005-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Nyakati Za Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

005-Nyakati Za Swalaah

 

 

Waislamu wanakubaliana kwamba Swalaah tano zina nyakati zake ambazo ni lazima ziswaliwe katika nyakati hizo. Asili ya hili ni Kauli Yake Ta’alaa:

((فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتً))

((Mtakapomaliza Swalaah, mdhukuruni Allaah msimamapo, na mkaapo na mnapolala ubavuni mwenu Mtakapopata utulivu, simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu)). [ An Nisaa (4:103) ]

 

 Na ufuatao ni uainisho wa mipaka ya nyakati hizi na ubainisho wa alama zake:

 

[1] Swalaah Ya Adhuhuri

 

Adhuhuri ni pale jua linapopindukia upande wa Magharibi toka katikati ya mbingu. Swalaah hii inakuwa ni wajibu wakati wa Adhuhuri unapoingia, nayo huitwa pia vile vile “Al-Uwlaa” kwa  kuwa ndiyo Swalaah ya kwanza kabisa ambayo Jibriyl alimswalisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

[Al-Miswbaahul Muniyr, Al-Majmu’u (3/24) na Al-Mughniy (1/372)]

Huitwa pia “Al-Hajiyrah” kutokana na yaliyopokelewa toka kwa Abu Barzah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiiswali Al-Hajiyrah wanayoiita Al-Uwlaa wakati jua linapopinduka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (541)].

 

Mwanzo wake:

 

Ni pale jua linapopindukia upande wa Magharibi toka katikati ya mbingu. Maulamaa wote wamekubaliana hilo kutokana na kuthibiti habari toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba aliswali Adhuhuri wakati jua lilipopinduka kama ilivyo katika Hadiyth ya Barzah iliyotangulia.

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri ya kuwa Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((Wakati wa Adhuhuri ni pale jua linapopinduka na kivuli cha mtu kikawa sawa na kimo chake madhali Alasiri haijaingia. Na wakati wa Alasiri ni kabla ya jua kuwa la kinjano. Na wakati wa Swalaah ya Magharibi ni kabla ya kupotea wekundu, na wakati wa Swalaah ya isha ni mpaka nusu ya usiku. Na wakati wa Swalaah ya Alfajiri, ni kuanzia Alfajiri inapotokea madhali jua halijachomoza, na jua linapochomoza basi usiswali, kwani huchomoza kati ya pembe mbili za shaytwaan)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (612)].

 

Mwisho wake:

 

Maulamaa wametofautiana kuhusiana na wakati huu. Kauli sahihi zaidi ni ile isemayo kuwa mwisho wake ni pale urefu wa kivuli cha kitu unapokuwa mfano wa kimo chake bila kuhesabu urefu wake wakati jua linapopinduka. [Kila kitu kinakuwa na kivuli kabla ya Adhuhuri, kisha kivuli hiki hupungua, halafu huanza tena kuongezeka. Na hiki ndicho kivuli cha kupinduka jua na ndio mwanzo wa wakati wa Adhuhuri. Kivuli kikizidi na kupindukia kipimo hiki na kuwa sawa na urefu wa kitu, unakuwa ndio mwisho wa wakati wa Adhuhuri].

 

Wakati huu unakuwa ndio wakati wa kuingia Alasiri. Hii ndiyo rai yenye nguvu zaidi ya Jamhuri ya Maulamaa. Abu Haniyfah amekwenda kinyume na rai hii. Anasema kuwa mwisho wa Adhuhuri ni pale kivuli cha kitu kinapokuwa mara mbili yake bila kuhesabia urefu wa kivuli wakati jua linapopinduka. [Mawaahibul Jaliyl (1/382), Mughnil Muhtaaj (1/121), Al-Mughniy (1/371), Al-Awsatw (2/327), Badaai’u Asw-Swanaai’i (1/123) na Al-Aswl (1/144)]

Jamhuri ya Maulamaa wametoa dalili kwa haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyotangulia isemayo: “Wakati wa Adhuhuri ni pale jua linapopinduka na kikawa kivuli cha kila mtu kama kimo chake madhali Alasiri haijaingia”.

 

2- Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah Al-Answaariy isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka akaswali Adhuhuri wakati jua lilipopinduka, na kivuli kikawa kiasi cha kamba ya kiatu. Halafu aliswali Alasiri wakati kivuli kilipokuwa kiasi cha kamba ya kiatu na kivuli cha mtu. Kisha aliswali Magharibi wakati jua lilipokuchwa. Halafu aliswali ishaa pale wekundu ulipotoweka, kisha akaswali Alfajiri wakati ilipochomoza Alfajiri. Na siku iliyofuatia, aliswali Adhuhuri wakati kivuli kilipokuwa sawa na kimo cha mtu, kisha aliswali Alasiri wakati kivuli cha mtu kilipokuwa mara mbili yake kiasi cha mwendo wa kutoka Al-‘Unuk hadi Dhul Hulayfah kwa mtu aliyepanda mnyama. Halafu aliswali Magharibi wakati jua lilipozama, kisha aliswali ishaa mpaka theluthi ya usiku au nusu ya usiku (shaka ya msimuliaji), halafu aliswali Alfajiri kukipambazuka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1/261). Angalia “Al-Irwaa” (1/270)].

