Kisa Cha Ardhi Ya Fadak - Baina Ya Abu Bakr Asw-Swiddiyq Na Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘Anhuma)

 

Imetafsiriwa na Muhammad Faraj

 

 

Utangulizi

 

Mashia wanadai kuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimdhulumu Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) binti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) kwa kukataa kumrithisha ardhi ya Fadak iliyoachwa na baba yake, na kwamba Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alizusha hadithi ya uongo aliyoisikia peke yake inayodai kuwa eti Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) amesema:

“Sisi Mitume haturithiwi, na kile tunachokiacha (baada ya kufa kwetu) ni Sadaka”.

Na kwamba kwa ajili hiyo Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuudhi Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) na kwamba mwenye kumuudhi Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) amemghadhibisha Allaah.

 

 

Nini Fadak?

 

Fadak ni ardhi iliyokuwa ikikaliwa na Mayahudi katika nchi ya Hijaz, na inasemekana pia kuwa ardhi hiyo ipo Madina, karibu na mji wa Khaibar.

Baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) kuuteka mji wa Khaybar uliokuwa ukikaliwa na Mayahudi, hofu iliingia ndani ya nyoyo za Mayahudi waliobaki, jambo lililowafanya wakubali kuandikiana mkataba na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), mkataba ambao ndani yake walikubaliana kuwa ardhi ya Fadak ichukuliwe na Waislamu, na kwa ajili hiyo ardhi hiyo ikaingia katika hukmu ya ‘Fai’y’, nayo ni mali aliyoleta Allaah kwa Mtume wake bila kuitaabikia wala kutumia farasi wala ngamia, na kwa ajili hiyo ardhi hiyo ikawa milki ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam).

Allaah Anasema:

“Na mali (ya Fai’y) aliyoleta Allaah kwa Mtume Wake kutoka kwao hamkuyaendeshea mbio farasi wala ngamia (hamkuyataabikia), lakini Allaah huwapa mamlaka Mitume yake juu ya wowote awatakao (kama alivyokupeni hivi); na Allaah ni Mwenye uweza juu ya kila kitu”.

Al-Hashr - 6

 

 

 

Nilimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) Akisema

 

Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim na wengine kuwa baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) kufariki dunia, alikuja Bibi Faatwimah kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhum) akidai urithi wake kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), na urithi huo ni ardhi ya Fadak na pia sehemu ya ngawira ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) aliyoipata katika vita vya Khaibar.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:

“Mimi nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) akisema:

“Sisi (Mitume) haturithiwi, tulichokiacha (baada ya kufa kwetu) ni Sadaka”.

Na katika riwaya nyingine iliyomo ndani ya Musnad ya Imam Ahmed kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) alisema:

“Sisi Mitume haturithiwi”.

Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) akamkasirikia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) huku akitoa dalili kutoka katika Qur-aan tukufu aya isemayo:

“Allaah anakuusieni juu ya watoto wenu; mwanamume apate sawa na sehemu ya wanawake wawili”.

An Nisaa – 11

Na akasema kuwa Allaah amesema:

“Na Sulaymaan alimrithi Daawuud”, na Amesema juu ya Zakariyaa:

“Nipe mrithi kutoka kwako atakayenirithi na kuwarithi kizazi cha Yaakubu na umfanye Mola wangu awe mwenye kukuridhisha”.

Surat Maryam – 5-6

 

Kabla sijaendelea mbele ningependa kuashiria kwa ufupi tu, kuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuichukua ardhi hiyo kwa manufaa ya nafsi yake, wala hakukitumia kile alichopata ndani ya ardhi hiyo kwa ajili ya watu wa nyumba yake, bali alikuwa akikusanya mali inayopatikana humo na kufanya kama alivyokuwa akifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) aliyekuwa akiigawa baina ya watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), na kilichobaki akiitumia katika njia ya Allaah kwa manufaa ya Waislamu kama alivyosema Allaah katika Suratul Hashr katika aya tutakayoitaja kwa ukamilifu kila tukiendelea mbele.

 

 

 

 

Hadithi Hii Ni Sahihi?

 

Jambo muhimu la kulishughulikia hivi sasa ni usahihi wa hadithi hii aliyosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) ndani yake kuwa:

“Sisi Mitume haturithiwi”.

