"Mimi Ni Mji Wa Elimu Na ‘Aliy Ni Mlango Wake"

 

Abuu 'Abdillaah

 

 

MASHIA (RAAFIDHWAH) huitumia sana Hadiyth hii: "MIMI NI MJI WA ELIMU NA ‘ALIY NI MLANGO WAKE'', kuitolea kama ni ushahidi wa utukufu wa Khaliyfah wa nne ‘Aliy رضي الله عنه, na kama ndio moja ya hoja yao kuu ya kuwa ‘Aliy رضي الله عنه alikuwa ni bora kuliko Maswahaba wengine na kwamba alistahiki kuwa Khaliyfah wa kwanza baada ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم.

 

HAPA TUTAPATA MASWALI YAFUATAYO NA MAJIBU YAYACHAMBUAYO:

MASWALI:

1. Ni nini makusudio ya Hadiyth ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم, ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake’, basi atakayetaka kuingia katika mji huo na apitie mlango wake.’?

2. Je, hii Hadiyth haimaanishi kwamba njia pekee ya kupata elimu – elimu ya kidini – ni ‘Aliy رضي الله عنه na kwamba njia zingine zote zilizotumika kupata elimu hiyo ni pungufu, na kwa sababu hiyo hazina umuhimu wowote katika Uislamu?

 

MAJIBU:

Kabla ya kutumia Hadiyth kutolea hoja ni lazima kwanza kuangalia kama hiyo Hadiyth imepokewa kutoka kwa Mtume صلي الله عليه وآله و سلم kwa njia (isnaad) sahihi au laa. Kisha baada ya kuhakikisha hivyo tujaribu kuangalia maneno (matni) ya hiyo Hadiyth na kuelewa kwamba yanamaanisha kitu gani. Kuielewa Hadiyth moja ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم kwa maana ambayo itakuwa inapingana na kauli zake zingine nyingi, au ambayo itasababisha mabaya mengi, haiwezi kuwa sahihi. Badala ya hiyo kama kuna maana nyingine ya hiyo Hadiyth ambayo haipingani na kauli zingine za Mtume صلي الله عليه وآله و سلم na ambayo haisababishi baya lolote basi maana hiyo ndiyo itakayokubalika na mtu yeyote mwenye akili timamu.

Kwa kuzingatia kanuni hii inatupasa kwanza tuangalie hadhi ya hii Hadiyth, ‘Mimi ni mji wa elimu’ kwa upande wa Riwaya (elimu ya kuchunguza sanad au mapokezi ya Hadiyth za Mtume صلي الله عليه وآله و سلم Katika vitabu Sahihi vya Hadiyth, Hadiyth hii imepokewa na At-Tirmidhiy peke yake na yeye ameisimulia kwa maneno, ‘Mimi ni nyumba ya hekima na ‘Aliy ni mlango wake’ badala ya ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake’. Raawiy (msimulizi) wake ni ‘Aliy رضي الله عنه mwenyewe. Baada ya kunukuu Hadiyth hii Imaam At-Tirmidhiy anasema yafuatayo kuhusu usahihi wake:

'‘Hii ni Hadiyth Ghariyb na Munkar. Baadhi yao wameipokea hii Hadiyth kutoka kwa Shurayk na hawakumtaja Sunaabihi katika sanad yake. Na hatuijui hii Hadiyth kutokana na Thiqah yeyote isipokuwa Shurayk.’'

Hadiyth Ghariyb, katika Istilahi ya Wanachuoni wa Hadiyth, ni Hadiyth ambayo inategemea mpokezi mmoja tu katika sehemu yoyote ya sanad yake, na Munkar ni Hadiyth ambayo si Ghariyb tu bali mpokezi wake (huyo mmoja) pia ni dhaifu. Kwa hiyo tunajua hadhi ya Hadiyth hii ya At-Tirmidhiy kwa upande wa Riwaya na pia kuitegemea kuweka msingi wote wa Dini ni kiasi gani.

