004-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ni Wajibu Kwa Nani?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

004-Swalaah Ni Wajibu Kwa Nani?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swalaah ni wajibu kwa mwenye akili, aliyebaleghe mwanamume au mwanamke, au muungwana na mtumwa.

 

1- Ama akili, hii ni sharti ya wajibu wa Swalaah kwa mtu. Swalaah si wajibu kwa mwendawazimu kwa Ijma’a kutokana na kauli yake Rasuli Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam: ((Kalamu imenyanyuliwa kwa watatu: Aliyelala mpaka aamke, mtoto mpaka abaleghe, na mwendawazimu mpaka akili iwe timamu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (4398), An-Nasaaiy (6/156), Ibn Maajah (2041) na wengineo].

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na mtu ambaye akili yake imepotea kwa sababu ya ugonjwa, au kwa kupotewa na fahamu au kwa kutumia dawa halali. Kiilivyo ni kwamba aliyepotewa na fahamu na mfano wake, anakuwa hana akili na hatambui lolote. Hukmu kwa huyu inakuwa haipo na wakati wote huo halazimikiwi na Swalaah. Na kama atazindukana akawa na akili katika wakati ambao anaweza kuswali baada ya kujitwaharisha, basi itambidi aswali.

 

Ama mtu aliyelewa, au aliyelala au aliyesahau mpaka Swalaah ikampita, hawa (hasa) itawabidi walipe Swalaah zilizowapita kutokana na Neno Lake Ta’alaa:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا))

((Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho. Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi mtayammam (ikusudieni) ardhi safi ya mchanga, pakeni nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kughufuria)). [ An Nisaa (4:43)]

 

Allaah Mtukufu Hakumruhusu mlevi kuswali mpaka akili yake iwe sawa na akijue anachokisema. Na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Akisahau mmoja wenu Swalaah, au akalala ikampita, basi aiswali anapoikumbuka)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (684)].

 

Haya ndiyo waliyoyasema Maalik na Ash-Shaafi’iy [isipokuwa wao wametofautisha kati ya ulevi wa kukusudia na wa kutokukusudia]. Na haya haya ndiyo aliyoyasema Ibn Hazm na kukhitariwa na Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah) ya kwamba ikiwa akili itamwondoka kwa kujipiga ganzi au kunywa dawa ya kulewesha kwa hiari yake mwenyewe, basi ni lazima alipe, na kama si kwa khiyari yake, basi si lazima alipe.  [Haashiyatud Dusuwqiy (1/184), Mughnil Muhtaaj (1/131), Al-Muhallaa (2/233-234) na Al-Mumti’i (2/18)]

 

2- Ama kubaleghe, hii ni sharti ya wajibu wa Swalaah bila upinzani. Swalaah si wajibu kwa mtoto mpaka abaleghe kutokana na dalili yenye kuonyesha kwamba kalamu ya makalifisho haifanyi kazi kwa mtoto kama ilivyotangulia katika Hadiyth.

 

·       

Kumfundisha Kijana Mdogo Swalaah Na Kumwamuru

 

Kijana mdogo hata kama si wajibu kwake kuswali, lakini hata hivyo ni lazima baba yake amwamuru kuswali anapofikia umri wa miaka saba, na ampige kumtia adabu kama ataacha anapofikia miaka kumi ili aizoee kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwamrisheni kijana mdogo kuswali akiwa na miaka saba, na mpigeni akiiacha akiwa na miaka kumi)). [Swahiyh kwa nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (494) na At-Tirmidhiy (407) toka kwa Sibrah bin Ma’abad. Ina Hadiyth mwenza iliyopokelewa na ‘Abdullaah ‘Umar]

 

Hii ndio rai yenye nguvu ya Jamhuri ya Maulamaa; Hanafi, Ash- Sha’afi’i na Hanbali. Ama Maalik, yeye ameichukulia amri hii katika Hadiyth kama jambo zuri tu la Sunnah. [Haashiyat Ibn ‘Aabidiyn (1/234), Ad-Dusuuqiy (1/186), Mughnil Muhtaaj (1/131) na Kash-Shaaful Qinaa (1/225).

 

Na hili ikiwa litaswihi kwao katika kauli yake Rasuli ((Waamrisheni)), basi halitosihi katika kauli yake ((na wapigeni)), kwa kuwa kupiga ni kumtia mtu adabu, nalo haliendani na jambo lililosuniwa. Inavyoonekana ni kuwa imewachanganya amri ya kumwamuru aswali na kumpiga naye bado hajakalifishwa!!

 

Jawabu: Hilo litakuwa wajibu endapo kama kungelikuwepo usawa, na hapa hauko. Mzazi yuko upande wa wajibu kwa kuwa ni mukallaf, na mtoto wa chini ya miaka kumi hayuko upande huu. Kutokuwepo ulazima kwa mtoto hakumaanishi kwamba mzazi pia hana ulazima, bali ni lazima ampige,  lakini mtoto naye hapati dhambi kwa kuacha Swalaah. [Naylul Awtwaar (1/369-370) kwa mabadilisho madogo. Tizama As Saylul Jarraar (1/156)]

 

·       

Tanbihi

 

Baadhi ya Mafuqahaa wameufanya Uislamu kuwa ni sharti ya kumwajibikia mtu Swalaah. Wanasema: “Si wajibu kwa kafiri wa asili, na kafiri huyu anaposilimu, haamuriwi kuzilipa Swalaah. Na kutowajibishiwa kwa kafiri kunakwenda kinyume na yale yaliyoswihi katika usuul ya kwamba makafiri  wanaamuriwa kufuata Uislamu. Hivyo basi ni wajibu kwao, na wao wataadhibiwa huko aakhirah kwa kuiacha.” [As Saylul Jarraar (1/155)]