 

Hadiyth hii inachukulika kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimaliza Adhuhuri wakati kivuli cha kila kitu kilipokuwa sawa nacho. Na katika siku ya kwanza, aliianza Alasiri wakati kivuli cha kila kitu kilipokuwa sawa nacho. Na hapa hakuna maingiliano kati ya nyakati mbili. [Naylul Awtwaar (1/374)]

 

Na hatuwezi kusema kwamba kivuli cha kitu kinapokuwa mfano wake ndio kwamba wakati wa Alasiri umeingia na wakati wa Adhuhuri haujatoka, bali kunabakia baada ya hapo muda wa kiasi cha rakaa nne kinachofaa kuswaliwa Adhuhuri na Alasiri kama walivyosema baadhi yao. [An-Nawawiy ameinasibisha kauli hii kwa Maalik kwenye Sharhu Muslim. Pia ameisimulia toka kwa Maalik katika Bidaayatul Mujtahid (1/125) ambapo pia Ibn Al-Mundhir (2/327) kainasibisha kwake kwamba amesema: “Wakati wa Adhuhuri unatoka” !!]

 

Tuliyoyaeleza yanatiliwa nguvu na Hadiyth ya Abu Qataadah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika kupoteza wakati ni kwa yule ambaye hakuiswali Swalaah mpaka ukaingia wakati wa Swalaah nyingine)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (595) na Muslim (681) katika Hadiyth ndefu.

 

·       

Faida:

 

- Wakati wa Adhuhuri unaweza kujulikana kwa njia ya kuhesabu masaa. Ni kuhesabiwa wakati wa baina ya jua linapochomoza mpaka pale linapokuchwa, na wakati wa Adhuhuri utakuwa katikati ya masaa hayo kamili.

 

- Imesuniwa kuharakisha kuswali Adhuhuri mwanzoni mwa wakati wake kutokana na Hadiyth ya Jaabir bin Samurah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Adhuhuri linapopinduka jua kuelekea Magharibi”. Pia Hadiyth ya Abu Barzah iliyotangulia nyuma kidogo.

 

- Imesuniwa kuichelewesha joto linaposhitadi kutokana na Hadiyth ya Anas aliyesema: “Baridi ilipokuwa inashitadi, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwahisha Swalaah, na joto linaposhitadi huikawiza”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (618), Abu Daawuud (403) na Ibn Maajah (673)].

 

Na Hadiyth ya Abu Dharri aliposema: “Tulikuwa safarini pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mwadhini akataka kuadhini akamwambia: ((Subiri papoe)). Kisha akataka kuadhini akamwambia: ((Subiri papoe)) mara mbili hivi au tatu mpaka tukaona kivuli cha vilima. Halafu akasema: ((Ukali wa joto unatokana na mwako na pumuo la Jahannam, na joto linaposhitadi basi kawisheni Swalaah papoe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (906), na mfano wake iko kwa Al-Bukhaariy (534) na Muslim (615) toka kwa Jaabir].

 

Mpaka wa kukawisha Swalaah hadi joto lipungue unatofautiana kwa mujibu wa hali. Cha kuangaliwa ni muda usiachiwe mpaka mwisho wa wakati.

 

[2] Swalaah Ya Alasiri

 

Alasiri ni saa za mwisho wa mchana jua linapokuwa jekundu na huitwa “Al-‘Ashiy”. Swalaah ya Alasiri huitwa “Swalaah ya Kati” na inakuwa ni wajibu wakati wake unapoingia.

 

Mwanzo wake:

 

Ni pale kivuli cha kitu kinapokuwa mfano wake kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri kinyume na rai mashuhuri ya Abu Haniyfah. Yeye ameufanya mwanzo wake ni pale kivuli cha kitu kinapokuwa mara mbili yake!! Hadiyth zilizotangulia kuhusiana na wakati wa Adhuhuri, zinaipa nguvu kauli ya Jamhuri. [Jawaahirul Ikliyl (1/32), Mughnil Muhtaaj (1/121), Al-Mughniy (1/375) na Fat-hul Qadiyr (1/195)]

 

Mwisho wake:

 

Udhahiri wa Hadiyth umegongana kuhusiana na mwisho huo. Mgongano huo unaonekana katika:

 

-  Hadiyth ya Jaabir wakati Jibriyl alipomswalisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kwamba, katika siku ya kwanza, aliswali Alasiri wakati kivuli cha kitu kilipokuwa mfano wake. Na katika siku ya pili, aliswali Alasiri wakati kivuli cha kitu kilipokuwa mara mbili yake. Kisha akasema: “Wakati ni kati ya nyakati hizi mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imeshaelezwa nyuma]

 

Na haya ndiyo aliyoyasema Ash-Shaafi’iy [lakini hili ni katika wakati wa khiyari] na Maalik katika moja ya riwaya mbili. [Bidaayatul Mujtahid (1/126) na Al-Umm (1/73)]

 

- Hadiyth Marfu’u ya ‘Abdullaah bin ‘Amri isemayo: ((Wakati wa Alasiri ni kabla ya jua kuwa la kinjano)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa nyuma kidogo] Kayasema haya Maalik, Abu Thawr na riwaya toka kwa Maalik. [Bidaayatul Mujtahid (1/126), Al-Mughniy (1/376) na Al-Awsatw (2/331). Kuna kauli sita zilizosimuliwa katika mas’ala haya]

 

Pia Hadiyth mwenza ya Abu Musa kuhusiana na kisa cha mtu aliyeuliza kuhusu nyakati za Swalaah akituambia: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Alasiri siku ya kwanza jua likiwa limenyanyuka, na katika siku ya pili mwisho wa Alasiri. Akaondoka baada ya Swalaah huku muulizaji akisema: “Jua limekuwa jekundu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (614), Abu Daawuud (395) na An-Nasaaiy (1/260)].

 

- Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mwenye kuipata rakaa ya Alasiri kabla ya jua kuchwa, basi kaipata Alasiri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (579) na Muslim (163/608)].

