16-Uswuul Al-Fiqhi: Sura Ya Tatu - Utungaji Sheria Baada Ya Kipindi Cha Maswahaba

 

UTUNGAJI SHERIA BAADA YA KIPINDI CHA MASWAHABA

 

Kipindi cha Swahaabah kilifikia hatamu baina ya mwaka 90-100 H, na kufuatiwa na kipindi cha Taabi’uun ambapo wanazuoni wake walianza kuwa na majukumu kwenye Fiqhi na kutoa Fataawa. Swahaabah wa mwisho wa Kuufah alifariki mwaka 86 au 87 H. Wa mwisho kwa Madiynah, ni Sahl bin Saa’d as-Saa’di, alifariki mwaka 91 H. Wa mwisho kwa Baswrah, ni Aanas bin Maalik, alifariki mwaka 91 H (wengine wanasema mwaka 93 H). Wa mwisho kwa Damascus, ‘Abdullaah bin Yusr, alifariki mwaka 88 H. Wa mwisho katika Swahaabah wote ni ‘Aamir bin Wathillah bin ‘Abdillaah (Abuu Twufayl), alifariki mwaka 100 H.

 

Hapo tena, wale waliokuja kuwa na jukumu la kutoa Fataawa walikuwa ni watu huru Mawaalii, wengi miongoni mwao wamewahi kuishi pamoja na Fuqaaha miongoni mwa Swahaabah, kama vile: Naafi’i, aliyeachwa huru na Ibn ‘Umar, ‘Ikrimah aliyeachiwa huru na Ibn ‘Abbaas, ‘Atwaa bin Rabbaah, Faqiyh (mwanachuoni wa sheria) wa Makkah; Twaawuus, Faqiyh wa Yamaamah. Ibraahiym an-Nakha’iy, Faqiyh wa Kuufah; Hasan al-Baswriy Faqiyh wa Baswrah na Ibn Siyriyn ambaye pia ni Faqiyh wa Baswrah; ‘Atwaa al-Khurasaaniy wa Khurasaan, na wengineo. Hakika, Madiynah ilikuwa ni ya aina yake kwa kuwa na Faqiyh wa ki-Quraysh, Sai’yd bin al-Musayyab.

 

Taabi’uun hawa, kwa uchache sana walibadili Fataawa za Swahaabah ambao kutokana nao wamepata elimu yao, hivyo ni vigumu kupata tofauti baina ya taratibu zao za kufikia maamuzi na za mababu zao. Hata hivyo, taratibu za kufikia maamuzi zilikuwa, kwa kipindi hichi, zinaanza kukua na, katika kuendelea kwake, zimekuwa wazi kuliko hapo kabla.

 

Imesimuliwa kwamba Hasan bin ‘Ubaydullaah an-Nakha’iy alisema: Nilimuuliza Ibraahiym an-Nakha’iy: “Umesikia kutoka wengine Fataawa zote ambazo nimesikia wewe ukitoa?” Alisema: “Hapana” Nilimuuliza “Hivyo wewe unatoa Fataawa ambazo hujazisikia?” Alisema: “Nimesikia nilichofanikiwa kusikia; lakini nilipokutana na masuala kuhusiana na yale nisiyowahi kuyasikia kitu, nilitofautisha, kwa kufananisha, pamoja na masuala niliyowahi kusikia[1].”

 

Miongoni mwa sifa zenye maana kwa kipindi hichi ni kuibuka kwa tofauti za maoni baina ya wanazuoni Wakishia kwenye masuala tofauti. Hili linaweza kuwekwa wazi kwa maamuzi mawili yaliyochukuliwa na Khaliyfah wa wakati huu, ‘Umar bin Abdil-‘Aziyz.

 

1.      Aliamrisha kwamba mwenendo uliosifiwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukusanywe na kuwekwa kwenye maandishi. Kwa sababu hiyo, watu wa kila jimbo waliandika vitabu wanavyotambua kuwa ni sehemu ya Sunnah[2].

2.      Alizuia mamlaka ya kutoa Fataawa, kwenye wilaya nyingi; kwa watu wachache waliotajwa kwa majina, kama alivyofanya nchini Misri, pale alipotaja majina matatu tu kwa lengo hili. Cha kushangaza, wawili miongoni mwao walikuwa huru, Yaziyd bin Abi Habiyb na Abdullaah bin Abi Ja’afar, na wa tatu alikuwa ni Mwarabu, Ja’afar bin Rabi’ah. Khalifyah alipoulizwa kuhusu uteuzi wa watu wawili walio huru na Mwarabu mmoja tu, alijibu: “Ni kosa gani la kwangu kama watu hao walio huru wanajiendeleza wao wenyewe na nyinyi hamfanyi hivyo[3].”

