Ghadiyrul Khum - Katika Qur-aan, Sunnah Na Historia

 

Imefasiriwa Na Muhammad Faraj

 

 

Mashia wanasema kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyestahiki kuwa Khalifa wa Waislam na si Abu Bakr wala ‘Umar wala ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Hoja zao wanaziegemeza katika baadhi ya hadithi zilizomo katika vitabu vya Ahli Sunnah (Al-Bukhaariy na Muslim), na mojawapo ya hoja hizo ni hadithi hii ya Ghadiyr al-Khum.

 

Kabla hatujaanza inatubidi tuelezee kwanza kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni mume wa binti yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) mwanamke bora kupita wote Peponi, na yeye pia ni bin ammi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye pia ni Khalifa wa nne muongofu wa Waislamu na kwamba sifa zake njema tunazijuwa vizuri.

 

Hata hivyo, hapa hatuzungumzi juu ya utukufu wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa sababu sote tunauelewa vizuri, lakini hapa tunazungumza juu ya Hadithi ya Ghadiyr al-Khum kuwa ni dalili yakuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyestahiki kuwa Khalifa wa mwanzo.

 

Hebu tuisome kwanza hadithi hii kutoka katika kitabu cha Sahih Muslim kitabu cha hadithi nambari 36 kitabu cha fadhila za Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Imepokelewa kuwa Yazid bin Hayyaan amesema:

“Nilikwenda pamoja na Huswayn bin Sabra na ‘Umar bin Muslim kumtembelea Zayd bin Arqam, na tulipokuwa tumekaa pamoja naye Huswain akamwambia Zayd:

“Zayd, wewe umebahatika sana, umemuona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na umemsikia akihadithia, na umepigana vita vingi pamoja naye, na umesali nyuma yake. Kwa hakika Zayd umebahatika sana. Zayd, hebu tuhadithie yale uliyomsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema.

 

Akasema:

“Ewe mwana wa ndugu yangu, waLlaahi umri wangu umekuwa mkubwa na siku zangu zimesogea mbele na nimeyasahau mengi niliyokuwa nikiyakumbuka kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa hivyo nitakachokuhadithia wewe kikubali na nisichoweza kukuhadithia basi usinilazimishe. Kisha akasema:

 

“Siku moja Mtume wa Allaah alisimama kutuhutubia mahali penye maji panapoitwa Khum baina ya Makkah na Madiynah. Akamtukuza Allaah na kumpwekesha, akawaidhi na kukumbusha, kisha akasema:

 

“Enyi watu! Mimi ni mwanadamu, na hivi karibuni anaweza kunijia mjumbe wa Allaah na mimi nikamuitikia, na mimi nakuachieni vizito viwili. Cha kwanza ni kitabu cha Allaah ambacho ndani yake umo uongofu (uongozi) na nuru, kwa hivyo shikamaneni nacho kitabu cha Allaah na mkikamate vizuri”. Akatusisitiza juu ya kitabu cha Allaah na kutupendekezesha nacho. Kisha akasema: “Na watu wa nyumba yangu. Nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu.”

 

Huswayn akamuuliza Zayd:

“Ni nani hao watu wa nyumba yake ewe Zayd, si wake zake pia katika watu wa nyumba yake?”

Akasema: “Wake zake ni katika watu wa nyumba yake, lakini watu wa nyumba yake (alowakusudia hapa) ni wale walioharamishiwa kupokea sadaka”.

Akasema:

“Ni nani hao?”

Akasema:

“Hao ni watu wa nyumba ya ‘Aliy na watu wa nyumba ya ‘Aqiyl na watu wa nyumba ya Jaafar na watu wa nyumba ya ‘Abbaas”.

Akauliza:

“Wote hao wameharamishiwa Sadaka?”

Akasema:

“Ndiyo”.

 

Hadithi hii imo pia katika vitabu vya At-Tirmidhiy na Ahmad na An-Nasaaiy na Al-Hakim na wengine.

 

Kutoka katika Musnad ya Imam Ahmad imeandikwa kama ifuatavyo;

Tumehadithiwa na Ibnu Namir kuwa ‘Abdul-Malik bin Abu Sulaymaan amesema kutoka kwa ‘Attwiyah Al-Awfiy amesema: “Nilimuuliza Zayd bin Al-Arqam nikamwambia kuwa watu wamenihadithia hadithi juu ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) na wakanambia kuwa wamehadithiwa na wewe juu ya siku ya Ghadiyr al-Khum, na mimi nataka kuisikia kutoka kwako”.