Baada ya At-Tirmidhiy Hadiyth zote zenye maana hii zinategemea kitabu Al-Mustadrak cha Al-Haakim ambacho chenyewe hakihesabiwi katika vitabu vyenye kutegemewa vya Hadiyth. Yeye ananukuu Hadiyth mbili zenye matni tofauti kutoka kwa Ibn ‘Abbaas رضي الله عنه na Jaabir bin ‘Abdullaah رضي الله عنه Riwaya ya Ibn ‘Abbaas رضي الله عنه ni, ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake kwa hiyo mwenye kuukusudia mji huo basi apitie mlango wake’ na Hadiyth ya Jaabir رضي الله عنه ni, ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake kwa hiyo mwenye kutaka kupata elimu basi na apitie huo mlango.’

Al-Haakim amedai kuwa Hadiyth hizi mbili ni Sahihi. Lakini kwa maoni ya wanachuoni wakubwa wa Hadiyth, Hadiyth hizi mbili na Hadiyth zingine zote katika mlango huu ni dhaifu na si zenye kutegemewa. Kuhusu Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas رضي الله عنه Haafidh Adh-Dhahabiy anasema wacha kuwa sahihi, hii Hadiyth ni Mawdhuu’ na maoni yake kuhusu Hadiyth ya Jaabir رضي الله عنه ni, ‘Namshangaa Al-Haakim na ushujaa wake katika kusahihisha Hadiyth hii na Hadiyth zingine batili mfano wake, wakati huyu Ahmad (mmoja katika wapokezi wa Hadiyth hii) ni muongo sana.’

Yahya bin Ma’iyn anasema kuhusu Hadiyth hii, ‘Haina asli yoyote.’ Maoni ya Al-Bukhaariy ni kwamba, ‘Ni Munkar na haina sanad yoyote sahihi.’ An Nawawiy na Jazriy wanaitaja kuwa ni Mawdhuw’ (ya kutungwa). Haijathibiti vilevile kwa Ibn Daqiyq Al-‘Iyd. Ibn Jawziy amejadili kwa kirefu na kuthibitisha kuwa Hadiyth zote zenye maana ya ‘Mimi ni mji wa elimu’ hazina sanad hata moja sahihi.

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba, ni sahihi kiasi gani kutumia Hadiyth ambayo hali ya sanad yake ni hii! Kuamua maamuzi makubwa kama kuchukua elimu kwa Mtume صلي الله عليه وآله و سلم kwa kumpitia ‘Aliy رضي الله عنه peke yake na kuwaacha Maswahaba wengine wote? Ni dhahiri kwamba hayo si maamuzi madogo. Baada ya Qur-aan mwongozo wetu ni maisha na mfano mwema ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم na ni Maswahaba peke yao ambao wanaweza kutuambia miongozo ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم katika nyanja mbalimbali za maisha yalikuwa yapi. Sasa kama tutategemea Hadiyth hii na kumfanya ‘Aliy رضي الله عنه ndiye chanzo pekee cha elimu hiyo, basi bila shaka tutakuwa tunajinyima sehemu kubwa sana ya elimu hiyo iliyonukuliwa na Maswahaba wengine. Je, haiingii akilini kwamba ili tuweze kufanya maamuzi makubwa kama hayo basi tungekuwa na Hadiyth ambayo imetufikia kwa sanad yenye nguvu zaidi na yenye kutegemewa zaidi kuliko Hadiyth hii? Bali ingepasa iwe imenukuliwa kupitia si sanad moja tu bali sanad nyingi sahihi ili kusiwe na shaka kabisa kuhusu usahihi wake.

Tuangalie sasa, jinsi gani Hadiyth hii inapingana na Hadiyth zingine nyingi za Mtume صلي الله عليه وآله و سلم. na matendo yake kama tutaielewa kwa dhahiri ya maneno yake. Mtume صلي الله عليه وآله و سلم aliwatuma Maswahaba wengi kama viongozi wa majeshi yake katika misheni mbalimbali, Aliwateua kuwa magavana wa sehemu mbalimbali wa Dola ya Kiislamu, Aliwateua kukusanya Zaka, Aliwateua kuswalisha Swalah za Jamaa na kuwatuma katika miji tofauti tofauti kwenda kufundisha Uislamu. Haya ni mambo ambayo ni vigumu sana kwa mtu yeyote kuyakataa. Swali ni kwamba, je, kazi zote hizi zilifanywa bila ya hawa Maswahaba kuwa na elimu ya Kidini? Au kwamba hawa Maswahaba wote hawakuwa wanafunzi wa Mtume صلي الله عليه وآله و سلم bali wa ‘Aliy رضي الله عنه? Kama mambo haya mawili si kweli basi ukweli ni kwamba Maswahaba wote hawa walipata elimu kutoka katika ‘Mji wa elimu’ au ‘Nyumba ya Hekima’ na wao wote pia ni milango yake kama ‘Aliy رضي الله عنه.