 

Is-Haaq na Ahlu Adh-Dwaahirwakasema: “Mwisho wa wakati wake ni kabla ya kuchwa jua kwa rakaa moja”. [Bidaayatul Mujtahid (1/126), Al-Awsatw (2/332) na Al-Muhalla]

 

Ninasema: “Kile ambacho dalili za Hadiyth hizi zote na zinginezo zinakutania, ni kuchukuliwa Hadiyth ya Jibriyl kwamba inabainisha wakati wa khiyari, Hadiyth ya Ibn ‘Umar inabainisha wakati wa kujuzu, na Hadiyth ya Abu Hurayrah inabainisha wakati wa udhuru na dharura. Tunasema: Mwisho wa wakati wa khiyari ni kivuli cha kitu kuwa mara mbili yake na huendelea mpaka jua linapokuwa njano, na hukirihishwa kuchelewesha kupindukia muda huo bila ya udhuru kutokana na Hadiyth ya Anas aliyesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hiyo ni Swalaah ya mnafiki. Hukaa akilichunga jua mpaka linapokuwa kati ya pembe mbili za shaytwan, ndipo hapo husimama akiidonoa nne, na hamdhukuru Allaah isipokuwa kidogo tu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (622), Abu Daawuud (409), At-Tirmidhiy (160) na An-Nasaaiy (1/254)].

 

Na kama kuna udhuru au dharura, itajuzu kuiswali bila ukaraha kabla jua kuchwa kwa kiasi cha rakaa moja. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

Imesuniwa Kuharakisha Alasiri

 

1- Kwa Hadiyth ya Anas isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Alasiri jua likiwa angavu limenyanyuka. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (550) na Muslim (621)]

 

Mtu akaenda hadi Al-’Awaaly akarudi na jua bado limenyanyuka”. Al-‘Awaaly ni umbali wa maili nne toka Madiynah.

 

2- Imepokelewa toka kwa Raafi’i bin Khudayj akisema: “Tulikuwa tukiswali Alasiri pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha tukachinja ngamia, tukamgawa mafungu kumi. Halafu tukapika na tukaila nyama yake kabla jua halijakuchwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2485) na Muslim (625)].

 

Pia inasisitiziwa kuiharakisha katika siku yenye mawingu kwa kuwa ni aghalabu watu kutatizikiwa na wakati. Muda ukivutwa, basi wakati unaweza kuponyoka, au jua likawa njano kabla ya Swalaah. Imepokelewa toka kwa Abul Mulayhi akisema: “Tulikuwa pamoja na Buraydah vitani katika siku iliyofunga mawingu akasema: Iwahisheni Swalaah ya Alasiri, kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuacha Swalaah ya Alasiri, basi amali zake zimepomoka)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (553), An-Nasaaiy (1/83) na Ahmad (5/349)].

 

Hamasisho La Kuilinda Swalaah Ya Alasiri Na Matahadharisho Ya Kuiacha Katika Qur-aan na Hadiyth.

 

1- Allaah Anasema:

((حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ))

((Shikamaneni na Swalaah na khaswa Swalaah ya katikati (Alasiri), na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu)). [ Al-Baqarah (2:238)]

 

“Swalat Al-Wustwaa” ni Swalaah ya Alasiri kwa mujibu wa kauli sahihi kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposhughulishwa na makundi: ((Wametushughulisha tukaghafilika na “Swalat Al-Wustwaa: Swalaah ya Alasiri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2931) na Muslim (627) na tamko ni lake].

 

2- Imepokelewa na Abu Buswrah Al-Ghaffaariy (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha Alasiri huko Al-Makhmasw. Akasema: ((Hakika Swalaah hii ilifaradhishwa kwa waliopita kabla yenu wakaipoteza. Mwenye kuihifadhi, basi atakuwa na malipo mara mbili, na hakuna Swalaah baada yake mpaka nyota ichomoze)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (830)].

 

3- Imepokelewa toka kwa ‘Ammaarah bin Ru’uyah (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hatoingia motoni yeyote aliyeswali kabla ya kuchomoza jua na kuchwa)). Yaani Alfajiri na Alasiri. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (634)].

 

4- Hadiyth Marfu’u ya Buraydah tuliyoieleza nyuma isemayo: ((Mwenye kuacha Swalaah ya Alasiri, basi amali yake imepomoka)).

 

Ibn Al-Qayyim amesema: [As-Swalaatu wa Hukmu Taarikihi uk. 43-44]

 

“Kinachoonekana katika Hadiyth – na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi muradi wa Rasuli Wake - ni kuwa kuacha ni kwa aina mbili: Ima kuacha kabisa Swalaah, na hili hupomosha amali yote, au kuacha baadhi ya siku, na hili hupomosha amali ya siku hizo tu. Kuporomoka kiujumla ni kwa kuacha kabisa, na kuporomoka kisehemu ni kwa kuacha siku fulani. Ikiwa pataulizwa: Vipi amali zitapomoka bila mtu kuritadi? Itajibiwa kuwa Qur-aan, Sunnah na nukuu toka kwa Maswahaba zinaonyesha kwamba mabaya hupomosha mema kama ambavyo mema huondosha mabaya. Allaah Amesema:

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالْأَذَىٰ كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ صَفْوَانٍ عَلَيْهِ تُرَابٌ فَأَصَابَهُ وَابِلٌ فَتَرَكَهُ صَلْدًا ۖ لَّا يَقْدِرُونَ عَلَىٰ شَيْءٍ مِّمَّا كَسَبُوا ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ))

((Enyi walioamini! Msibatilishe swadaqah zenu kwa masimbulizi na udhia kama yule ambaye anatoa mali yake kwa kujionyesha kwa watu wala hamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama jabali juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa ikaliacha tupu. Hawana uwezo juu ya lolote katika waliyoyachuma. Na Allaah Haongoi watu makafiri)). [Al-Baqarah (2:264)]

 

Na Anasema:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَأَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ))