Akasema; “Nyinyi watu wa ‘Iraaq mnacho kile mlichonacho”.

Nikamwambia: “Usiwe na wasi wasi juu yangu”.

Akanambia: “Ndiyo tulikuwepo Al-Juhfa na ulipofika wakati wa adhuhuri Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea akiwa ameushika mkono wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

“Enyi watu, hamjuwi kuwa mimi ninawsatahiki zaidi (Awla) Waislamu kuliko nafsi zao?”

Wakasema:

“Ndiyo”.

Akasema:

“Basi mwenye kunipenda mimi lazima ampende na ‘Aliy (man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu).”

Attwiyah akasema:

“Alisema (Allahumma waali man walaahu wa ‘aadi man ‘aadahu) Mola wangu uwe adui wa atakayemfanyia uadui na umpende atakayempenda?”

Akasema:

“Nimekuhadithia kama nilivyosikia.”

 

Kauli ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema; ‘Man kuntu mawalahu fa ‘Aliy mawlaahu’ ‘Basi mwenye kunipenda mimi lazima ampende na ‘Aliy’, ingawaje haimo katika Sahih Muslim lakini baadhi ya wanavyuoni wamesema kuwa ziada hii ni sahihi.

 

Ama ile ziada ya ‘Allahumma waali man waalahu wa ‘aadi man ‘aadahu’ Mola wangu uwe adui wa atakayemfanyia uadui na umpende atakayempenda” na ziada nyenginezo, ingawaje baadhi ya Maulamaa wamesema kuwa ni sahihi, lakini Maulamaa wengi wa hadithi wanasema kuwa ziada hii ni maudhui. Yaani maneno ya uongo yaliyozidishwa.

 

 

Hadithi hii inatumiwa na Mashia katika kuthibitisha kuwa ‘Aliy ndiye Khalifa baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwamba neno ‘mawlaa’ maana yake ni ‘waali’ yaani kiongozi, na kwa ajili hiyo tukio hili lina maana kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapa anawaambia Waislamu kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye atakayekuwa khalifa baada yake.

 

Huu ndio ushahidi wao katika hadithi hii, kwa hivyo tofauti iliyopo ni katika kulifasiri neno ‘man kuntu mawlahu fa ‘Aliy mawlahu’. Mashia wanasema kuwa maana ya maneno haya ni kuwa ‘man kuntu WALIYYAHU fa ‘Aliy WALIYYAHU’, lakini Masunni wanasema kuwa neno hili maana yake ni mapenzi na uhusiano mwema.

 

Katika lugha ya Kiarabu, neno ‘Muwalaat’ ni kinyume (opposite) ya neno ‘Mu’adaat’ na ushahidi unapatikana katika ziada ya mwanzo; ‘Mola wangu mpende atakayempenda na uwe adui wa atakayemfanyia uadui’.

 

Kwa hivyo hapa tunazungumza juu ya ‘Muwalaat na Mu’adaat’, yaani ‘Kupenda na Uadui’, yanayohusiana na watu kumpenda ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Kabla hatujaendela mbele, kwanza hebu tuzungumze juu ya sababu iliyomfanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusema maneno hayo.

 

Mashia wanasema kuwa; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimamisha watu mahali hapa wakati wa joto kali, na wanasema kuwa idadi yao inafika watu mia moja elfu, na wanasema kuwa hapa ndipo mahali wanapokusanyika Mahujaji wote, na sababu kubwa ya kuwakusanya watu hao ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kuwaambia watu kuwa; ‘Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu’, pamoja na maneno mengine waliyoongeza.

 

Sababu ya kweli iliyomfanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusema maneno haya ni hii ifuatayo;

Anasema Al Bayhaqi kutoka kwa Abu Sa’iyd kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwakataza Maswahaba (alokuwa nao safarini walipokuwa wakirudi kutoka nchi ya Yemen) wasiwapande ngamia wa sadaka, kisha akamchagua mmoja wao awe kiongozi na yeye akaondoka na kwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Aliporudi akaona kuwa kiongozi wao aliwaruhusu kuwapanda ngamia. Alipoona hivyo, ‘Aliy akakasirika na kumlaumu kiongozi wao. Na riwaya nyingine zinasema kuwa aliwakataza kuvaa nguo lakini wao wakazivaa. Anasema Abu Sa’iyd kuwa; tuliporudi Madiynah tukamhadithia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukali wa ‘Aliy juu yetu, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

“Acha kusema ewe Sa’ad bin Maalik baadhi ya maneno yako juu ya ndugu yako ‘Aliy, kwani waLlaahi ninavyoelewa mimi ni kuwa (‘Aliy) amefanya mema mengi katika njia ya Allaah”.