Vilevile, mtu yeyote aliyesoma Siyrah ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم anajua kwamba kuanzia alivyopewa Utume hadi kufariki kwake Mtume صلي الله عليه وآله و سلم alikuwa akilingania watu katika Uislamu na kuifundisha yeye peke yake. Na mtu yeyote aliyetaka kujua jambo lolote la Uislamu alikuwa akimuuliza Mtume صلي الله عليه وآله و سلم moja kwa moja na kupata jibu. Je, ilishawahi kutokea kwamba Mtume صلي الله عليه وآله و سلم alipata mafunzo fulani ya Uislamu kutoka kwa Allaah kisha akawa amemfundisha ‘Aliy رضي الله عنه peke yake mafunzo hayo na kumuachia yeye peke yake jukumu la kuyafikisha kwa watu wengine? Au, mtu akaja kwa Mtume صلي الله عليه وآله و سلم kumuuliza swali na yeye akamuambia aende kwa ‘Aliy رضي الله عنه au aje kwake kwa kumpitia ‘Aliy رضي الله عنه? Kama yote hayo hayakutokea katika muda wote wa miaka 23 wa Utume basi kauli hii kwamba mlango wa mji wa elimu ni mmoja tu una maana gani?

Al-Haakim mwenyewe ambaye anasisitiza usahihi wa Hadiyth hii amepokea Hadiyth nyingi sana kutoka kwa Maswahaba wengine katika kitabu chake Al-Mustadrak na kuna Hadiyth nyingi tu katika Hadiyth hizo ambazo zina mafunzo na maana ambayo hajanukuu kabisa kutoka kwa ‘Aliy رضي الله عنه. Swali ni kwamba kama Hadiyth hii ilikuwa sahihi kweli kwa Al-Haakim na mlango wa mji wa elimu ulikuwa ni mmoja tu basi milango hii mingine ilitoka wapi na kwa nini aliiendea (milango hiyo)?

‘Aliy رضي الله عنه mwenyewe alikuwa akikanusha madai ya kwamba kuna mambo alifundishwa na Mtume صلي الله عليه وآله و سلم ambayo Mtume صلي الله عليه وآله و سلم hakumfundisha mtu mwingine yeyote. Kuna Hadiyth sahihi katika Al-Bukhaariy, Muslim na Musnad Ahmad zinazosema kuwa ‘Aliy رضي الله عنه alikanusha mara nyingi madai ya watu waliokuwa na fikra kama hizo. alitoa karatasi moja na kuwaambia watu kuwa zaidi ya yaliyoandikwa katika karatasi hii Mtume صلي الله عليه وآله و سلم hakunifundisha mambo yoyote maalumu. Karatasi hiyo ilikuwa na hukmu nne au tano za ki-Fiqhi. Kauli hii ya ‘Aliy رضي الله عنه imenukuliwa kupitia sanad 13 tofauti katika Musnad Ahmad. Tukikusanya Hadiyth zote hizi tunaona kwamba ‘Aliy رضي الله عنه mwenyewe alikanusha mara nyingi na katika nyakati tofautitofauti kwamba Mtume صلي الله عليه وآله و سلم alimfundisha jambo lolote la Uislamu amba lo hakumfundisha mtu yeyote mwingine. Watu wengi sana walimsikia akikanusha madai haya na yamewafikia Wanachuoni kwa kupitia sanad nyingi tofauti kiasi kwamba inakuwa vigumu sana kutia shaka kuhusu usahihi wake. (Angalia Musnad Ahmad (Chapa ya Daar ul Ma’arif Misri) Hadiyth nambari 599, 615, 782, 798, 858, 874, 954, 959, 962, 993, 1037, 1297, 1306 )

