Nasaha Za Imaam Sufyaan Ath-Thawriy (رحمه الله)

 

 

Nasaha Za Imaam Sufyaan Ath-Thawriy (رحمه الله)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Miongoni mwa Nasaha za Imaam Sufyaan Ath-Thawriy (Rahimahu-Allaah) ni kauli zake zifuatazo:

 

 

1. Kuwa mkweli wakati wote na kila mahali. Jiweke mbali na uongo na udanganyifu, na usikae pamoja na watu waongo na wadanganyifu, kwani kufanya matendo yote haya ni madhambi makubwa.

 

 

2. Ndugu yangu, jihadhari na riyaa (kujionyesha) aidha katika khutbah au matendo yako, kwa sababu riyaa ni shirki.

 

 

3. Usiwe ni mwenye kujiona, hata ikiwa ni kwa 'amali nzuri kumbuka kuwa haitopanda mbinguni kama 'amali hiyo itakuwa na majivuno yoyote ndani yake.

 

 

4. Chukua Dini yako kutoka kwa yule ambaye ni mwangalifu na mwenye dhati kuhusiana na uongozi wa Dini. Mfano wa ‘Aalim (Mwanachuoni) ambaye si mwangalifu kuhusu Dini yake, ni kama mfano wa daktari ambaye ni mgonjwa. Hali kadhalika, ikiwa mtu mwenyewe hawezi kutibu ugonjwa wake, basi vipi atawezeje kutibu magonjwa ya wengine?

 

Kwahiyo, kama mtu si mwenye kujali na kustawisha kithabiti dini yake, vipi basi ataweza kujali juu ya dini na ustawi wa wengine?

 

 

5. Ndugu yangu, Dini yako si kingine zaidi kuliko mwili na damu yako (yaani, unapaswa kujali Dini yako vizuri, kwa sababu kama sivyo, mwili wako na damu ndivyo vitakuja kulipa fidia kwa adhabu ya Allaah).

 

 

6. Lia juu ya wasiwasi wa nafsi yako, na kuwa ni mwenye huruma juu ya hilo. Ikiwa hutokuwa na huruma juu ya nafsi yako, basi huruma haitojionyesha juu yake.
 

 

7. Keti kwenye kundi ambalo wanakunasihi na wasio na tamaa ya dunia hii na wanaokuhimiza wewe kuweka matumaini zaidi katika Aakhirah. Kuwa makini (muangalifu) sana kukaa na watu wa kidunia ambao huongelea mara kwa mara kuhusu masuala ya kidunia. Watu wa namna hiyo wataharibu ustawi na umakinifu wa dini yako na watachafua moyo wako.

 

 

8. Kumbuka kifo mara nyingi, kama jinsi unavyomuomba Allaah mara kwa mara Akughufurie madhambi yako yaliyopita.

 

 

9. Muombe Allaah Al-‘aafiyah (kubakika salama, amani na hifadhi ya kila shari, fitnah za dunia na Dini) kwa ajili ya uhai wako uliobaki.

 

 

10. Ndugu yangu, boresha tabia nzuri na njema. Usifanye kitendo ambacho ni kinyume na Jamaa'ah, kwa ajili ya wema na usalama ni matokeo ya wewe kuwa kwa amani na Jamaa'ah.

 

 

11. Yeyote mwenye kufanya juhudi daima kwa ajili ya dunia hii ni kama mfano wa mtu ambaye anajenga nyumba moja na kuharibu nyingine (kwa sababu anajenga ufanisi kwa ajili yake mwenyewe katika dunia hii, wakati yeye anaharibu mafanikio katika Aakhirah).

 

 

12. Toa nasaha za dhati kwa kila Muislamu ambaye anakuuliza swali kuhusiana na Dini yake. Na usiwe kamwe ni mwenye kuficha ushauri mzuri kwa mtu yeyote yule ambaye anakuuliza juu ya jambo litalomuelekeza katika radhi za Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa).

 

 

13. Ikiwa utampenda ndugu yako (Muislamu) kwa ajili ya Allaah, basi mpatie kutoka kilichoko kwako mwenyewe na mali yako.

 

 

14. Jiweke mbali na mambo ya mijadala, malumbano, ugomvi, na migogoro. Kinyume chake utakuwa khasimu kwa watu, utakuwa muasi na utajenga uadui na watu.