(Anasema Ibn Kathiyr kuwa hadithi hii ni njema kwa masharti yaliyowekwa na An-Nasaaiy). Na hadithi hii pia imetolewa na Al-Bayhaqiy na wengine.

 

Anasema Ibn Kathiyr kuwa malalamiko ya wanajeshi yalipoongezeka baada ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwakataza kuwapanda ngamia wa sadaka na kuwanyang’anya nguo mpya walizoruhusiwa kuzivaa na msaidizi wa ‘Aliy, na Allaah ndiye anayejuwa zaidi, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akirudi kutoka katika hija yake na baada ya kumaliza shughuli zote zinazohusiana na hija hiyo, na alipokuwa njiani kuelekea Madiynah, alipopita mahali panapoitwa Ghadiyr al-Khum akainuka na kuwahutubia watu akamtetea ‘Aliy, na kuinyanyua heshima yake na akawatanabahisha watu juu ya fadhila za ‘Aliy na pia kuwajulisha juu ya mapenzi yake kwa ‘Aliy na uhusiano uliopo baina yake na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), yote haya kwa ajili ya kuondoa yale yaliyoingia katika nyoyo za watu wengi dhidi ya ‘Aliy.

Al-Bidaayah wan-Nihaayah (5/55).

 

Na hii ndiyo maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaichelewesha hotuba yake mpaka walipokuwa karibu na mji wa Madiynah na hakuwahutubia pale walipokuwa Makkah wakati wa Hija.

Siku ya kusimama ‘Arafah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahutubia mahujaji wote, lakini hakulizungumzia jambo hili kabisa, na baada ya kumaliza hotuba yake akawauliza watu:

“Nimeufikisha ujumbe?”

Watu wakajibu:

“Ndiyo (umeufikisha)”

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Mola wangu shuhudia”.

Kwa ajili gani basi Mtume alichelewesha khutbah yake juu ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) mpaka walipokuwa wakirudi, tena karibu na mji wa Madiynah?

Kwa sababu wale waliokuwa wakisikitika juu ya ‘Aliy walikuwa ni watu wa Madiynah, wale waliokwenda naye vitani, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalizungumzia jambo hili walipowasili mahali panapoitwa Ghadiyr al-Khum katika mji wa Juhufa, mji uliopo kilomita 250 mbali na mji wa Makkah.

 

Ukiiangalia ramani iliyopo chini utaona kuwa si kweli yale maneno yanayosemwa kuwa mahali hapo (Ghadiyr al-Khum) ni mahali wanapokusanyika mahujaji.

 

Mahujaji wanakusanyika mji wa Makkah na wanaondokea huko huko Makkah. Mahujaji hawakusanyiki mahali penye umbali wa kilomita 250 kwa ajili ya kuondoka Makkah baada ya kumaliza shughuli za Hija, kwani watu wa Makkah wanabaki huko huko Makkah, na  watu wa Twaif wanakwenda Twaif, na watu wa Yemen wanakwenda zao Yemen na watu wa Al-Kuufa wanakwenda Al-Kuufa na hivi ndivyo ilivyo, na watu wa makabila mbali mbali wanaelekea makwao, na watu waliobaki na kufuatana na msafara wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wale tu watu wa Madiynah na wale wanaopita njia hiyo wakielekea makwao, na hao ndio ambao Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza nao aliposema;

Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlahu”.

Isitoshe khutbah hiyo haikuwa juu ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) peke yake, ingawaje Ali anastahiki hotuba nyingi, isipokuwa katika hotuba hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza pia juu ya Qur-aan na umuhimu wake na akawakumbusha watu pia juu ya kuwapenda watu wa nyumba yake (Radhiya Allaahu ‘anhu), kisha akawatanabahisha watu juu ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

 

 

MAANA YA NENO (MAWLAA)

 

Anasema Ibn al-Athiyr kuwa neno Mawlaa maana yake ni;

Mwenye kumiliki,

Mwenye kusaidia,

Mwenye kuwaacha huru watumwa,

Msaidizi,

Mpenzi,

Mtumwa aliyeachwa huru (kwa mfano Zaid (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaitwa ‘Mawlaa wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)’,

Bin Ammi,

Na pia Mtoto wa mjomba na shangazi.

Yote haya katika lugha ya Kiarabu yanabeba maana ya neno hili ‘Mawlaa’.