Baada ya yote hayo, tukiangalia Hadiyth zingine za Mtume صلي الله عليه وآله و سلم zinazozungumzia fadhila za Maswahaba wengine tunaona ya kuwa Hadiyth hii inapingana nazo zote. Katika Musnad Ahmad na At-Tirmidhiy kuna Hadiyth ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم kwamba Zayd bin Thaabit رضي الله عنه ni mwenye elimu ya mirathi kuliko Maswahaba wengine. Kuhusu Mu’adh bin Jabal رضي الله عنه: Yeye ni mwenye kujua Halaal na Haraam kuliko Maswahaba wote. Kuhusu Ubay bin Ka’ab رضي الله عنه: Yeye ni msomaji bora wa Qur-aan katika Maswahaba.

Katika Musnad Ahmad, ‘Aliy رضي الله عنه mwenyewe anasimulia kauli ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم, ‘Laiti ningetaka kumteua yeyote katika umma wangu kuwa kiongozi bila kumshauri mtu basi ningemteua Ibn Ummi A'bd (‘Abdullaah bin Mas’uwd).’

Katika At-Tirmidhiy kuna riwaya ya Hudhayfah رضي الله عنه, ‘Sijui nitabaki nanyi hadi lini, kwa hiyo wafuateni Abu Bakr na ‘Umar baada yangu.’

Abu Sa’iyd Al-Khudriyy رضي الله عنه anasimulia kwamba Mtume صلي الله عليه وآله و سلم ‘Aliysema, ‘Kila nabii alikuwa na mawaziri wawili mbinguni na wawili ardhini; Mawaziri wangu mbinguni ni Jibriyl na Miykaiyl na ardhini ni Abu Bakr na ‘Umar.’

At-Tirmidhiy amepokea kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir رضي الله عنه kwamba Mtume صلي الله عليه وآله و سلم alisema, ‘Kama kungekuwa na Nabii baada yangu basi angekuwa ‘Umar.’

Al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Sa’ad bin Abi Waqqaas رضي الله عنه kwamba Mtume صلي الله عليه وآله و سلم alimuambia ‘Umar رضي الله عنه, ‘Ewe Mwana wa Khattwaab! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, shetani akikutana nawe njiani basi hubadilisha njia na kupita njia usiyoipita wewe.’

Abu Daawuwd kapokea kutoka kwa Abu Dharr رضي الله عنه kwamba Mtume صلي الله عليه وآله و سلم kasema, ‘Allaah Ameiweka haki katika ulimi wa ‘Umar na yeye (‘Umar) huitamka.’

Al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy رضي الله عنه kwamba Mtume صلي الله عليه وآله و سلم alisema: ‘Niliota jana watu wakiletwa mbele yangu wakiwa wamevaa makanzu makubwa na madogo. Wengine kanzu zao zilikuwa zimefika kifuani, wengine chini zaidi. ‘Umar alivyoletwa alikuwa akiburuza kanzu yake. Maswahaba wakamuuliza Mtume صلي الله عليه وآله و سلم kuhusu tafsiri ya ndoto hiyo. Akasema, ‘Kilichokusudiwa kuwa ni kanzu katika ndoto hiyo ni Dini.’

Hadiyth hizi zimepokewa na Maswahaba wengine. Hebu tuangalie Hadiyth alizozipokea ‘Aliy رضي الله عنه mwenyewe na zilizopo katika vitabu vya Hadiyth vyenye kutegemewa:

Katika Al-Bukhaariy, mtoto wa ‘Aliy رضي الله عنه Muhammad bin Al-Hanafiyyah anasema: ‘Nilimuuliza baba yangu, ‘Ni nani bora baada ya Mtume?’ Akajibu: ‘Abu Bakr.’ Nikasema, ‘Na baada yake?’ Akajibu, ‘Umar.’ Baada ya hapo nikawa na shaka kwamba nikimuuliza tena atasema ‘Uthman kwa hiyo nikasema, ‘Na baada ya ‘Umar ni wewe sio?’ Akajibu, ‘Mimi ni mtu tu wa kawaida katika Waislamu.’’ Jibu hili linafanana kabisa na Siyrah tukufu na safi ya ‘Aliy رضي الله عنه. Ilikuwa kawaida ya mtu mwenye makamu ya juu katika Uislamu kama yeye kuepuka kutaja fadhila zake na badala ya hiyo kujiweka tu katika safu ya Waislamu wa kawaida.

