi kikamilifu kwa hukumu yake. Na Akajaalia hilo ni katika ulazima wa mtu kuwa na Imani, pale aliposema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [An-Nisaa: 65]

 

Allaah Ametuamrisha kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa anayotuamrisha na kuacha anayotukataza. Amesema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

  ۚ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

Na lolote analokupeni Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Hashr: 7]

 

Katika Hadiyth zifuatazo ambazo zinatupatia mwelekeo wa mada hii yetu. Amepokea Al-Bukhaariy kuwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Ummah wangu wote utaingia Jannah isipokuwa kwa anayekataa”. Pakasemwa: “Na ni nani atakayekataa, ee Rasuli wa Allaah?” Akasema: “Mwenye kunitii mimi ameingia Jannah na anayeniasi amekataa”.

 

Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote atakayenitii mimi basi amemtii Allaah, na anayeniasi mimi amemuasi Allaah [Al-Bukhaariy].

 

Na hivyo hivyo, kama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyowaamuru Waislamu kumtii, amewaonya wasitoke katika Sunnah zake wala kuzipuuza.

 

Amesema katika Hadiyth ya Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na Muslim kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ya kwamba: “Yeyote atakayekengeuka kutoka katika Sunnah zangu si katika mimi”.

 

Na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kuzua katika jambo letu hili (la dini) ambalo halipo basi litarudishwa” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na katika riwaya ya Muslim: Yeyote atakayefanya amali ambayo haina hukumu yetu basi itarudishwa”.

 

Usikose kusoma maudhui nyingine hapa chini kuhusiana na Mawlid,

 

 

Mawlid: Historia Yake, Hukmu Na Kauli Za 'Ulamaa

 

 

Ee Rabb wetu! Tujaalie ni wenye kusikiliza maneno na utupatie hima na moyo wa kuyafuata yaliyo mazuri na mema. Ee Rabb wetu! Tujaalie ni wenye kufuata Sunnah na kumtii Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kauli na matendo.

 

 

 

Share