19-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kujitolea kwa kumlipia madeni Maiti

 
Kujitolea kwa kumlipia madeni Maiti:
 
 
Pindi atakapokufa maiti na ameacha madeni anayodaiwa na hakuacha mali ya kutosha kulipa madeni yale inapendeza watu wajitolee kumlipia madeni yale anayodaiwa.
 
Kutoka kwa Salama bin Al-akwaa (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema, ‘tulikuwa tumekaa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) zama ilipokuja jeneza na kutakiwa kuswalia, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza je, ana madeni? Wakajibu, ‘Hana’. Mtume akauliza tena je, ameacha chochote? Wakajibu, ‘Hapana’. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamswalia. Kisha likaja Jeneza lingine wakasema Ee, Mtume Tuswalie maiti huyu, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza, “Je, amewacha madeni?” wakajibu, ‘Ndiyo’ akauliza tena, “Je, amewacha chochote? Wakajibu, ‘Ndio ameacha Dinari tatu.’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamswalia.
Kisha likaja jeneza la tatu, watu wakamuomba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aswalie, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza, ‘Je, amewacha kitu.’ Wale watu wakajibu, ‘hakuacha chochote.’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akawauliza tena, “Je, amewacha madeni?” wakamjibu, ‘Ndio, anadaiwa Dinari tatu.’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akawaambia, “Mswalieni Sahibu yenu.” Abu Qatada akasema, “Ee Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) mswalie nami nitamlipia hilo deni lake hilo.” (Bukhari)
 
 
 Katika mapokezi mengine imepokewa kuwa Mtume hakumswalia hadi Abu Qatada alipomlipia lile deni alilokuwa anadaiwa yule maiti.
 
Hadithi hizi na mfano wake zina tupa dalili za wazi kuwa deni lisipolipwa linamzuilia maiti kheri nyingi sana na si hivyo tu, hali kadhalika inamzuilia na kuingia peponi, kama tunavyojifunza katika hadithi sahihi kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), ‘Je, nikiuliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu (jihadi ya vita) nikapambana na nikawa sijarudi nyuma Je, nitaingia peponi? Akawa anauliza hivyo mara tatu na Mtume humjibu, “Ndiyo” alipoondoka Mtume akamuita kisha akamwambia, “ila ukiwa una madeni, kwani Jibril ameniambia hivyo sasa hivi.”
 
Share