((Enyi walioamini! Msipandishe sauti zenu juu ya sauti ya Nabiy, na wala msiseme naye kwa sauti ya juu, kama mnavyosemezana wenyewe kwa wenyewe kwa sauti za juu; zisije zikaporomoka ‘amali zenu nanyi hamhisi)). [Al-Hujuraat (49:2)]

 

Ninasema: “Hili ni kwa yule aliyeitelekeza kabisa na kupuuzilia mbali fadhila ya wakati wake naye ana uwezo wa kuiswali. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

5- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhumaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anayepitwa na Swalaah ya Alasiri, ni kama aliyepokonywa ahli wake na mali yake)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (552) na Muslim (626/200)].Yaani ni kama vile amebakia pweke bila mali wala ahli. Na hii ni taswira ya kupomoka amali kwa sababu ya kuiacha kwa namna tuliyoielezea. [As-Swalaat cha Ibn Al-Qayyim (44)]

 

Au inaweza kusemwa: Mtu atahadhari isimpite kama anavyotahadhari kupotea ahli zake na mali yake.

 

[3] Swalaah Ya Magharibi

 

Neno “Al-Maghrib” lina maana ya wakati jua linapokuchwa, au sehemu linapokuchwia, au Swalaah inayoswaliwa wakati huu. [Al-Miswbaahul Muniyr na Kash-Shaaful Qinaa (1/253)]

Al-Maghrib huitwa pia vile vile Al-’Ishaa, lakini hili ni makruhu kutokana na kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo katika Swahiyh Mbili:

((Angalieni Mabedui wasiwazidini nguvu juu ya jina la Swalaah yenu ya Magharibi)). Mabedui huiita ‘Ishaa.

 

Mwanzo wake:

 

Ni pale jua linapokuchwa, likapotea na machweo yakakamilika kwa mujibu wa Ijma’a ya Maulamaa. Hili huonekana wazi kwenye majangwa, na hujulikana kwenye miji kwa kutoweka mwangaza juu ya vilele vya milima, na giza kuanza kutanda toka mashariki na kuchomoza nyota. [Al-Badaai’u (1/123), Al-Mughniy (1/381), na Naylul Awtwaar (2/5,6)]

 

Mwisho wake:

 

Maulamaa wamehitalifiana juu ya kauli mbili:

 

Ya kwanza: Magharibi ina wakati mmoja tu baada ya kuchwa jua kwa kiasi cha mtu kutawadha, kujisitiri, kuadhini na kuqimu. Hii ni rai ya Maalik, Al-Awzaa’iy na Ash-Shaafi’iy. [Bidaayatul Mujtahid (10/126), Al-Majmu’u (3/28) na Al-Awsatw (2/335)]

 

Hoja yao ni Hadiyth iliyotangulia ya Jibriyl kumswalisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambapo katika siku ya kwanza na ya pili, aliswali Magharibi wakati mmoja pale jua lilipokuchwa. Pia yaliyosimuliwa na Suwayd bin Ghafalah anayesema kwamba amemsikia ‘Umar bin Al-Khattwaab akisema: “Swalini Swalaah hii nailhali njia zina mwanga, yaani Magharibi”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (2092) na Ibn Abu Shaybah (1/329)]

 

Ya pili: Mwisho wake ni kutoweka wekundu. Ni kauli ya Ath-Thawriy, Ahmad, Is-Haaq, Abu Thawr, Abu Haniyfah na Mafuqahaa wa Kihanafi, na baadhi ya Mafuqahaa wa Kishaafii. An-Nawawiy kaikubali na Ibn Al-Mundhir kaikhitari. [Bidaayatul Mujtahid (1/127), Al-Majmu’u (3/28) na Al-Awsatw (2/337)]

 

Ni kauli sahihi, na dalili juu ya usahihi wake ni:

 

1- Hadiyth Marfu’u ya Ibn ‘Amri: ((Na wakati wa Swalaah ya Magharibi ni kabla ya kupotea wekundu)).

 

2- Hadiyth ya Abu Muusa kuhusu mtu aliyeuliza nyakati za Swalaah isemayo: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Magharibi siku ya kwanza wakati jua lilipokuchwa, na siku ya pili mwishoni mwa Magharibi mpaka wekundu ulikuwa unakurubia kuondoka”. Tushaitaja nyuma kama ilivyo Hadiyth ya Buraydah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (613), At-Tirmidhiy (152), na An-Nasaaiy (1/337)].

 

3-Hadiyth ya Zayd bin Thaabit kwamba alimwambia Marwaan: “Vipi wewe unasoma katika Swalaah ya Magharibi Suwrah ndogo za Aayah fupi fupi?! Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma Suwrah ndefu zaidi ya Suwrah mbili ndefu”. Yaani Al-A’araaf. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (764), An Nasaaiy (2/170) na Ahmad (5/188)].

 

Na kisomo cha Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kilikuwa bayana, herufi kwa herufi na tartiyl pamoja na utulivu katika rukuu na sijdah. Na hii inaonyesha kwamba wakati wa Magharibi unaendelea mpaka wekundu unapopotea.

 

4- Hadiyth ya Anas (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Chajio kikitengwa, basi anzeni kula kabla ya Swalaah ya Magharibi, na wala msiharakishe Swalaah mkaacha mlo wenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (672) na Muslim (557)].

 

Na katika tamshi la Hadiyth ya ‘Aaishah: ((Swalaah ikiqimiwa na chajio kikatengwa, basi anzeni kwanza kula)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (671)].

Hadiyth iko wazi kwamba inajuzu kuichelewesha Swalaah ya Magharibi mpaka baada ya kula baada ya kuingia wakati wake.

 

5- Hadiyth ya Mu’aadh isemayo kwamba alikuwa akiswali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Magharibi, kisha hurejea kwa watu wake akawaswalisha. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (711) na Muslim (465)].

