Amezaa Nje Ya Ndoa, Mume Anajua Na Ameridhika, Mtoto Apewe Jina La Baba Yupi Kati Ya Wawili – Nini Hukmu Ya Mirathi?

SWALI:

 

Asalaa alaykum.

Mimi nina swali mbalo nimejaribu kulituma kupitia kwenye website yenu limekataa, hivyo basi ndio maana nimetumia private e-mail adr. Nilikua nauliza, Kama mume hamsikilizi mkewe kwa lolote lile. Mke akijaribu kuongea na mume lakini mume hataki hata kusikiliza, nakama alikua na safari basi huvaa viatu nakutoka. Na wakati mwengine kama mume alikua anangalia TV basi huongeza na sauti kabisa. Hali hiyo iliendelea mpaka siku moja mke akajikuta anatoka nje ya ndoa na kuzini. Wakati huohuo mke alimpenda sana mumewe na hakuchoka kupigana na hali hiyo.

 

Siku moja mume akamjia mkewe na kumuomba samahani kwa yote na akaomba wasameheane ili walee watoto wao wawili wa kiume. Na mke bila ya kusita wakasaeheana na wote wamekuwa ni wafanya ibada mchana na usiku kwa ajili ya kumuomba mwenyeezi mungu awasamehe madhambi yao waliyoyatenda na waliotendeana.

 

Na mume alifaham ya kwamba mkewe alikwenda nje ya ndoa. Lakini wakati huo mtihani mgumu ukawajia, mke alijikuta ni mja mzito wa mtu mwengine na akaogopa kumuambia mumewe. Na vile vile mke aliogopa dhambi ya kutoa mimba ni kama ya kuua hivyo basi akaamua kuzaa.

 

Baada ya mtoto kuzaliwa kukapita kama kipindi cha miaka miwili mke hana raha kwa sababu ya siri hiyo. Na mungu mkubwa mume huyo akaligundua hilo na kumuuliza mkewe na mke hakukataa akasema ukweli. Mume huyo alijilaumu sana ya kwamba yote hayo aliyasababisha yeye kutokusikilizana na mkewe.

 

Na akamuambia mkewe ya kwamba najua kwenda nje ilikua uamuzi wake hakuna aliyemshauri kufanya vile. Lakini kwa kuwa yeye ndio aliye lea ujauzito na mtoto mpaka akazaliwa na akafikisha miaka 2 basi yeye anaona ni bora wasameheane na waendelee kuishi na kulea watoto wao kama kawaida.

 

Sasa hali kama hiyo, kwa sababu baba mzazi wa mtoto huyo alifaham ya kwamba huyo mwanamke alikua mke wa mtu. Je baba huyo anastahili kupata haki kama baba? na kivipi?

 

Na je kama ilivyo kidini yetu mtoto huyo anastaili kutumia ubini upi, wa baba amleae au huyo baba mzazi? Vile vile mtoto ikibidi alitumie jina la baba mzazi je hali hiyo si inaweza ikasababisha baba mlezi kupata hasira na labda kutokea kumchukia mtoto huyo. Na haswa ukizingatia wote mke na mume wameamua kuwa wachamungu.

 

Halafu pia kwenye maswaala ya Mirathi inakuaje ikiwa mke na mume huyo wanashirikiana wote katika maswala ya kuzalisha mali kwa ajili ya watoto wao na urithi wao hapo baadae? Shukran.

 

Neema na Amani zake Allah ziwashukie ninyi mnaoutumia muda wenu kwakuielimisha jamii ya kiislam. Mwenyeezi mungu awazidishie kila la kheri hapa duniani na a kesho akhera, na pia awarahisishie yaliyoko magumu kwenu.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Mwanzo tunawapatia pongezi hao wanandoa ya kuweza kusameheana kwa yote yaliyopita baina yenu na kuanza maisha yetu mapya kwa kumuabudu Allaah Aliyetukuka na kuendea uchaji Allaah.

 

Hata hivyo, mara nyingi yanayotupata kisha tukajuta ni kwa yale yaliyochuma mikono yetu. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na misiba inayokupateni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu, na juu ya hivi Allaah Anasemehe mengi” [42: 30].

 

Kwa hiyo, yaliyopita yamepita lakini baada ya hapo wanatakiwa wasifanye makosa mengine, ambayo yanaonekana ya kwamba yatakuja kutokea kwa kuzaliwa mtoto huyo nje ya ndoa. Baba wa nje ya ndoa hana haki yoyote kwa mtoto anayezaliwa mbali na kwamba ni damu yake, shari'ah ya Kiislamu haimtambui kabisa.

 

Ama huyo mtoto, hatohusishwa na huyo mwanamme aliyezini na we, bali mtoto atahesabika kuwa ni mtoto wa mume wako japo umezaa nje ya ndoa. Na dalili ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

“Mtoto atahusishwa na mume (mwenye kitanda cha ndoa) na mzinifu hastahiki chochote.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hivyo, mumeo ndiye mwenye kuhusishwa na huyo mtoto na hilo halitofutika hadi mume amkatae huyo mtoto kuwa si wake kishariy’ah kwa njia ya Li’aan (taratibu za kishariy’ah za mtu kumkana mtoto kuwa si wake). Hilo ni kwa sababu misingi ya asli ya kishariy’ah, mtoto anahesabika ni wa yule mwenye kitanda (akikusudiwa mume halali wa mke wa ndoa) kama ilivyotangulia Hadiyth hapo juu.

 

Pia haifai huyo mtoto kuitwa kwa jina la mwanaume aliyemtia mimba huyo mke au huyo mume wa halali. Linalotakiwa ni huyo mtoto kuitwa kwa ubini wa mama yake au kwa ubini wa ‘Abdullaah. Kwa mfano ikiwa mtoto jina lake ni ‘Uthmaan, anaweza kuitwa ‘Uthmaan bin Maryam (kwa jina la mama) au ‘Uthmaan bin ‘Abdillaah.

 

Huyo mume  ndio atakuwa na haki ya ulezi kwani atakuwa ni kama baba yake kama Hadiyth juu ilivyoweka wazi, ilhali mzinifu aliyesababisha kuzaliwa mtoto huyo, hatokuwa na haki yoyote. Ama kuhusu mas-alah ya mirathi, mtoto huyo aliyezaliwa nje ya ndoa ataweza kumrithi huyo mume wa mama yake kwa mujibu wa dhahiri ya  Hadiyth hapo juu ilivyofahamika.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share