 

Ikiwa hadithi hii aliyoitamka Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni sahihi, basi hatutokuwa na haki ya kumlaumu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), bali hatuna budi kuikubali na kuacha upendeleo, kwani aliyetamka maneno hayo (Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) ndiye aliyetuletea Qur-aan kutoka kwa Mola wake, na yeye ndiye mwenye kujuwa zaidi kuliko Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) na kuliko mtu yeyote mwingine.

 

Kwa hivyo sisi tunasema kuwa; Maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) tunayaweka juu kuliko maneno ya mtu yeyote mwingine awe mtu huyo mtukufu namna gani. Sasa ikiwa kweli Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) ametamka maneno hayo, kwanini basi tumlaumu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kuyafuata na kuyatekeleza?

 

 

 

Ushahidi Ndani Ya Vitabu Vya Mashia

 

Hadithi hii ya kuwa Mitume (‘Alayhimu Ssalaam) hawarithiwi, ni sahihi na imo hata ndani ya vitabu vya Mashia na si katika vitabu vya Ma Sunni peke yao.

Sasa ikiwa hadithi hii ni sahihi na imo hata ndani ya vitabu vya Mashia, kwanini basi atuhumiwe Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ameitunga yeye hadithi hii na kwamba kwa ajili hiyo amemghadhibisha Bibi Faatwimah?

 

Imesimuliwa na Al-Kulayniy katika kitabu chake maarufu ‘Al-Kaafiy’ kuwa:

“Abu ‘Abdillaah (Imam Ja’afar asw-Swaadiq) amesema:

“Na hakika Maulamaa ni warithi wa Mitume. Na hakika Mitume hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa”

Al-Kaafiy 1/42.

Imam Muhammad Baaqir al-Majlisiy katika kitabu chake kiitwacho Mir'at al – ‘Uquul 1/111 amesema kuwa hadithi hii ni sahihi.

 

Khomeini ameiandika hadithi hii katika kitabu chake kiitwacho ‘Al-Hukuumah al-Islamiyah’ (Serikali ya Kiislamu), na akaitumia kama ni ushahidi wa Wilaayat al-Faqiyh chini ya kichwa cha maneno; (Sahihat al Qaddah) aliposema:

“Amesema ‘Aliy bin Ibraahiym kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Hammad bin Issa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Maymun al Qaddah kuwa Abu ‘Abdillaah (Ja’afar asw-Swaadiq (‘Alayhi Ssalaam) amesema:

“Atakayefuata njia ya kutafuta elimu, basi Allaah atamrahisishia njia ya Peponi. Na maulamaa ni warithi wa Mitume. Na Mitume hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa.”

Al-Kaafiy, kitab fadhl Al-‘Ilm, mlango wa Sifat al Ilm wa Fadhlihi, hadithi nambari 2

 

Na katika kitabu hicho hicho cha ‘Al-Hukuumah al-Islaamiyah’ ukurasa wa 133 Khomeini ameiandika hadithi nyingine iliyopokelewa kwa njia ya Muhammad Yahya kutoka kwa Ahmad bin Muhammad bin Iysa kutoka kwa Muhammad bin Khalid kutoka kwa Abu Abdullah (Imam Ja’afar asw-Swaadiq (‘Alayhi Ssalaam) kuwa amesema:

“Hakika Maulamaa ni warithi wa Mitume, na hii ni kwa sababu Mitume hawaachi Dirham wa Dinari kwa ajili ya kurithiwa, bali wao wanaacha maneno yao”.

Al-Hukuumat al-Islaamiyah uk. 133

 

Kutokana na yaliyotangulia tunamaliza kwa kusema kuwa;

Si haki kutoikubali hadithi hii ya Kutorithiwa kwa Mitume katika kadhia ya Fadak, na kuikubali katika kadhia ya Wilayat al Faqih, kama alivyoandika Khomeini na kabla yake Majlisi.

Kwa nini Mashia wawe wanaikubali kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) pale wanapotaka na waikatae pale wasipoitaka juu ya kujuwa kwao kuwa kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) haiwezi kubadilishwa na kiumbe chochote kile, hata kama kiumbe huyo ni binti yake na kipenzi chake?

