Mwanamume Aliyetembea Na Mke Wa Mtu vipi Atubie?

SWALI:

 

 

 

Assalaam aleykum. Mie nilikuwa nauliza jee? Mwanaume akitembea na mke wa mtu vipi atubie.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika ni kwamba hili ni swali zuri na nyeti na inabidi liwekwe wazi ili watu walipatie umuhimu na uzito unaopaswa kupewa.

 

Wamesema wanavyuoni: “Toba ni wajibu kwa kila dhambi. Ikiwa dhambi alolifanya mja ni baina yake mja na Allaah Aliyetukuka haliingiliani na haki ya binadamu, litakuwa na sharti tatu:

 

Ya kwanza: Kuacha maasiya.

Ya pili: Kujuta kwa kufanya hayo maasiya.

Ya tatu: Kuazimia kutorudia tena kosa lile milele. Likikosekana sharti moja katika hizi tatu basi toba haitosihi”.

 

Na ikiwa dhambi lililofanywa lina mafungamano na mwanadamu sharti za kupata toba zinakuwa ni nne: “Sharti hizi tatu zilizotajwa hapa juu na ya nne ni kuirudishia haki ya yule mtu, ikiwa ni mali au kitu chengine chochote umrudishie. Ikiwa umefanya hiyana kwa kulala au kuzini na mke wa mtu inabidi uombe msamaha kwa mume wa huyo mwanamke ili upate toba kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa dhambi lako hilo.

 

Ni wajibu kwa Muislamu kutubu (kuomba msamaha) kwa madhambi yote. Ikiwa atatubia baadhi ya dhambi husihi toba yake kwa dhambi ile na zinabaki zile zilizobakia. Zimedhihiri dalili katika Kitabu na Sunnah na Ijma’ ya Ummah katika uwajibu wa toba.

 

Allaah aliyetukuka amesema: “Na tubuni nyote kwa Allaah, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa” (24: 31).

 

Na toba inafaa iwe ya sawa na ya kweli kwani Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi mlioamini! Tubuni kwa Allaah toba iliyo ya kweli” (66: 8).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share