 

Imesuniwa Kuiharakisha

 

1- Imepokelewa toka kwa Raafi’i bin Khudayj akisema: “Tulikuwa tunaswali Magharibi pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mmoja wetu anapoondoka, anaweza kuona sehemu ya kuangukia mshale wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (559) na Muslim (637)].

 

2- Imepokelewa toka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Umma wangu hautaacha kuwa juu ya kheri – au juu ya Uislamu- madhali hawakuichelewesha Magharibi mpaka nyota zikaingiliana)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (414) na Ahmad (4/147)]

 

[4] Swalaah Ya ‘Ishaa

 

‘Ishaa ni pale giza linapoingia kuanzia Magharibi hadi linaposhitadi “atamah”. Swalaah ya ‘Isha imeitwa hivi kwa vile huswaliwa katika wakati huu. Pia huitwa “‘Ishaa ya mwisho” kama alivyosema Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwanamke yeyote aliyejifukiza manukato, basi asitoke kuswali nasi ‘Ishaa ya mwisho)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (444), Abu Daawuud (4175) na An-Nasaaiy (5128)].

 

Huitwa pia vile vile “Atamah” kama anavyosema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Lau wangelijua yaliyomo katika ‘Atamah na Alfajiri, basi wangeziendea hata kwa kutambaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (615,721) na Muslim (437)].

 

Lakini kuitwa kwa jina hilo kumeelezewa kuwa ni makruhu katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar anayesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Angalieni sana mabedui wasije kuwazidieni nguvu katika jina la Swalaah yenu. Jueni kwamba inaitwa ‘Ishaa, nao huichelewesha mpaka giza linaposhitadi ili kukama ngamia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (228), An-Nasaaiy (1/270) na Ibn Maajah (705)].

 

Kuiita ‘Ishaa “atamah” ni kinyume cha ubora kwa mujibu wa Hadiyth hii kama wanavyoona hivi akina Maalik na Ash-Shaafi’iy na kukhitariwa na Ibn Al-Mundhir. Ibn Hajar katilia nguvu.

 

Mwanzo wake:

 

Maulamaa wote (isipokuwa wachache mno) wanasema kwamba mwanzo wa wakati wa ‘Ishaa ni pale unapopotea wekundu. Lakini wamehitilafiana kuhusu maana ya neno “Ash-Shafaq”. [Angalia Al-Awsatw (2/339-342) na Al-Majmu’u (3/44-45)]

 

Jamhuri wanasema maana yake ni wekundu, lakini Abu Haniyfah na Al-Awzaa’iy wanasema ni weupe baada ya wekundu.

 

Ninasema: “Maana ya kwanza ndio sawa, kwa kuwa lililothibiti ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali wakati wekundu ulipotoweka. Mtaalamu wa taaluma ya mapambazuko na machweo anajua kwamba weupe haupotei isipokuwa katika theluthi ya kwanza ya usiku. [Ukweli huu umenukuliwa katika Naylul Awtwaar (2/16) toka kwa Ibn Sayyidi An Naas katika Sharh At-Tirmidhiy. Kisha ninamwona Ibn Rushd katika Bidaayatul Mujtahid (1/127) akiukadhibisha]

 

Na imethibiti katika Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba wao walikuwa wakiswali baina ya pale wekundu unapopotea mpaka theluthi ya kwanza ya usiku.” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (569) na Muslim (218)]

 

Mwisho  wake:

 

Maulamaa wamehitilafiana kuhusu hili katika kauli tatu mashuhuri:

 

Ya kwanza: Ni mpaka mwisho wa usiku. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy katika madhehebu mapya [isipokuwa hili kwake ni wakati wa khiyari. Na kwenye Al-Ummu ameeleza kwamba theluthi inapopita, basi Swalaah nayo imepita]. Pia wamelisema hili Abu Haniyfah na Maalik. [Al-Awsatw (2/343), Al-Ummu (1/74), Bidaayatul Mujtahid (1/128) na Al-Majmu’u ( 3/42)]

 

Dalili yao ni Hadiyth ya Jibriyl kumswalisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Inasema kwamba katika siku ya pili, aliiswali na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika theluthi ya usiku.

 

Ya pili: Ni mwisho wa nusu ya usiku. Waliosema hivi ni Ath-Thawriy, Ibn Al-Mubaarak, Is-Haaq, Abu Thawr, Aswhaab Ar Ra-ay na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu yake ya zamani. [Isipokuwa Aswhaab Ar Ra-ay wanasema kwamba inatosheleza baada yake pamoja na ukaraha. Ama Ash-Shaafi’iy, yeye anaona kwamba ni wakati wa khiyari, na Swalaah haimpiti mtu mpaka Alfajiri]. Pia Ibn Hazm kasema hivi.

 

Dalili yao ni Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amri iliyotajwa mara nyingi isemayo: “Wakati wa ‘Ishaa ni mpaka nusu ya kati ya usiku”, pamoja na Hadiyth ya Anas isemayo: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikawiza Swalaah ya ‘Ishaa mpaka nusu ya usiku”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (572)].

 

Aidha, ‘Umar bin Al-Khattwaab alimwandikia Abu Musa Al-Ash’ariy akimwambia: “Na uswali ‘Ishaa katika wakati wa baina yako na kati ya theluthi ya usiku, na kama utaichelewesha, basi hadi nusu ya usiku, na wala usiwe katika wenye kughafilika”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik, At-Twahaawiy na Ibn Hazm kwa Sanad Swahiyh kama ilivyo kwenye Tamaam Al-Minnah (uk. 142)].