 

 

Imepokelewa Kwa Njia Nyingi

 

Si kweli kusema kuwa hadithi hii imepokelewa kwa njia ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) peke yake, na mwenye kumtuhumu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) anakuwa ama amekusudia kumsingizia uongo Sahaba huyu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), au ni mtu mjinga asiyeelewa elimu ya hadithi.

 

Inajulikana na kila mtu kuwa hadithi hii ni maarufu sana na imesimuliwa na Maswahaba wengi sana wakiwemo ‘Umar, ‘Uthmaan, ‘Aliy, Twalhah, Az-Zubayr, Sa’ad, Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Al-‘Abbaas bin ‘Abdul Muttalib, wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), Abu Hurayrah na wengine (RadhiyAAllaahu anhum), na riwaya zote hizo ni sahihi zilizothibiti katika vitabu vya Ahlus Sunnah.

 

Kwa hivyo kauli hii imesimuliwa na Maswahaba wengi (Radhiya Allaahu ‘anhum) katika vikao mbali mbali, na hapana hata mmoja aliyeikanusha, bali wote waliikubali na kwa sababu hii hapana hata mmoja kati ya wake zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) aliyekuja kudai urithi wake, na hata ami yake alipokumbushwa juu ya hadithi hiyo hakushikilia kuutaka urithi, na kila aliyekuja kutaka urithi alikuwa akikubali mara anapokumbushwa juu ya hadithi hii, na hali hii ikaendelea bila kubadilika hata ulipofika wakati wa ukhalifa wa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye hakuwarithisha mali hiyo wanawe kama tutakavyoona kila tukiendelea mbele.

 

Ifuatayo ni mojawapo ya hadithi iliyomo ndani ya Al-Bukhaariy na ndani ya vitabu vingine inayotujulisha kuwa hadithi hii ni maarufu miongoni mwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum)

Anasema Malik bin Aus (Radhiya Allaahu ‘anhu):

“Nilikuwa nimekaa nyumbani kwa ‘Umar na mtumishi wake Yarfa akaja na kumwambia ‘Umar:

“‘Uthmaan na ‘Abdur-Rahmaan na Az-Zubayr na Sa’ad wanataka kukuona, niwaingize?”

‘Umar akasema:

“Waache waingie”.

Kisha akaja tena na kumwambia ‘Umar:

“Niwaingize ‘Aliy na ‘Abbaas?”

‘Umar akasema:

Waache waingie”.

‘Abbaas (baada ya kuingia) akasema:

“Ewe amiri wa Waislam, nakutaka uhukumu baina yangu na mtu huyu (Ali juu ya mali ya urithi)”.

‘Umar akasema (kuwauliza Othman na ‘Abdur-Rahmaan na Az-Zubayr na Sa’ad):

“Nakuombeni kwa ajili ya Allaah ambaye kwa amri Yake mbingu na ardhi zimenyanyuka; Nyinyi si mnajuwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) alisema:

“Sisi haturithiwi na tunachokiacha (baada ya kufa kwetu) ni sadaka? Na kwamba alijikusudia nafsi yake?”

Wakajibu:

“Kweli alisema hayo”.

Kisha ‘Umar akawageukia Ali na ‘Abbaas akawauliza:

“Nyinyi nyote (wawili wenu) si mnajuwa pia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) alisema hayo?”

Wawili wao wakasema:

“Kweli amesema hayo”?

‘Umar akasema:

“Sasa niacheni nizungumze nanyi juu ya jambo hili; Allaah alimchagua Mtume wake (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) kuisimamia Fa'iy hii”, na akamhusisha nayo yeye peke yake na si mtu mwengine yeyote, kama Allaah alivyosema:

‘Na (Fa'iy) mali aliyoleta Allaah kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuyaendeshea mbio farasi wala ngamia (hamkuyataabikia), lakini Allaah huwapa mamlaka Mitume yake juu ya wowote awatako (kama alivyokupeni hivi); na Allaah ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

Mali (Fa'iy) aliyoleta Allaah kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji (vilivyo karibu na Madina) ni kwa ajili ya Allaah. (Basi yatatumika kwa ajili ya dini ya Allaah) na kwa ajili ya Mtume (wake, na anachokupeni basi atachukua mwenyewe) na jamaa (zake) na mayatima na maskini na msafiri aliyeharibikiwa, ili wasiwe kinyang’anyiro baina ya matajiri wenu tu. Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni basi jiepusheni nacho. Na muogopeni Allaah; kwa yakini Allaah ni Mkali wa kuadhibu”.

