Jirani Kafiri Anatubughudhi Sana Tumuombee Du’aa Gani?

SWALI:

 

Assalaam alaykum,

 

Nina jirani ambae anatubughudhi

sana (SI MUISLAMU) mimi na aila yangu kwa muda mrefu sasa. tumejaribu kila mbinu kuzungumza nae aachane na maovu na pia kutubughudhi lakini nimeshindwa. Anaonekana kushinda kila wakati tukitaka kimshitaki mbele ya serekali. Tumekosa raha, tunapata maradhi kwa ajili yake.

Kuna dua ya kumuomba Allaah atusaidie, mtume (saw) najuwa alibughudhiwa sana, alikuwa na dua maalum akisoma??? hili ni tatizo kubwa sana ambalo linaharibu familia yetu kiasi kikubwa sana. Tafadhali tupe mawazo

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

 

 

Shukrani zetu kwako ewe ndugu yetu kwa swali lako. Hakika ni kuwa mitihani ni jambo la kawaida kwa mwanaadamu na hasa Waislamu. Hili ni jambo ambalo haliwezi kukosekana katika maisha ya mwanaadamu katika dunia hii. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea: “Hakika jazaa kubwa ni pamoja na mtihani na misukosuko, na hakika Allaah Aliyetukuka Anapoipenda kaumu huipatia mtihani” [At-Tirmidhiy, aliyesema kuwa ni Hadiyth nzuri (Hasan)].

 

Na Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

  ((أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ))  

 ((وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ))  

 

((Je, mwanaadamu anadhani ataachwa tu kwa kusema kuwa nimeamini naye hajapatiwa mtihani?))

 

(Hakika Tumewapatia mitihani na kuwatia katika taabu waliokuwa kabla yenu, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha wale walio wakweli na wale walio waongo))  [Ar-Ruum: 29: 2 – 3].

 

 

Vilevile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuhimiza tumfanyie wema jirani katika Aayah kadhaa, Anasema:

 

((وَاعْبُدُواْ اللّهَ وَلاَ تُشْرِكُواْ بِهِ شَيْئًا وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَى وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالجَنبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ إِنَّ اللّهَ لاَ يُحِبُّ مَن كَانَ مُخْتَالاً ))

 

((Muabuduni Allaah wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Allaah Hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri)) [An-Nisaa: 36]

 

Tunaona kwamba kumfanyia wema khaswa jirani aliye karibu na ndipo Mama wa Waumini 'Aishah (Radhiya Allaahu 'anha) alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutaka kujua yupi jirani mwenye haki zaidi naye:

 

 عن عائشة رضي الله عنها وقالت له: ((يا رسول الله! إن لي جارين فإلى أيهما أهدي؟ قال: إلى أقربهما منك باباً))  رواه البخاري

 

Kutoka kwa Mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) aliuliza: "Ee Mjumbe wa Allaah, nnao jirani wawili, yupi miongoni mwao nimpe zawadi" Akanijibu: ((Aliye karibu na mlango wako [aliye karibu zaidi])) [Al-Bukhaariy]

 

Kuwa na jirani muovu ni mojawapo ya mitihani migumu. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akahimiza sana mtu kumtendea wema jirani yake kwani kutendana maovu kutaleta vurugu na ukosefu wa amani. Wema huu Muislamu anatakiwa amtendee kila jirani ikiwa ni Muislamu au si Muislamu. Miongoni mwa kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni:

 

 ((من كان يؤمن بالله واليوم الآخر فليحسن إلى جاره))   البخاري و مسلم

 

((Yeyote mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho basi amkirimu jirani yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Miongoni mwa njia bora za kuweza kuvunja makali ya adui ni kusuburi, kutenda mema, kutekeleza 'Ibaadah, na kumtendea wema huyo adui mbali na yale maovu anayokufanyia. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

 

((وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ))

(( وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ))

 ((وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ))

 

((Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye kwa Allaah na mwenyewe kafanya vitendo vizuri na akasema: ‘Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu’.))