 

Ya tatu: Mwisho wake ni kuchomoza Alfajiri ya kweli (walau bila ya dharura). Waliosema hivi ni ‘Atwaa, Twaawus, ‘Ikrimah na Daawuud Adh-Dwaahiriy. Nayo imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Abu Hurayrah. Ibn Al-Mundhir ameikhitari. [Al-Awsatw (2/346) na Bidaayatul Mujtahid (1/128)]

 

Dalili yao ni:

 

1- Hadiyth Marfu’u ya Qataadah: ((Hakika kupoteza wakati ni kwa yule ambaye hakuiswali Swalaah mpaka ukaingia wakati wa Swalaah nyingine)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshatajwa nyuma].

 

2- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Lau kama si kuuchelea umma wangu uzito, ningeliichelewesha ‘Ishaa mpaka nusu ya usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Itakuja muda si mrefu].

 

Wanasema: “Hii ni dalili ya kwamba hakuna ubaya kwa aliyeichelewesha hadi nusu ya usiku. Na kama Rasuli angeliichelewesha kisha akatoka kwenda kuwaswalisha baada ya nusu ya usiku, basi Swalaah ingelikuwa ni baada ya sehemu ya nusu ya usiku. Na ikiwa ni hivyo, basi inathibiti kwamba wakati wake ni mpaka Alfajiri inapotoka”. [Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (2/346)]

 

3- Hadiyth ya ‘Aaishah: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichelewa usiku ule mpaka sehemu kubwa ya usiku ikapita na watu Msikitini wakalala. Halafu alitoka akaswali, kisha akasema: ((Hakika huu ndio wakati wake lau kama si kuuchelea umma wangu uzito)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (219) na An-Nasaaiy (1/267)].

 

Hadiyth Yenye Uzito Zaidi

 

Hadiyth yenye nguvu zaidi kati ya Hadiyth zilizotangulia ambayo ina ainisha mwisho wa Swalaah ya ‘Ishaa, ni Hadiyth ya ‘Abdullah bin ‘Amri isemayo: ”Wakati wa ‘Ishaa ni mpaka nusu ya kati ya usiku”. Ash-Shawkaaniy kaipa uzito lakini kaufanya mwisho wa wakati wa khiyari. Ama wakati wa kujuzu, huu unaendelea mpaka Alfajiri kwa kuitegemea Hadiyth iliyotangulia ya Qataadah isemayo: “Kiilivyo ni kuwa wakati wa kila Swalaah huendelea mpaka unapoingia wakati wa Swalaah nyingine isipokuwa Swalaah ya Alfajiri, Swalaah hii ina hali pekee toka kwenye ujumuishi huu kwa Ijma’a”.

 

Ninasema: [Nimefaidika hapa kwa maneno ya Al-‘Allaamah Al-Albaaniy kwenye Tamaam Al-Minnah (uk. 141). Maana yake imenukuliwa toka kwa Ibn Hazm (3/178)]

 “Ama kutolea dalili kwa Hadiyth ya Qataadah ya kwamba wakati wa ‘Ishaa unaendelea mpaka kuchomoza Alfajiri, hapa pana neno. Kwa kuwa Hadiyth haibainishi nyakati za Swalaah, na wala haikuja kwa ajili ya hilo, bali imekuja kwa ajili ya kubainisha madhambi ya mwenye kuichelewesha Swalaah kwa makusudi mpaka wakati wake ukatoka, sawasawa ikiwa inafuatiliwa na Swalaah nyingine kama Alasiri pamoja na Magharibi, au haifuatiwi kama Alfajiri na Adhuhuri.  Linaloonyesha hilo ni kuwa Hadiyth imekuja kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri wakati ilipompita Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake wakiwa wamelala safarini. Maswahaba wakahisi vibaya mno kutokea hilo kwao, na hapo Rasuli akaisema Hadiyth hiyo. Na lau kama makusudio ni hayo waliyoyasema ya kuwa wakati wa kila Swalaah unaendelea mpaka unapoingia wakati wa Swalaah nyingine, basi maneno yangelibainisha wazi kwamba wakati wa Alfajiri unaendelea mpaka wakati wa Adhuhuri, lakini wao hawasemi hivyo. Na kwa ajili hiyo, wamelazimika kuivua Swalaah ya Alfajiri na kuiweka kando. Na uvuaji huu juu ya tuliyoyabainisha kutokana na sababu ya Hadiyth, unakuja kuibatilisha, kwa kuwa Hadiyth imekuja kuhusiana na Swalaah ya Alfajiri tu. Basi vipi iwezekane kuivua Swalaah hii?! Kiukweli ni kuwa Hadiyth haikuja kwa ajili ya kuainisha, bali kwa ajili ya kukataza kuitoa Swalaah nje ya wakati wake kiujumla”.

 

Ninasema tena: “Ama Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo: “Mpaka sehemu kubwa ya usiku ikapita”, makusudio yake hapa si sehemu kubwa sana. Ni lazima tuifanye taawili hii kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika huu ndio wakati wake)). Na haijuzu makusudio ya kauli hii yawe ni baada ya nusu ya usiku, kwa kuwa hakuna Mwanachuoni yeyote aliyesema kwamba ni bora kuichelewesha hadi baada ya nusu ya usiku. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy]

 

[Na haibakii kwa wanaosema kwamba wakati wa ‘Ishaa unaendelea mpaka Alfajiri (sawasawa kwa khiyari au kwa lazima) isipokuwa Hadiyth ya Anas asemaye: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliichelewesha Swalaah ya ‘Ishaa mpaka nusu ya usiku, kisha akaiswali..” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (572)]

 

Ikiwa itaswihi kuchukulia kwamba alimaliza kuiswali nusu ya usiku, basi neno lake “kisha akaiswali” linakuwa ni la wapokezi wao wenyewe, na kama si hivyo, neno linakuwa ni neno lao. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

Imesuniwa Kuichelewesha ‘Ishaa

 