Al Hashr – 6-7

 

‘Umar akaendelea kusema

“Kwa hivyo ngawira ile alipewa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) peke yake. WAllaahi hakuichukuwa yeye akakunyimeni nyinyi, bali alikuwa akikugawieni katika mapato ya ardhi hiyo mpaka ilipobaki mali hii.

Kwa hivyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa watu wa nyumba yake katika mali hii matumizi yao ya mwaka mzima, kisha alikuwa akichukuwa kilichobaki ndani yake na kuijaalia kuwa mali ya Allaah (kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu).

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) akaendelea hivyo maisha yake yote. Nakuombeni kwa ajili Allaah muniambie: Si mnayajuwa yote hayo?”

Wote wakasema:

“Ndiyo”

Kisha ‘Umar akawauliza Ali na ‘Abbaas:

“Nakuombeni kwa ajili Allaah muniambie:

“Si mnayajuwa yote hayo?”

Wote wawili wakasema:

“Ndiyo”.

Kisha ‘Umar akaongeza:

“Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) alipofariki dunia, Abu Bakr akasema:

“Mimi ni Khalifa wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), na akachukuwa dhamana na kufanya kama alivyokuwa akifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam). Na Abu Bakr alipofariki dunia, mimi (‘Umar) nikasema:

“Mimi ni Khalifa wa Khalifa wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), nikawa kwa muda wa miaka miwili nafanya vile vile kama alivyokuwa akifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) na Abu Bakr. Kisha mkanijia wawili nyinyi (‘Aliy na ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhum) na neno lenu likawa moja mkinishtakia juu ya jambo hili hili. Mlikuja kutaka sehemu yenu katika urithi wa bin ami yako na huyu (Aly) akitaka sehemu ya urithi wa mkewe kutoka kwa baba yake. Nikakuambieni: Mkitaka nitakupeni nyinyi dhamana hiyo, kwa sharti ile ile (kuwa mfanye vile vile alivyokuwa akifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) na alivyokuwa akifanya Abu Bakr na mimi).

(Sasa mnanitaka mimi nitowe uamuzi mwingine kinyume na uamuzi huo (wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam)?

WaLlaahi naapa kwa Yule ambaye kwa amri Yake, mbingu na ardhi zimenyanyuka kuwa sitohukumu kinyume na hivyo mpaka Kiama kitakaposimama. Na kama mumeshindwa kuisimamia basi irudisheni kwangu na mimi sitoshindwa kukusimamieni”.

Al-Bukhaariy – Muslim – At-Tirmidhyy – An-Nasaaiy – Ibn Maajah – Abu Daawuud na wengine.

 

Katika hadithi hii tunapata faida zifuatazo;

 

1.     Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakusema uongo wala kuizuwa hadithi hii

 

2.     Maswahaba wote walikuwa wakiijuwa pia

 

3.     Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiisimamia ardhi hiyo ya Fadak na kugawa mapato yake sawa kama alivyokuwa akifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), jambo ambalo hata ‘Aliy na Al-‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikiri.

 

Kwa hivyo mwenye kuikanusha hadithi hii anaonesha dalili ya ujahili wake au kukusudia kwake kumsingizia uongo Khalifa wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam).

 

 

 

Du’aa ya Nabii Zakariyaa (‘Alayhi Ssalaam)

 

Kuhusu kauli ya Nabii Zakariyaa (‘Alayhi Ssalaam) alipoomba du’aa akasema:

“Nipe mrithi kutoka kwako atakayenirithi na kuwarithi kizazi cha Yaakubu na umfanye Mola wangu awe mwenye kukuridhisha.”

Surat Maryam – 5-6

 

Kusema kuwa Nabii Zakariyaa (‘Alayhi Ssalaam) alikusudia kuomba mrithi wa kurithi mali yake ni hoja isiyokuwa na uzito kutokana na sababu zifuatazo;

Haitokuwa vizuri kwa Mcha Mungu wa kawaida tu kumuomba Allaah Amruzuku mtoto kwa ajili ya kurithi mali yake. Itakuwaje basi kwa Mtume mtukufu kama Nabii Zakariyaa (‘Alayhi Ssalaam) aombe mtoto kwa ajili ya kumrithi mali yake? Alichokiomba Mtume Zakariyaa (‘Alayhi Ssalaam) ni mtoto atakayeweza kurithi matendo pamoja na daraja yake baada ya kufa kwake.