 

((Mambo mazuri na mabaya hayawi sawa. Ondosha ubaya unaofanyiwa kwa mema, tahamaki yule ambaye baina yako na yake kuna uadui atakuwa kama ni jamaa yako mwenye kukufia uchungu))

 

((Lakini jambo hili hawatopewa ila wale wanaosubiri, wala hawatapewa ile wenye hadhi kubwa)) [Fusw-swilat 41: 33 – 35].

 

Anasema tena Aliyetukuka:

 

((وَاسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاَةِ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلاَّ عَلَى الْخَاشِعِينَ))

 

((Na jisaidieni katika mambo yenu kwa kusubiri na kwa kuswali, na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu)) [Al-Baqarah 2: 45).

 

Kama ulivyotaja kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alibughudhiwa na kuteswa kwa kiasi kikubwa kuliko mtu mwengine yeyote lakini alivumilia na mwishowe aliweza kuwateka mahasimu wake wakubwa kama kina Abuu Sufyaan, Hind bint 'Utbah na wengineo na baada ya hapo wakawa wafuasi wake wakuu. Usikate tamaa kabisa kwani ushindi itakuwa ni wako dhidi yake leo au kesho.

 

Msijitie maradhi kabisa kuhusu suala hilo bali mfanyieni wema na mpuuze maudhi yake kwa kuyafanya si lolote si chochote. Jaribuni tena kumfanyia wema kwa kumpelekea hadiya, mzuruni akiwa na msiba au mgonjwa na kadhalika. lakini kwa sharti la kumlingania aingie kwenye Dini ya Haki, kama alivyofanya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokwenda kumzuru yule mtoto wa Kiyahudi aliyekuwa akimbughudhi kila mara, na alipomzuru alimlingania aingie kwenye Uislamu.  

 

Ikiwa yote hayo hayakufaa kitu basi someni du’aa zifuatazo aliyotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

1-Du'aa ifuatayo aliyokuwa akijinga na jirani muovu kama alivyokuwa akiomba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

  ((اللهم إني أعوذ بك من جار السوء في دار المقامة، فإن جار البادية يتحول)) حديث صحيح، رواه ابن حبان، والحاكم وصححه الذهبي والألباي

((Allaahumma Inniy audhu Bika min jaaris-suu fiy daaril-muqaamah, fainna jaaral-baadiyah yatahawwal

[Ee Allaah, najikinga Kwako na jirani muovu katika makazi ya kudumu kwani jirani wa jangwani hubadilika badilika kuhama)) [Hadiyth Swahiyh aliyosimulia Ibn Maajah, Al-Haakim na akaipa daraja ya Swahiyh Shaykh al-Albaaniy]

 

 

2- Vile vile alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiomba:

 

اللهم إني أعوذ بك من يوم السوء، ومن ليلة السوء، ومن ساعة السوء، ومن صاحب السوء، ومن جار السوء في دار المقامة .

((Allaahumma Inniy audhu Bika min yawmis-suu, wa min laylatis-suu, wa min saa'atis-suu, wa min swaahibis-suu, wa min jaaris-suu fiy daaril-muqaamah

Ee Allaah najikinga Kwako na siku ovu, na usiku muovu, na saa ovu, na rafiki muovu, na jirani muovu katika makazi ya kudumu))

 

3- Na du'aa ifutayo (japo Wanachuoni wametofautiana usahihi wake) ambayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliisoma aliporudi kutoka Twaaif baada ya kupata maudhi na watu wa mji huo, kwa kumpiga mawe, kumtukana na kumfukuza:

 