Katika Musnad Ahmad kuna riwaya ya Al-Hasan bin ‘Aliy رضي الله عنه (na riwaya hii iko katika At-Tirmidhiy na Ibn Maajah pia) kwamba baba yake, ‘Aliy رضي الله عنه alisema, ‘Nilikuwa na Mtume صلي الله عليه وآله و سلم wakaja Abu Bakr na ‘Umar. Mtume akasema: ‘Ewe ‘Aliy! Hawa wawili ni viongozi wa watu wazima peponi baada ya Mitume.’’ (Musnad Ahmad Hadiyth nambari 602)

Katika Hadiyth nyingine iliyopokewa na Ahmad, Al-Bazzaar na At-Twabaraaniy kwa sanad sahihi, ‘Aliy رضي الله عنه anasema: ‘Mtume صلي الله عليه وآله و سلم aliulizwa nani atakuwa kiongozi wa Waislamu baada yake? Akajibu: ‘Mkimfanya Abu Bakr kiongozi basi mtamkuta ni muaminifu, mwenye kuupa mgongo pesa (dunia) na mwenye shauku ya Akhera. Mkimfanya ‘Umar kiongozi basi mtamkuta ni mwenye nguvu, muaminifu na haogopi lawama ya mwenye kulaumu kwa ajili ya Allaah na mkimfanya ‘Aliy kiongozi na siwaoni mkifanya hivyo basi mtamkuta mwenye kuongoa, aliyeongoka na atawapeleka katika njia iliyonyooka.’ (Musnad Ahmad Hadiyth nambari 859)

Katika Musnad hiyo hiyo ya Ahmad imesimuliwa, kupitia sanad 26 sahihi, kwamba siku moja ‘Aliy رضي الله عنه alisema juu ya minbar katika khutbah yake moja kwamba baada ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم watu bora wa Ummah huu ni Abu Bakr رضي الله عنه na baada yake ‘Umar رضي الله عنه. Wapokezi wa Hadiyth zote hizi ni Thiqaat (wenye kuaminika) na hakuna aliyejeruhiwa (yaani aliyetolewa makosa). Hadiyth 23 ni sahihi kutokana na elimu ya Mustwalah ul Hadiyth, 2 ni Hasan na moja tu ndiyo Dhwa’iyf. Katika Hadiyth hizo, 12 zimesimuliwa na Abu Juhayfah رضي الله عنه ambaye ni Swahaba na alikuwa ofisa wa Baytul Maal wakati wa Ukhaliyfah wa ‘Aliy رضي الله عنه anasema, ‘Aliy رضي الله عنه alituuliza katikati ya khutbah yake, mnajua mtu bora wa Ummah huu baada ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم ni nani? Mimi nikajibu, ‘Ni wewe ewe Amiyr ul Muuminiyn.’ Akasema, ‘Hapana! Baada ya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم mtu bora katika Ummah huu ni Abu Bakr رضي الله عنه na baada yake ni ‘Umar رضي الله عنه.’’

Mpokezi mwingine ni ‘Abd Khayr Hamdaani ambaye riwaya 13 zinaishia kwake, alipoulizwa, ‘Je, kweli ulimsikia ‘Aliy رضي الله عنه akitamka maneno hayo?’ alisema, ‘Niwe kiziwi kama sikuyasikia kutoka kwenye ulimi wake yeye mwenyewe.’