 

Inajulikana pia kuwa Nabii Zakariyaa (‘Alayhi Ssalaam) alikuwa mtu masikini aliyekuwa akifanya kazi ya useremala. Utajiri gani basi atakaoupata kutokana na kazi yake hiyo hata amuombe Allaah amruzuku mtoto wa kuurithi.

 

Bali uhakika unaojulikana na kila mtu ni kuwa Mitume yote (‘Alayhimu Ssalaam) hawakuwa wakijiwekea chochote na kwamba kile wasichokihitajia walikuwa wakiwapa masikini.

 

Kwa ajili hiyo neno ‘al irth’ (urithi) linapotumika kwa ajili ya Mitume (‘Alayhimu Ssalaam) siku zote huwa ni kwa ajili ya urithi wa elimu au urithi wa utume na si kwa ajili ya urithi wa mali.

 

Kwa mfano;

Allaah Anasema:

“Kisha tumewarithisha Kitabu (hiki cha Qur-aan) wale tuliowaongoza miongoni mwa waja wetu.”

Faatwir – 32

 

Na Akasema:

“Hao ndio warithi. Ambao watarithi Pepo, wakae humo milele.”

Al-Muuminuun – 10-11

 

Aayah hizi na nyingine zilizo mfano wake zinatufahamisha uzuri maana ya ile hadithi inayosema kuwa; Mitume hawarithiwi mali, bali wanarithiwa elimu.

 

 

 

Nabii Sulaymaan alimrithi Nabi Daawuud (‘Alayhimu Ssalaam)

 

Kutokana na ushahidi uliotangulia tunaweza kuifahamu vizuri maana ya kauli ya Allaah Subhanahu wa Taala Aliposema:

“Na Sulaymaan alimrithi Daawuud”

An-Naml – 16

 

Tunafahamu kuwa Allaah Subhanahau wa Taaala anatujulisha hapa juu ya urithi wa Utume na urithi wa Ilimu, na si urithi wa mali na mambo mengine ya kidunia.

 

Na inafahamika zaidi tutakapofahamu kuwa Nabii Daawuud (‘Alayhi Ssalaam) alikuwa na wake wengi sana na watoto wengi pia, na hakutajwa hapa isipokuwa Nabii Sulaymaan peke yake (‘Alayhi Ssalaam) aliyeurithi utume kutoka kwa babake.

Ungekuwa urithi uliokusudiwa katika aya hii ni urithi wa mali, kwa nini basi wasitajwe na ndugu zake pia?

Ungekuwa urithi uliokusudiwa katika aya hii ni urithi wa mali na mambo ya kidunia, pasingekuwa na umuhimu wowote wa kutajwa ndani ya Qur-aan, kwani ni jambo la kawaida katika mila zote na katika dini zote kwa mtoto kumrithi mwanawe na si kawaida ya Qur-aan kusema kwa mfano:

“Fulani alifariki dunia na mwanawe akarithi mali yake”.

 

 

Urithi Wa Wanawake Katika Madhehebu Ya Ithna- ‘Ashariyah

 

Jambo la kushangaza ni kuwa katika madhehebu ya Kishia Ithna- ‘Ashariyah, wanawake hawaruhusiwi kurithi ardhi wala nyumba.

Katika Al-Kaafiy, kitabu maarufu kinachotegemewa sana na Mashia kilichoandikwa na Al-Kulayniy, mwanachuoni huyo ameuhusisha mlango maalum chini ya kichwa cha maneno;

‘Hakika wanawake hawarithi nyumba wala ardhi’.

Ndani ya mlango huo ameinukuu hadithi iliyosimuliwa na Abu Ja’afar kuwa amesema:

“Hakika wanawake hawarithi chochote katika ardhi wala nyumba”.