Kuna Hadiyth nyingi Swahiyh zilizozungumzia kuhusu kuichelewesha ‘Ishaa. Hili ndilo linalofuatwa na Maulamaa wengi katika Maswahaba na Taabi’iyna. [Tabyinul Haqiyqah cha Az-Zayla’iy]

 

Kati ya Hadiyth hizo ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Lau kama si kuuchelea umma wangu uzito, ningeliwaamuru waicheleweshe ‘Ishaa mpaka theluthi ya usiku au nusu yake)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (167), Ibn Maajah (691) na Ahmad (2/245)]

 

Hikma yake ni kuwa wakati huu una faida zaidi kwa kuwa akili ya mtu haishughulishwi na mambo yenye kumsahaulisha kumdhukuru Allaah Ta’alaa, na pia hukata gumzo la usiku. Lakini hata hivyo, kuichelewesha huenda kukapelekea kuipunguza jamaa na kuwakimbiza watu. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaichelewesha wakati, na wakati mwingine anaiharakisha, yaani akiwaona watu wamekusanyika huikarakisha, na akiwaona wamekawia huichelewesha. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (560) na Muslim (233) toka Hadiyth ya Jaabir].

 

Ni Karaha Kulala Kabla Yake Na Kupiga Gumzo Baada Yake

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Barzah isemayo kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichukia kulala kabla ya ‘Ishaa, na kuzungumza baada yake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (568) na Muslim (237)].

 

Sababu ya ukaraha wa kulala kabla ya Swalaah ya ‘Ishaa ni kuchelea kupitiwa na usingizi wakati wake ukatoka, au likawafungulia watu mlango wakashindwa kuiswali kwa jamaa. [Tabyinul Haqaaiq (1/84), Al-Fawaaqihu Ad Dawaaniy (1/197) na Naylul Awtwaar (2/18)]

 

Ama ukaraha wa kuzungumza baada yake, ni kuwa hilo linaweza kuwafanya watu wakeshe halafu wakapitwa na Alfajiri, au ili wasije kuzungumza maneno yasiyo na faida ambayo si vizuri mtu kuyamalizia kwayo siku yake, au kwa kuwa mtu anaweza kupitwa na ‘ibaadah za usiku. Swalaah inatakikana iwe ndiyo amali bora anayoimalizia kwayo mtu amali zake, na usingizi ni nduguye mauti, na mtu huenda akafia usingizini. [As-Saabiq, Al-Majmu’u (3/42) na Mughnil Muhtaaj]

 

Lakini hii ikiwa mazungumzo yenyewe hayana umuhimu. Ikiwa yana umuhimu wa kidini kwa wote au kwa mtu binafsi, au yana faida kwa mtu au maslaha kwa Waislamu, basi hakuna ubaya. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikesha pamoja na Abu Bakr na ‘Umar kwa ajili ya jambo kati ya mambo ya Waislamu. [Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (169) na Ahmad (1/26). Ina mkatiko, na pia Hadiyth wenza].

 

Na katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza na mkewe Maymounah saa moja, kisha akalala. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (190)].

 

[5] Swalaah Ya Alfajiri

 

Asili ya Alfajiri ni “Ash-Shafaq” yenye maana ya mwanga wa asubuhi. Alfajiri mwishoni mwa usiku, ni kama “Ash-Shafaq” mwanzoni mwake.

 

Alfajiri ziko za aina mbili: [Al-Badaai-’i (1/122), Mughnil Muhtaaj (1/124), Al-Fawaakih (1/192) na Kash-Shaaful Qinaa (1/255)]

 

Alfajiri ya kwanza (ya bandia), nao ni weupe wa kimstatili unaoonekana kutoka sehemu ya mbingu, kisha hutoweka na kufuatiliwa na kiza. Weupe huu unajulikana kwa Waarabu kama “Mkia wa mbwa mwitu”.

 

Alfajiri ya pili (ya kweli), nao ni weupe kinza wenye kusambaa upeoni, na nuru yake huzidi kuongezeka mpaka jua linapochomoza. Katika Hadiyth Rasuli anasema:

((Angalieni isiwazuieni daku yenu adhana ya Bilaal wala Alfajiri ya kimstatili, lakini Alfajiri yenye kusambaa upeoni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1094), At-Tirmidhiy (706) na tamko ni lake, Abu Daawuud (2346), An-Nasaaiy (2171) na wengineo].

 

Alfajiri hii ya pili ndiyo inayofungamana na hukmu zote, si ya kwanza ya bandia. Na Alfajiri huitwa Swalaah ya Alfajiri kwa kuwa huswaliwa katika wakati huu, na pia huitwa “Swalaatus Subh” na Swalaatul Ghadaat”.

 

Mwanzo wake: Maulamaa wote wanakubaliana kwamba mwanzo wa wakati wa Alfajiri ni kuchomoza Alfajiri ya kweli.

 

Mwisho wake: Na wote wanakubaliana kwamba mwisho wake ni kuchomoza jua.

 

Imesuniwa Kuiharakisha:

Jamhuri ya Maulamaa akiwemo Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq, na Abu Thawr,  wanaona kwamba kuiswali Alfajiri wakati giza bado liko ni bora zaidi kuliko kuiswali jua likianza kuwa la kinjano. [Al-Mudawwanah (1/56), Al-Awsatw (2/377), Mughnil Muhtaaj (1/125), Al-Mughniy (1/394) na Sharhus Sunnah cha Al Baghawiy (1/197)]

 

Hili limesimuliwa toka kwa Makhalifa wanne pamoja na Ibn Mas-’oud. Hoja yao ni:

 

(a) Kwamba habari zinaeleza kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Alfajiri giza likiwa bado lingaliko. Kati ya hizo ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah anayesema: “Wanawake Waumini walikuwa wakihudhuria pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalaah ya Alfajiri wakijifunika mitandio (murutw) yao, kisha hurejea majumbani mwao wanapomaliza Swalaah. Hakuna anayewatambua kutokana na kiza kilichochanganyika na mwanga”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (578) na Muslim (230)]

 

2- Hadiyth ya Abu Barazah Al-Aslamiy asemaye: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali Alfajiri, kisha huondoka, na mtu kati yetu hamjui aliyekaa naye, na alikuwa akisoma Aayah sitini hadi mia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (541) na Muslim (1097)].