Mpokezi mwingine ni Ibraahiym An-Nakha’iy anayesema, ‘Alqamah aliupiga minbar wa Msikiti wa Kufah na mkono wake na kusema, ‘Nilimsikia ‘Aliy رضي الله عنه akihutubu juu ya minbar hii na kusema, mtu bora baada ya Mtume alikuwa Abu Bakr na baada yake ‘Umar.’’ (Kusoma Hadiyth hizi angalia Ahmad Hadiyth nambari, 833 – 837, 871 – 878, 880, 909, 922, 932 – 934, 1030 – 1032, 1040, 1051, 1052, 1054, 1055, 1059, 1060 )

Al-Bayhaqiy na Ahmad wamepokea kauli ya ‘Aliy رضي الله عنه, ‘Tulikuwa hatuoni ajabu kwamba Sakina inatamka juu ya ulimi wa ‘Umar.’

Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad wamepokea Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas رضي الله عنه kwamba ‘Umar رضي الله عنه alivyouawa na maiti yake ilivyoletwa na kuwekwa juu ya meza tayari kwa kuoshwa watu waliizingira pande zote na kuanza kumuombea du’aa za kheri. Mtu mmoja akaja kwa nyuma yangu, kaniegemea na akasema, ‘Allaah Akurehemu. Sijawahi kutamani ningekutana na Mola wangu na Amali za mtu yoyote zaidi yako. Natarajia Allaah سبحانه وتعالى Atakuweka pamoja na Masahiba wako wawili (yaani Mtume صلي الله عليه وآله و سلم na Abu Bakr رضي الله عنه) kwani nilikuwa nikimsikia Mtume صلي الله عليه وآله و سلم mara nyingi akisema, Nilikuwepo mahala fulani pamoja na Abu Bakr na ‘Umar, Nilifanya kazi fulani na Abu Bakr na ‘Umar, Nilienda mahali fulani na Abu Bakr na ‘Umar.’’ Ibn ‘Abbaas رضي الله عنه anasema, ‘Nilivyogeuka kutazama ni nani anayesema maneno hayo nikakuta ni ‘Aliy رضي الله عنه.’

Sasa jambo la kuzingatia ni kwamba kama kweli Hadiyth ‘Mimi ni mji wa elimu…’ ni sahihi na ina maana ileile ambayo huchukuliwa, basi tusemeje kuhusu Hadiyth zingine nyingi kuhusu fadhila za Maswahaba wengine zilizowaridi na sanad sahihi zaidi kuliko ya Hadiyth hii? Tuzikatae vipi Hadiyth zote hizo kwa Hadiyth hii ambayo ina sanad dhaifu na yenye mashaka. Kama hatuwezi kuzikataa basi je, tunaweza kuipa Hadiyth hii tafsiri nyingine ili ‘Aliy رضي الله عنه abaki kuwa mlango wa mji wa elimu na pia kauli zingine zote za Mtume صلي الله عليه وآله و سلم na ‘Aliy رضي الله عنه mwenyewe kuhusu Maswahaba wengine yabaki kuwa ya kweli? Kwanza kabisa kuna Hadiyth nyingi sahihi kuhusu fadhila za ‘Aliy رضي الله عنه na wala hakuna upungufu wa Hadiyth hizo katika vitabu vya Hadiyth na kwa hiyo hakuna haja kuleta Hadiyth kama hii ambayo sanad yake ni mbovu kuliko Dhaif kutokana na ‘Ilm ya Mustwalah ul Hadiyth. Kama kuna mtu ambaye atang'ang'ania kuwa hii Hadiyth ni sahihi basi sehemu hii, ‘kwa hiyo mwenye kuukusudia mji huo basi apitie mlango wake’ ya Hadiyth hii si sahihi kabisa kwa sababu inapingana na kauli za Mtume صلي الله عليه وآله و سلم zingine na vilevile na vitendo vya maisha yake yote na pia na kauli zake ‘Aliy رضي الله عنه mwenyewe. Sana sana tunaweza kukubali sehemu ya Hadiyth hii ya kwanza ambayo ni, ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake’ kuwa ni sahihi na hiyo pia si kwa maana ya kwamba mlango wa mji huo ni ‘Aliy رضي الله عنه peke yake bali kwa maana ya kwamba mji huo una milango mingi na ‘Aliy رضي الله عنه ni mlango mmojawapo wa milango hiyo. Maana hii ni sahihi na inakubaliana na kauli na vitendo vya Mtume صلي الله عليه وآله و سلم.

 

WA ALLAAHU A'LAM

 

Share