 

Imeandikwa na At-Tuwsi pia katika At-Tahadhiyb na Al-Majlisi katika Bihaar al-Anwaar kuwa Maysar amesema:

“Nilimuuliza Abu ‘Abdillaah (‘Alayhi Ssalaam) juu ya wanawake na haki zao katika urithi akasema:

“Wana haki zao katika thamani ya udongo na ujenzi na mbao na miti tu, ama ardhi na nyumba, wao hawana haki ya urithi (wowote ndani yake).”

 

Na kutoka kwa Muhammad bin Muslim kutoka kwa Abu Ja’afar (‘Alayhi Ssalaam) kuwa amesema:

“Wanawake hawana haki ya kurithi ardhi wala nyumba”.

 

Na kutoka kwa ‘Abdul Malik bin Aayun kuwa mmoja wa ma Imam alimwambia:

“Wanawake hawana haki ya urithi katika ardhi wala nyumba”.

 

Ni jambo la kushangaza wAllaahi! Vipi wanaweza kuzungumza juu ya kudhulumiwa kwa bibi Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa eti amenyimwa urithi wa ardhi ya Fadak iliyoachwa na baba yake (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) wakati katika madhehebu yao, mwanamke hana haki ya kurithi vitu hivyo?

 

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Naye Hakuwarithisha Wanawe

 

Inajulikana kuwa alipotawala ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye pia hakuwarithisha ardhi hiyo watoto wa Bibi Faatwimah ambao ni Al-Hasan na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Hii ni dalili kuwa hata Sayiduna ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alkuwa akiijuwa vizuri na kuikubali hadithi hii isemayo; ‘Sisi Mitume haturithiwi’, ama sivyo kwa nini basi awanyime wanawe haki ya urithi kutoka kwa mama yao alourithi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam)?

Yeye mwenyewe Ali (Radhiya Allaahu ‘anhu) ana hiari yake kama hana haja ya haki yake katika urithi huo, lakini wanawe ilimbidi awarudishie haki yao hiyo wanayodai kuwa walinyang’anywa na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Sasa ikiwa ‘Aliy mwenyewe hakuirudisha ardhi hiyo kwa wenyewe, kwanini basi wanamlaumu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)?

Bali imepokelewa hadithi kutoka kwa Murtadha katika kitabu chake kiitwacho Ash-Shaafi’i fil Imaamah kuwa alipopewa Ali (Radhiya Allaahu ‘anhu) ukhalifa wa Waislamu, watu walimwendea na kumkumbusha juu ya kuirudisha ardhi ya Fadak, lakini ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akajibu:

“Kwa hakika ninamsitahi Allaah kuibadilisha amri na kurudisha kile alichokizuwia Abu Bakr, kisha ‘Umar akaiendeleza amri hiyo”.

 

 

 

Vichekesho

 

Katika kitabu cha Al-Kaafiy, kilichoandikwa na Al-Kulayniy imo hadithi ya kushangaza sana na ya kuchekesha, hii ikiwa ni dalili ya kwenda kwa kupepesuka na kujigonga huku na kule kama vipofu wale wanaoshikilia kuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimdhulumu Bi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

Hadithi inasema:

“Abul Hassan (Imam ‘Ali ar-Ridhwaa) alipokwenda kumtembelea Al-Mahdi alimkuta akiwarudishia watu haki zao zilizochukuliwa kwa dhulma. Imam Ridhwaa akamuuliza:

“Na haki zetu tulizodhulumiwa, kwanini huturudishii?”

Al-Mahdi akamuuliza:

“Ni nini hicho mulichodhulumiwa ewe Abal Hassan?”

Akajibu:

“Allaah Alipompa Mtume wake ushindi na kuiteka ardhi ya Fadak…”

Al-Mahdi akamwambia:

“Hebu nielezee iwapi ardhi hiyo?”

Imam Ridhwaa akasema:

“Sehemu moja ya ardhi hiyo ni mlima Uhud, na ya pili imefika mpaka Al-‘Ariysh iliyopo Misri na nyengine ni sehemu ya kandokando ya bahari na sehemu nyingine ni Dawmat al Jandal.”

Al-Kaafiy, bab al Fay wal Anfal 1/543 na pia katika Bihar al Anwar 48/156.

 

Itakuwaje basi kipande cha ardhi kilichopo Khaybar kikaweza kuwa na ukubwa wa kiasi hicho.