 

 

15. Kuwa na subira wakati wote na kila mahali, kwa kuwa uvumilivu unaongoza kwenye uadilifu na uadilifu unaongoza katika Jannah (Pepo).

 

 

16. Usiwe ni mwenye hasira na kununa, kwa kuwa hizo hisia mbili zinasababisha uovu, na uovu unaongoza motoni.

 

 

17. Usihojiane na ‘Ulamaa. Kwa kufanya hivyo itamfanya yeye aweze kukuchukia na hatimaye kukutenga.

 

 

 

18. Jiwekee nafasi ya kuwatembelea ‘Ulamaa (na kujifunza kutoka kwao) kwa kuwa ni rahmah kufanya hivyo. Kinyume chake cha kujiweka mbali nao, ni kajitwika ghadhabu ya Allaah ('Azza wa Jalla). Bila shaka, ‘Ulamaa ni hazina za Manabii ('Alayhimus-Salaam) na pia ndiyo warithi wao.

 

 

19. Jiweke mbali na anasa za ulimwengu na vitu visivyokuwa na faida, na matokeo yake Allaah ('Azza wa Jalla) Atakuwezesha kuona makosa na kasoro za dunia hii.

 

 

20. Kuwa mtu mwenye Wara' (kujiweka mbali na maasi na yenye shaka na kuwa na taqwa),  Atafanya kisimamo chake cha uwajibikaji kiwe ni rahisi kwake.

 

 

21. Acha mambo mengi yenye mashaka (utata) katika Dini yako, na badala yake yabadilishe kwa kufanya au kufuata mambo yasiyo na mashaka au na utata,  matokeo yake ni kwamba utabaki ukiwa salama katika Dini yako.  

 

 

22. Amrisha wenzio kufanya mema na kataza yaliyokuwa maovu. Kwa kufanya hivyo utapendwa na Allaah ('Azza wa Jalla).

 

 

23. Chukia watu waovu na pambana na mashaytwaan (wa ki binadaam na wa majini).

 

 

24. Kama unataka kuwa mwenye nguvu (wa iymaan), basi usijigambe na cheka kidogo pindi unapopata vitu kadhaa kwenye hii dunia.

 

 

25. Jishughulishe sana na kuitumikia Aakhirah. Ukifanya hivyo Allaah ('Azza wa Jalla) Atakutosheleza kwa kila jambo lako linalohusiana na dunia hii (hata liwe kubwa kiasi gani).

 

 

26. Muombe Allaah ('Azza wa Jalla)  Al-‘afwa wal ‘Aafiyah  (usalama kwenye Dini yako na dunia).

 

 

27. Ukikusudia (ukinuia) kufanya kitu kwa ajili ya Aakhirah  yako – mathalan kama kutoa Zakaah, Swadaqah n.k. - Basi jihimize kufanya hivyo haraka kabla ya shaytwaan hajakushawishi na usiweze tena kufanya ‘amali hiyo.

 

 

28.  Usiwe ni mwenye kula sana (kwa kupitiliza), ambapo ukawa sasa unafanya kazi kidogo zaidi ya unavyokula. Kwa sababu hilo ni lenye kuchukiza.  

 

 

29. Usile ovyo bila ya kuwa na njaa, na usile mpaka wakati utapokuwa na njaa. Na usijaze tumbo kila wakati ukaja kuwa kama maiti, ikasababisha kutokumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla)  wakati wa uhai wako.  

 

 

30. Punguza kutumbukia katika makosa.

 

 

31- Pokea msamaha (kwa wanaokukosea)  na wasamehe wanokukosea.

 

 

31. Kuwa mfano wa ambaye watu hutarajia mambo mema kutoka kwako; na mtu ambaye watu wanajihisi wana amanii na salama kwako kutokana na  na maovu.  

 

 

32. Usimchukie yeyote ambaye ni mwenye kumtii Allaah ('Azza wa Jalla) .

 

 

33-Kuwa mwenye rahma  kwa watu wote na kwa wale haswa ambao wanakutegemea.

 

 

33. Usikate undugu (Swillatur-Rahim). Unga mahusiano mazuri na wale ambao wamejitenga mbali nawe.

 

 

34. Wasamehe waliokudhulumu; utaona natija yake kwamba (In Shaa Allaah) utakuwa pamoja na Maswahaba na  Manabii na miongoni mwa Shuhadaa (Peponi).