 

Ash-Shaafi’iy na Hanbal wameeleza kwamba Swalaah haimlazimu kafiri wa asili ulazima wa kutakwa aswali hapa duniani kwa kuwa Swalaah kwake haiswihi, lakini ataadhibiwa aakhirah kwa kuiacha mbali na adhabu ya ukafiri wake, kwa kuwa lau angesilimu, basi angeweza kuswali. [Mughnil Muhtaaj (1/130) na Kash-Shaaful Qinaa (1/222)]

 

Na juu ya msingi wa haya, khilafu na wao inakuwa ni ya kilafudhi kwa maana kwamba Swalaah ni lazima kwa kafiri ingawa haiswihi, na hivyo basi Uislamu unakuwa ni sharti ya kuswihi Swalaah na si sharti ya wajibu wa Swalaah. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Ninasema: “Kwa mujibu wa Aayah, kafiri anaposilimu haamuriwi kuzilipa Swalaah. Na kwa kuwa yeye haamini kwamba ni wajibu, na akafanya kusudi kutoswali na Swalaah zikapita bila ya udhuru, basi hawezi kuzilipa kama utakavyokuja uhakiki wa hilo.”

 

·       

Idadi ya faradhi

 

Swalaah zilizofaradhishwa mchana na usiku ni tano. Nazo ni Adhuhuri, alasiri, Magharibi, ‘Ishaa na Alfajiri. [Hii ni kwa mujibu wa maneno ya Jamhuri ya Maulamaa. Abu Haniyfah na Maulamaa wa Kihanafi wamesema: “Witr ni wajibu pamoja na Swalaah Tano”. Ufafanuzi wake utakuja].

 

Ufaradhi wa Swalaah hizi umethibiti kwenye Qur-aan, Sunnah na Ijma’a, nao unajulikana na wote, na anayeupinga ni kafiri.  [Al-Badaai-’i (1/91), Al-Fawaakihu Ad-Dawaaniy (1/192), Mughnil Muhtaaj (1/121), na Al-Mughniy (1/370)]

 

1- Imepokelewa toka kwa Abu Raziyn amesema: “Naafi’i bin Al-Azraq alijibishana na Ibn ‘Abbaas akamuuliza: Je, unazipata Swalaah tano katika Qur-aan?”. Ibn ‘Abbaas akajibu ndio, kisha akamsomea (( فسبحان الله حين تمسون )): Magharibi na ‘Ishaa‘, ((وحين تصبحون)) Alfajiri, ((وعشياً )) Alasiri, ((وحين تُظهرون )), Adhuhuri.  [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabariy kwenye “At-Tafsiyr” (20/21), na Ibn Al-Mundhir kwenye “Al-Awsatw” (2/322), na Al-Bayhaqiy kwenye “Al-Kubraa” (1/359) na At-Twabaraaniy kwenye “Al-Kabiyr” (10/304)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Twalha bin ‘Ubaydullaah akisema: “Bedui alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Nieleze, ni Swalaah zipi ambazo Allaah Amenifaradhia?” Akasema: ((Ni Swalaah Tano mchana na usiku)). Akauliza: “Je, kuna zingine?”. Akasema: ((Hapana, ila za kujitolea za Sunnah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (46) na Muslim (11)].

 

3- Imepokelewa na Anas bin Maalik akisema: “Swalaah hamsini zilifaradhishwa kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku wa Israa, kisha zikapunguzwa mpaka zikabakia tano, kisha pakanadiwa: “Ee Muhammad! Hakika neno halibadilishwi Kwangu, na wewe utapata hamsini kwa hizi tano”. [Hadiyth Swahiyh: Al-Bukhaariy kaifanyia “ikhraaj” mfano wake (349) na Muslim (162) kwa urefu]

 

·       

Idadi ya rakaa

 

Ibn Al-Mundhir amesema kwenye Al-Awsatw (2/318):

 

“Maulamaa wote wanasema kwamba Swalaah ya Adhuhuri ni rakaa nne. Kisomo kwenye Swalaah hii ni cha sauti ya chini, na hukaliwa vikao viwili vya tashahhudi, na kila kimoja kinakuja baada ya rakaa mbili. Idadi ya rakaa za Alasiri ni nne kama Swalaah ya Adhuhuri na kisomo chake ni kwa sauti ya chini, na hukaliwa vikao viwili vya tashahhudi, na kila kimoja kinakuja baada ya rakaa mbili. Idadi ya rakaa za Swalaah ya Magharibi ni tatu. Katika rakaa mbili za mwanzo, kisomo ni kwa sauti ya juu na katika rakaa ya tatu, kinakuwa kwa sauti ya chini. Katika rakaa mbili za mwanzo kuna kikao cha tashahhudi, na katika rakaa ya mwisho pia kuna kikao. Idadi ya rakaa za Swalaah ya isha ni nne. Katika rakaa mbili za mwanzo, kisomo ni kwa sauti ya juu na katika rakaa mbili nyingine, kinakuwa kwa sauti ya chini. Hukaliwa vikao viwili vya tashahhudi, kila kikao katika kila rakaa mbili. Idadi ya rakaa za Swalaah ya Alfajiri ni rakaa mbili. Kisomo ni cha sauti ya juu katika rakaa zote mbili na hukaliwa kikao kimoja tu cha tashahhudi.

 

Hii ni faradhi kwa mkazi. Ama msafiri, faradhi yake ni rakaa mbili isipokuwa Swalaah ya Magharibi. Ufaradhi wa Swalaah hii kwa msafiri ni sawa na ufaradhi wa mkazi”.

 

 

 

Share