 

Mlima Uhud upo Madiynah, na Dawmat al-Jandal ipo karibu na mpaka wa Saudia na Jordan. Ama Al-‘Ariysh ni mji uliopo huko Misri karibu na mlima wa Sinai.

Bila shaka sisi hatuamini kuwa Ar-Ridhwaa alisema maneno kama hayo isipokuwa huu ni uongo mwingine wanaowazulia watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam).

 

 

 

Bibi Faatwimah Hakumsemesha Tena Abu Bakr?

 

Kutokana na ushahidi nitakaoutaja hapo chini tutaona kuwa zile kauli zinazosema kuwa Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) hakumsemesha tena Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) mpaka kufa kwake si kauli za kweli, bali ukweli ni kuwa alimsemesha na akaridhika naye kabla ya kufa kwake na ushahidi nitakaoutoa unatokana na hadithi zilizopokelewa kutoka pande zote mbili, yaani katika vitabu vya Mashia na vya Masunni.

 

Katika Fathul Bari 233/6, kitabu kinachosherehesha hadithi za Imam Al-Bukhaariy imeandikwa kuwa;

“Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikasirishwa na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa sababu alidhani kuwa Abu Bakr aliyasikia maneno hayo kutoka kwa mtu mwingine na hii ndiyo sababu iliyomfanya akasirike na asimsemeshe tena.

 

Na maana ya neno ‘asimsemeshe tena”, ni kuwa hakumsemesha tena kuhusu jambo hili la ardhi ya Fadak, kwa sababu imepokelewa kutoka kwa Al-Bayhaqiy kutoka kwa Ash-Sha’abiy hadithi sahihi inayoondoa tatizo hilo na kutuhakikishia kuwa Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliacha kumkasirikia Abu Bakr na akamsemesha, isipokuwa Bibi Faatwimah alishughulika sana na huzuni ya kufiwa na baba yake, kisha aliumwa sana mpaka alipofariki dunia.

 

Ama katika vitabu vya Mashia, imeandikwa katika kitabu ‘Mihjaajus Swaalihiy’, na vingine kuwa Abu Bakr alipoona kuwa Bibi Faatwimah amemkasirikia akamuendea mpaka nyumbani kwake na kumwambia:

“Maneno yako ni kweli, isipokuwa mimi nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) baada ya kukupeni nyinyi watu wa nyumba yake, akiwapa pia (katika mali hiyo) masikini na mafakiri na wasafiri wanaoishiwa. Nikataka kufanya kama alivyokuwa akifanya baba yako.”

Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema:

“WaLlaahi utafanya kama alivyokuwa akifanya?”

Akasema:

“WaLlaahi nitafanya hivyo – Mola wangu shuhudia”.

 

Bibi Faatwimah Akaridhika, Na Abu Bakr Akawa Anawapa Haki Yao Ndani Yake Kisha Kilichobaki Akikigawa Kwa Wanaostahiki.

 

 

 

Hitimisho

 

Kwa kumaliza tunasema kuwa;

Baada ya kutambua kuwa hadithi ya kutorithiwa Mitume (‘Alayhimu Ssalaam) ni sahihi upande wa Masunni na upande wa Mashia, tunaelewa pia kuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na haki alipokataa kumrithisha ardhi hiyo Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha), kwani hata hiyo aya inayozungumza juu ya mali ya Fa’iy, basi Allaah ameikamilisha kwa kusema:

“Na anachokupeni Mtume pokeeni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na muogopeni Allaah; kwa yakini Allaah ni Mkali wa kuadhibu”.

 

Tunaelewa pia kuwa urithi huo haukuwa haki ya Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) peke yake, bali ulikuwa wa watu wote wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) wakiwemo wake zake (Radhiya Llahu anhunna) na hapana hata mmoja kati yao aliyekwenda kuidai baada ya kufahamu maana ya hadithi hiyo.

 

Maswahaba wengi (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakiijuwa hadithi hiyo akiwemo Ali bin Abu Talib (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye hata alipotawala, yeye pia hakuirithisha ardhi hiyo, bali aliendelea kufanya kama alivyokuwa akifanya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) alimkasirikia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipodhani kuwa hakuisikia hadithi hiyo kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) lakini alipouelewa uhakika aliridhika na akaacha kuendelea kumkasirikia Abu Bakr.

 

 

 

Share