اَلَّلهُمَّ إِنِّي  أَشْكُو إِلَيْكَ ضَعْفَ قُوَّتِي, وَقِلَّةَ حِيْلَتِي, وَهَوَانِي عَلَى النَّاسِ, يَا أَرْحَمَ الرَّاحِمِين, أَنْتَ رَبُّ الْمُسْتَضْعَفِينَ وَاَنْتَ رَبّي إِلَى مَنْ تَكِلْنِي؟ إِلَى بَعِيدٍ يَتَجَهَّمُنِي أَمٍ إِلَى عَدُوٍ مَلَّكْتَهُ أَمْرِي؟ إِنْ لَمْ يَكُنْ بِكَ غَضَبٌ عَلَىَّ فَلاَ أُبَاِلي، وَلَكِنَّ عَافِيَتَكَ أَوْسَعُ لِي مِنْ ذُنُوبِي,  أَسْأَلُكَ بِنُورِ وَجْهِكَ الَّذِي أَشْرَقَتْ لَهُ الظُّلُمَاتُ، وَصَلَحَ عَلَيْهِ أَمْرُ الدُّنْيَا وَالأَخِرَةِ مِنْ أَنْ يُنْزِلَ عَلَيَّ غَضَبُكَ أَوْ يَحِلُّ عَلَىَّ سَخَطُُكَ   وَلاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِكَ      

((Allaahumma Inniy Ashkuu Ilayka Dhwa'fa Quwwatiy, Wa Qillata Hiylatiy, Wa Hawaaniy 'Alan-Naas.  Yaa Arhamar-Raahimiyn.  Anta Rabbul-Mustadhw'afiyn, Wa Anta Rabbiy Ilaa Man Takilniy?  Ilaa Ba'iydin Yatajahhamuniy? Am Ilaa 'Aduwwim-Mallaktahu Amriy?  In-lam Yakun Bika Ghadhwabun 'Alayya Falaa Ubaaliy, Wa Laakin 'Aafiyataka Awsa'u Liy Min Dhunuubiy.  As-aluka Binuuri Wajhika-lladhiy Ashraqat Lahudh-Dhwulumaat, Wa  Swalaha 'Alayhi Amrud-Duniyaa Wal-Aakhiratiy Min Ay-yunzila 'Alayya Ghadhwabuka Aw Yahillu 'Alayya Sakhatwuka, Wa Laa Hawlaa Walaa Quwwata Illaa Bik.   

Ya Allaah, Kwako peke Yako nalalamika udhaifu wa nguvu zangu, na uchache wa uwezo wangu na unyonge wangu (wa kukabili adha) za watu.  Wewe Ndiye Mwenye wingi wa Rehma na wingi wa Huruma na Upole.

Wewe ni Mola wa wasiojiweza na wadhaifu. Nawe ni Mola Wangu. Unanitupa kwenye mikono ya nani (atakayenisaidia)? Kwenye mikono ya jamaa yangu aliye mbali na asiye na huruma na mimi?  Ambaye ananihamakia kwa chuki na kunidharau? Au kwenye adui aliyepewa utawala juu ya mambo yangu? Lakini kama ghadhabu Yako haitoanguka kwangu au haitonifikia basi hakuna kitu nitakachojali. Na hakika msamaha Wako ni mkubwa kuliko dhambi zangu.     

Nakuomba kutokana na Nuru ya Wajihi Wako, ambayo inaangazia mbingu na inaondoa kiza na kutawala mambo yote ya dunia na akhera ili hasira Yako isinifikie au ghadhabu Yako isiniangukie. Na hakuna mamlaka wala nguvu na uwezo ila Wako peke Yako.))

 

Pia omba usaidizi kwa kukithirisha du’aa baada ya kila Swalah, unapoinuka usiku kwa Tahajjud na katika mwezi huu wa Ramadhwaan unapokuwa katika Swawm.

 

Ikiwa hukupata afueni lakini kwa njia hizo za kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) bila shaka utapata nafuu kubwa. Lakini ikiwa kinyume utambue kuwa huo ni mtihani mwingine kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), hivyo itabidi labda uamue kuhama sehemu hiyo.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusahilishie tatizo hilo na Akutolee njia muafaka, Aamiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share