Wake Wa Ndugu Wawili Waliogombana, Ni Haki Kuvunja Mawasiliano?

SWALI:

 

ASALAMU ALAYKUM .Mmoja wa jirani wangu ana mke mweza waume zao ndugu mmoja alimpigia simu mwenzake akamueleza maneno unapita ukinisema sitaki yakaanza majibizano wakagombana ndani ya simu yule mmoja aliporudi mumewe akamueleza, fulani kanipigia simu kanitukana mumewe akampigia simu kaka yake akamualeza. Basi yule mume wa aliyempigia simu mwenzake akamwambia mke wake. WALWAHI UKIMPIGIA SIMU NA KUMTUKANA NAKUWACHA. JE NINI HUKUMU YA MANENO HAYA. JE YULE MWANAMKE ALIAAMBIWA VILE HAWEZI KUMPIGIA SIMU TENA MWENZAKE


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu wake wa ndugu waliogombezana katika simu na maneno kuwafikia waume zao.

Mwanzo ni kuwapatia Waislamu wote nasaha ya kujaribu sana kutoghadhibika na mtu akikasirika basi ajitahidi kujizuia ili aweze kuimiliki nafsi yake ili asivuke mipaka ya Dini yetu.

 

Kutusiana ni jambo la makosa na dhambi katika Uislamu kwa hali zote – wakati wa amani au vita, wakati wa utulivu au kinyume chake au pia wakati wa hasira. Kufanya hivyo kunaweza kumpeleka mtu motoni, hivyo tujitahadhari sanasana. Kinachotakiwa sasa ni watu wenye busara kama wazazi, wanavyuoni kuingia kati na kusawazisha gogoro hilo.

 

Ama kauli ya mume aliyomuambia mkewe kwa kula yamini, “WALLAHI UKIMPIGIA SIMU NA KUMTUKANA NAKUWACHA”, ina maana ya kuwa mume atafikiria kumuacha mkewe akifanya hivyo. Na kauli hii ingekuwa na maana tofauti lau angesema: “WALLAHI UKIMPIGIA SIMU NA KUMTUKANA NIMEKUWACHA”. Hii ina maana ikiwa mkewe atampigia simu mke wa nduguye na kumtukana basi ameachika hapo hapo. Hii ya pili ni talaka iliyowekewa sharti na hupita kukipatikana sharti hilo.

 

Kwa hivyo, maneno hayo aliyosema ya awali hayana athari yoyote na wala mke huyo hakukatazwa kumpigia simu huyo mke wa shemeji yake ila tu anapopiga asiwe ni mwenye kutukana.

 

Kitu muhimu kwa wakati huu ni hao wanawake wa ndugu kupatanishwa na waonywe tabia hiyo ya kutukanana isiendelee na kuwepo na maelewano baina yao angalau ya kuzuia shari kutokuwepo kwani hizo si tabia za Kiislamu. Waislamu wanapaswa waishi kwa amani na mapenzi, n kukiwa hakuwezekani jambo kama hilo basi angalau kusiwe na shari na maudhi baina yao.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

 

Fadhila Za Kusuluhisha Waliogombana-1

 

Fadhila Za Kusuluhisha Waliogombana-2

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share