 

3- Hadiyth ya Anas toka kwa Zayd bin Thaabit asemaye: “Tulikula daku pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha tukaenda kuswali. Nikauliza: “Kulikuwa na muda gani kati ya daku na Swalaah?” Akasema: “Kiasi cha Aayah 50”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (576) na Muslim (47)].

 

Muda wa kati ya kumaliza daku na kuingia kwenye Swalaah ambayo ni kiasi cha Aayah khamsini, ni kiasi cha wudhuu. Na hili linatuhisisha kwamba aliiswali mwanzoni mwa wakati wa Alfajiri.

 

4- Hadiyth ya Abu Mas-’oud Al-Answaariy asemaye: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Alfajiri mara moja giza likiwa limechanganyika na mwanga, kisha akaswali mara nyingine jua likiwa njano. Kisha baada ya hapo, Swalaah yake ilikuwa ni wakati giza likiwa limechanganyika na mwanga mpaka alipofariki. Hakuswali tena jua likiwa njano”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (394). Asili yake ni kwenye Swahiyh Mbili bila neno “Kisha baada ya hapo, Swalaah yake ilikuwa…”.]

 

(b) Kwamba kuiswali mapema kunaingia ndani ya wigo wa ujumuishi wa Hadiyth zenye kupendezeshea kuharakia kuiswali Swalaah mwanzoni mwa wakati wake. Baadhi yake zitakuja karibuni.

 

(c) Kuiharakia ni kitendo cha Makhalifa Waongofu (Radhwiya Allaahu Anhum). [Angalia athar zilizopokelewa toka kwao katika Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (2/374 na yanayofuatia). Kuswali jua likiwa njano kumesimuliwa pia toka kwa ‘Aliy na ‘Uthmaan]

 

(d) Kwamba baadhi ya Maulamaa kama Ash-Shaafi’iy na Ahmad wanaichukulia maana ya jua kuwa njano juu ya uhakika wa kuchomoza Alfajiri na kuthibiti kwake. Na kwa vile unjano wa jua unabeba maana mbili, Hadiyth zilizothibiti toka kwa Rasuli ambazo hazibebi isipokuwa maana moja tu, zinakuwa ni bora zaidi.

 

Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na Mafuqahaa wa Kihanafi, wanaona kwamba kuswali jua likiwa linjano ni bora zaidi. [Tabyinul Haqaaiq cha Az Zayla’iy (1/82), Sharhu Ma’anil Aathaar (1/184) na Al-Awsatw (2/377)]

 

Wametoa hoja kwa haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya Raafi’i bin Khudayj isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Swalini Alfajiri jua likiwa njano, kwani hilo lina thawabu kubwa zaidi)). [Hadiyth Swahiyh Lighayrih: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (424), At-Tirmidhiy (154), An-Nasaaiy (1/272) na Ibn Maajah (672)].

 

Ibn Hibaan ameijibu hoja hii akisema: “Makusudio ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa neno lake: “Jua likiwa njano” ni katika masiku ya mbalamwezi ambapo weupe wa kuchomoza Alfajiri haubainiki, ili mtu asiswali Swalaah ya Alfajiri mpaka baada ya kupata uhakika wa kuchomoza Alfajiri kwa unjano wa jua. Kwani ikiwa Swalaah itaswaliwa kama tulivyoelezea, inakuwa na malipo makubwa zaidi kuliko kuswaliwa bila ya uhakika wa kuchomoza Alfajiri”. [Swahiyh Ibn Hibaan (4/359-Al-Ihsaan)]

 

2- Hadiyth ya Ibn Mas-’oud kuhusiana na Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huko Muzdalifah isemayo: “Na aliswali Alfajiri siku hiyo kabla ya wakati wake [giza likiwa limechanganyika na mwanga]..”. Wanasema: “Wamezingatia kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Alfajiri giza likiwa limechanganyika na mwanga kabla ya wakati wake ambao Ibn Mas-’oud anaujua, hivyo wakati wake aliouzoea ni jua linapokuwa njano”.

 

Ninasema: “Hili haliko wazi kwa upande wa dalili, kwani kuswali kwake Rasuli Alfajiri giza likiwa limechanganyika na mwanga kabla ya muda wake uliozoeleka, hakupingani na kuwa lililozoeleka pia ni kuswali giza likiwa limechanganyika na mwanga”.

 

Atw-Twahaawiy (Rahimahul Laahu) ambaye ni Mhanafi, amejaribu kuoanisha kati ya dalili za kuswali giza likiwa limechanganyika na mwanga, na kati ya kuswali jua likiwa la njano. Anasema kuwa mtu anaingia kwenye Swalaah mapema, kisha hurefusha kisomo mpaka akaimaliza jua likiwa limeshakuwa njano. [Sharhu Ma’anil Aathaar (1/184)]

 

Ninasema: “Huu ni mwoanisho mzuri. Lakini unatilia nguvu mwelekeo wa Jamhuri ya Maulamaa wa kufadhilisha kuiharakia Swalaah wakati giza likiwa bado limechanganyika na mwanga, kwa kuwa mzozano ni kuhusu wakati wa kuingia kwenye Swalaah, na si wakati wa kuimaliza. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

 

Share