Mume Amezini Nami Nimechukia Nifanye Nini?

SWALI:

MUME WANGU AMEZINI NA MKE WA MTU BAADA YA KUGUNDUA MAANA NIMEPATA MASHTAKA KUTOKA KWA MTOTO WANGU WA KIUME KUA ALIMFUNGIA NDANI YAYA NILIVYOMUULIZA AKAPINGA SANA LAKINI NILIVYOMWAMBIA KUHUSU HUYO MWANAMKE AKUBALI KUA KWELI AMEZINI NA KUSEMA KUA NI IBILISI.NIKIFIKIRIA ROHO INANIUMA SANA MPAKA INAFIKIA NAHISI NAMCHUKIA KWA KUNIHUNI JE NIFANYE NINI?

 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tumepokea Swali lako kwa masikitiko ya hayo yaliyokusibu kuhusu mumeo.

Nasiha yetu ni kuwa kwanza mumeo alitakiwa afiche siri ya maasi aliyofanya kwa sababu Muislamu haimpasi kutaja siri ya maasi yake. Anatakiwa anapofanya maasi ni kujisitiri na kutubia kwa Mola Wake.

Tunafahamu kuwa jambo kama hilo ni la kumchukiza sana mtu na linatia ghadhabu kubwa. Lakini kama alivyokiri mwenyewe kuwa ni ibilisi aliyemchezea hadi akafika kufanya maasi hayo, na hivyo ni kawaida yake ibilisi kumtumbukiza mtu katika maasi. Kumbuka dada yetu kuwa baba yetu Adam ('alayhis-salaam) alishindiwa na ibilisi, alimhadaa hadi akamsababisha kuingia katika kumuasi Mola wake na ikawa ni sababu ya kutolewa Peponi. Naye Adam alirudi kwa Mola wake akatubu na Allaah Alimsamehe madhambi yake.

Hivyo ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasamehe waja Wake Aliowaumba na kuwaruzuku kila jema, iwe vipi sisi binaadamu tusiwe wenye kusamehe wenzetu?

Imekuwa ni kazi nyepesi kwa ibilisi kuwatumbukiza wanaume  katika maasi haya ya kuzini kwa vile wao ni dhaifu sana mbele ya wanawake. Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaruhusu wao waoe wake wanne wanapohitaji. Na wanawake ni fitna kubwa kwao. Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alionya:

عن أسامة بن زيد رضي الله عنهما : عن النبي صلى الله عليه وسلم قال : ((ما تركت بعدي فتنة أضر على الرجال من النساء))   . رواه البخاري   ومسلم   .

Kutoka kwa Usaamah bin Zayd  (Radhiya Allahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sijakuachieni baada  yangu fitna iliyo na madhara kwa wanaume kama wanawake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika kutaja mapambo na matamanio mengi ya binaadamu (wanaume), Ametaja kwanza ni huba ya kupenda wanawake:

((زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ الشَّهَوَاتِ مِنَ النِّسَاء وَالْبَنِينَ وَالْقَنَاطِيرِ الْمُقَنطَرَةِ مِنَ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ وَالْخَيْلِ الْمُسَوَّمَةِ وَالأَنْعَامِ وَالْحَرْثِ ذَلِكَ مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاللّهُ عِندَهُ حُسْنُ الْمَآبِ))

((Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Allah ndio kwenye marejeo mema)) [Al-'Imraan:14]

Udhaifu huu wao mbele ya wanawake umemfanya ibilisi iwe rahisi kwake kuwahadai wanaume katika maasi ya zinaa.   

Kwa hiyo, unatakiwa uwe na moyo wa msamaha na umsamehe mumeo madamu amekiri makosa yake. Kufanya hivyo utarudisha mapenzi yenu na muweze kuendelea na maisha yenu bila ya kuyaharibu. Kufanya hivyo naye atakuthamini zaidi na atachukua tahadhari zaidi ya kutokuingia katika maasi tena kama hayo.

Kumbuka vile vile kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Humpa mtu mwenye kuzuia ghadhabu na kusamehe daraja ya muhsiniyn (Wenye kufanya wema). Na daraja hii sio kila mtu anaweza kuipata kwa wepesi ila wenye moyo mkubwa wa kufanya hivyo, na bila ya shaka dada yetu nawe utakuwa ni miongoni mwa wenye sifa hii.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((ألَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاء وَالضَّرَّاء وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ))

((Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Allah Huwapenda wafanyao wema)) [Al-'Imraan:134]

 

Yanayompasa mume kufanya na Nasiha zetu kwake:

Anatakiwa atubie kwa Mola wake Tawba ya kweli, kwa kuazimia kuacha kutenda maasi hayo. Atambue kuwa maasi ya zina ni jambo Alilolikemea sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) bali Ametuonya hata tusikaribie zina. Hivyo inampasa akhofu kurudia kufanya maasi hayo. Asome mada zinazohusu uovu wa maasi hayo na adhabu zake, ili apate kinaa ya kuacha  kutenda. 

Vile vile amuombe msamaha mkewe na arudie kwake na aridhike na mkewe na ampe haki zake sawa sawa kama inavyompasa.

Vile vile jitahidi wewe umridhishe mumeo daima na uhakikishe kuwa huweki kasoro katika kutimiza wajibu wako kwake kwa kujiweka katika hali ya kupendeza kila mara na kumstarehesha ili asipate matamanio kwa mwengine zaidi yako. Bila shaka utakuwa unafanya hivyo, lakini tunakukumbusha uzidi kuongeza mapambo katika ndoa yako, kwa kujipamba mwili wako, na nyumba yako pia.

Kisha kaa naye uzungumze naye kwa uwazi bila ya hamaki kwa hayo yaliyotokea. Mjadiliane kwa vizuri ili mpate kutatua yaliyo baina yenu.

Kisha someni mada katika viungo vifuatavyo huenda mkapata nukta za kukumbusheni kuzidisha mapambo ya ndoa yenu.  

Jinsi Ya Kumfurahisha Mumeo

Jinsi Ya Kumfurahisha Mkeo

Tunakuombea ndoa ya furaha, amani na mapenzi baada ya  hayo yaliyotokea.

Na Allah Anajua zaidi

  

 

Share