Na hadithi hii haina ndani yake dalili yoyote ile ya kuchaguliwa kwa Imam, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angekuwa amekusudia kumchagua Khaliyfah atakayetawala baada yake, basi asingetamka neno linaloweza kubeba maana zote hizo, bali angetamka neno linalobeba maana moja tu. Angelisema kwa mfano;

“’Aliy ndiye Khalifa wenu baada yangu”, au “Nikifa mimi basi msikilizeni na mtiini ‘Aliy bin Abi Twaalib”.

Lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya ufasaha wake katika lugha ya Kiarabu hakutamka lolote katika maneno haya yaliyo wazi kabisa na badala yake akasema;

Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu

 

Allaah Anasema;

Mawlaakumu nnaaru” (makazi yenu ni motoni ndio unaokustahikieni) (na ni marejeo mabaya kabisa).”

Katika aya hii Allaah Anauita moyo kuwa ni ‘mawlaa’, kwa sababu ya kukamatana nao sana na watu wa motoni.

 

Ningependa pia kuwatanabahisha wasomaji kuwa neno ‘mawlaa’ linakhitalifiana na neno ‘waliy’, kwani haya ni maneno mawili tofauti.

Neno ‘waliy’, (kwa kasrah) asili yake linatokana na neno ‘wilaayah’ na maana yake ni ‘Uongozi’, ama neno ‘mawlaa’ linatokana na neno ‘walaaya’, (kwa fat-hah) na maana yake ni ‘kupenda’, na ‘kusaidia’.

 

Allaah Anasema;

Fainna Allaaha huwa MAWLAAHU” (Kwani Allaah ni kipenzi chake)”.

Suratut Tahrym – 4

 

Katika kuifasiri hadithi hii ya Zayd, anasema Imam ash-Shaafi’iy;

“Kilichokusudiwa hapo ni mapenzi ya Kiislamu, kama Alivyosema Allaah;

“Hayo ni kwa sababu Allaah ni Mlinzi wa walioamini, ‘Mawlaa Lladhiyna aamanuu’, (anawapenda), lakini makafiri hawana mlinzi wao”.

Muhammad – 11

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelitumia neno hili ‘mawlaa’ mara nyingi na si kwa ajili ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) peke yake. Katika hadithi ifuatayo iliyosimuliwa na Abu Huraira (Radhiya Allaahu ‘anhu) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Makabila ya Quraysh na Answaar na Juhaynah na Muzaynah na Aslam na Ghifaar na Ashja-a wote ni wasaidizi wangu (mawaalii – wingi wa neno mawlaa) na hawana mlinzi mwingine isipokuwa Allaah na Mtume wake”.

Al-Bukhaariy Volume 4, Book 56, hadithi nambari 715 na imetolewa na wengine pia.

 

Ipo mifano mingi ya aina hiyo, lakini iliyotajwa hapo juu inatosha kuwa ni dalili.

Ni muhimu pia kuzingatia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutumia neno ‘baada yangu’, pale aliposema:

Man kuntu mawlaahu fa ‘Aliy mawlaahu”.

Alitamka maneno hayo bila kuweka wakati maalum, hii ikimaanisha kuwa amri hii haina wakati maalum na kwa ajili hiyo ikiwa kusudi ya hotuba yake ni kuwaambia watu kuwa ‘Yeyote aliye chini ya uongozi wangu basi na Ali ni kiongozi wake’, kama wanavyofasiri Mashia, kwa hivyo patakuwa na tatizo kubwa, kwani maneno haya yataleta maana kuwa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa na viongozi wawili wenye kuuongoza ummah, jambo lisiloingia akilini.

 

Bila shaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukusidia hivyo na wala Masahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhu) hawakufahamu hivyo, ama sivyo pangekuwa na fitna kubwa wakati ule.

Hata hivyo kuwepo kwa ‘mawlaa’ wawili au zaidi kwa maana ya wapenzi au wasaidizi ni jambo linalowezekana, yaani kumpenda na kumsaidia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia kumpenda na kumsaidia ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) wakati mmoja.

 

Kutokana na yote haya tunaelewa kuwa hadithi hii ya Ghadiyr al-Khum haina uhusiano wowote wa nani atakayekuwa kiongozi baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini wakati huo huo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatujulisha kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni kipenzi chake na kwamba anatutaka sisi tumpende pia na tumnusuru.

Tunamuomba Allaah atufufuwe pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pamoja na ‘Aliy na pamoja na Maswahaba wote watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

                                                                                                              

 

 

Share