 

 

35. Usiwe ni mwenye kutembea sokoni mara sokoni (madukani), kwa kuwa watu wengi huko (wauzaji na wanunuzi) ni kama mbwa mwitu waliovaa nguo za watu. Soko mara nyingi ndio maeneo ya shaytwaan. Shaytwaan wa kibin Aadam na wa majini. Na ikiwa kutakuwa hakuna budi ila kwenda basi ni wajibu juu yako kuamrisha mema na kukataza maovu. Lakini jua ya kuwa hutoona kingine zaidi ya maovu huko. Simama upande mmoja wa soko na uanze kuwalingania watu:

 

لا إلهَ إلاّ اللّه وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُلْـكُ ولهُ الحَمْـد، يُحْيـي وَيُميـتُ  وَهُوَ حَيٌّ لا يَمُـوت، بِيَـدِهِ الْخَـيْرُ وَهوَ عَلىَ كلّ شيءٍ قَدِيرٌ.

 

Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah  hali ya kuwa Peke Yake, Hana mshirika, ni Wake Ufalme na ni Zake Himdi,  Anahuisha na Anafisha, Naye ni Hai Asiyekufa, kheri iko mikononi Mwake, na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.”

 

 

36. Usiingie katika ugomvi na watu wa dunia hii katika mambo yao ya kidunia. Matokeo yake, Allaah ('Azza wa Jalla)  Atakupenda na watu wa duniani watakupenda.

 

 

37. Kuwa mnyenyekevu.

 

 

38. Wakati uko na afya njema fanya matendo mema, utaruzukiwa usalama na afya njema (ya kimwili na utulivu wa roho) kutoka kwa Aliye juu.

 

 

39. Kuwa mwenye kusamehe, utapata mambo yote unayotaka.

 

 

40. Kuwa mwenye rahmah na rahmah ya kila kitu itakushukia.    

 

 

41. Ndugu yangu, usiache siku yako, usiku wako au masaa yako yapite huku ukiwa kwenye mambo ya upuuzi yasiyokuwa na faida. Tumia muda wako kwa faida yako mwenyewe  kwa ajili ya Siku ya kiu. (Siku ya Qiyaamah).

 

 

42. Ndugu yangu, kiu chako hakitokatika siku hiyo ya Qiyaamah isipokuwa ikiwa Ar-Rahmaah Atakuwa radhi na wewe. Na huwezi kupata radhi Zake Siku hiyo isipokuwa ikiwa wewe ni mtiifu kwake.

 

 

43. Fanya khayraat (mambo ya kheri mengi) kwa kuwa yana athari ya kukujongeza karibu zaidi na Allaah ('Azza wa Jalla).

 

 

44. Kuwa mkarimu, na makosa yako yatafunikwa, na Allaah ('Azza wa Jalla) Atakuwekea wepesi katika kisimamo cha uwajibikaji (hiyo siku ya Qiyaamah) pia Atakuondolea khofu.

 

 

45. Tenda mengi mema Allaah ('Azza wa Jalla) Atakufanya uhisi furaha na kustarehe katika kaburi lako.

 

 

46. Jiepushe na yaliyoharamishwa na hivyo basi utaweza kuionja ladha ya iymaan.

 

 

47. Shikmana na ukae na wenye taqwa na watu wema, Allaah ('Azza wa Jalla) Atakutengenezea mambo yako ya Dini.   

 

 

48. Taka ushauri kwa watu wenye taqwa wenye kumkhofu Allaah.

 

 

49. Harakisha kutenda mema na Allaah ('Azza wa Jalla) Atakulinda wewe kutokana na kumuasi.

 

 

50. Mdhukuru  Allaah ('Azza wa Jalla) mara nyingi, na matokeo yake Allaah ('Azza wa Jalla) Atakufanya usiwe mwenye tamaa na  hii dunia.

 

 

51. Kumbuka kifo mara kwa mara, na matokeo yake Allaah ('Azza wa Jalla) Atakufanyia wepesi mambo yako ya dunia.

 

 

52. Fanyia kazi (kuchuma kwa ajili ya) Jannah, matokea yake Allaah Atakusaidia kumtii.

 

 

53. Kuwa ni mwenye khofu sana na Jahannam, na matokeo yake Allaah ('Azza wa Jalla) Atakufanyia sahali kwako uweze kuwa na subira katika mitihani yote ya maisha haya ya duniani."
 

 

[Historia Ya Sufyaan Ath-Thawriy, uk. (176-181)]

 

 

Share