 

Katika barua yake kwa Abuu Bakr, Muhammad bin ‘Aam bin Hazm al-Ansaarii, Khaliyfah huyo alieleza sababu zake za kuamrisha kwamba mwenendo uliosifiwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uwekwe kwenye maandishi. Aliandika: “Angalia kwa Hadiyth yoyote ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au Sunnah au mwenendo unaoweza kutafuta. Baadaye weka kwenye maandishi kwa ajili yangu; kwani nakhofia kwamba elimu hii itapotea kutokana na kufariki kwa wanachuoni[4].”

 

 

BAADA YA TAABI’UUN:

 

KIPINDI CHA MAIMAMU MUJTAHIDIYN

 

Kipindi hichi kilitambuliwa na Shah WaliyuLlaah ad-Dahlawiy kama ifuatavyo:

 

Fuqaaha wa kipindi hichi walichukua Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), maamuzi ya majaji wa mwanzo, na utambuzi wa kisheria wa Swahaabah, Taabi’uun na kizazi cha tatu, baadaye walitoa Ijtihaad zao wenywe.”

 

Huo ndio mtindo wa wanazuoni wa kisheria wa wakati huo walivyofanya kazi. Kimsingi, wote wao walikubali vyote, Hadiyth za Musnad[5] na pia Mursal[6].

Juu ya yote hayo, imekuwa ni tabia yao kutaja mawazo ya Swahaabah na Taabi’uun kama ni ushahidi. Kimsingi, kulikuwa na sababu mbili kwa hili:

 

1.     Mawazo kama hayo, yalikuwa hakika ni Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo imesimuliwa na mmoja wa Swahaabah au Taabi’uun ambaye kwa kukhofia kugeuza maneno, hawakuthubutu kuinasibisha Hadiyth kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

2.     Yawezekana sababu nyengine ni kwamba mawazo kama hayo yalitolewa na Swahaabah kutoka katika maandiko ya Hadiyth na kuwasilisha ufahamu wao wa Sunnah.

 

Bila ya shaka, kwa mfumo huu, hao Swahaabah walikuwa ni bora kuliko wale waliofuatia baadaye, kwa sababu walimfahamu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwa hivyo walikuwa na uwezo zaidi wa kuyatolea maana kila alichozungumza. Hivyo, maamuzi na mawazo yao yalikubaliwa kama ni yenye nguvu, isipokuwa kwenye kesi ambapo wao wenyewe walitofautiana, au pale ambapo matamko yao yalikuwa na mgongano ulio wazi kwa Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyothabiti.

 

Kwa upande mwengine, kwenye masuala ambapo Hadiyth mbili au zaidi ziligongana, wanazuoni watarudi kwenye maoni ya Swahaabah ili kutambua ipi miongoni mwa hizo Hadiyth mbili zilikuwa ni sahihi. Hivyo, kama Swahaabah alisema kwamba Hadiyth imebatilishwa, au haikuwa yenye kufahamika kimaana; au kama hawakutamka kwa uwazi kitu chochote kuhusiana na Hadiyth, lakini wameidharau, na haikuendana sambamba na ulinganifu wake, hivyo kuonesha kwamba Hadiyth hiyo ilikuwa kwa upande fulani ina kasoro, na kwamba ilikuwa haiendani na hali halisi, au kwamba tafsiri yake ilikuwa ni nyingine isiyokuwa ya maana hiyo, basi Maimamu Mujtahidiyn wataridhika na maoni yao.

 

Pale matamko ya Swahaabah na Taabi’uun yalipotofautiana kwenye suala lolote, basi kila Faqiyh atafuata maamuzi ya wale wanaotoka wilaya hiyo hiyo kama alivyo yeye, na walimu wake, kwa sababu atakuwa na uwezo zaidi wa kupambanua usahihi wake, kutegemeana na ukaribu wake na wasimulizi, wa mawazo na maelezo yaliyomfikia yeye katika mamlaka yao. Vivyo hivyo, Faqiyh huyo atakuwa amejengeka vizuri na utaratibu wao wa kisheria.

 

Elimu ya dhana ya sheria iliegemezwa kwenye mawazo ya ‘Umar, ‘Uthmaan, Ibn ‘Umar, ‘Aishah, Ibn ‘Abbaas na Zayd bin Thaabit, na wafuasi wao kutoka miongoni mwa Taabi’uun, kama az-Zubayr (amefariki mwaka 94), Saalim (amefariki mwaka 106), Atwaa’ bin Yassaar (amefariki mwaka 103), Qaassim bin Muhammad (amefariki mwaka 103), ‘Ubaydullaah bin ‘Abdullaah(amefariki mwaka 99), al Zuhri (amefariki mwaka 124), Yahya bin Sa’ad (amefariki mwaka 143), Zayd bin Aslam (amefariki mwaka 136) na Rabi’at ar-Ra’i (amefariki mwaka 136), ilikuwa ni elimu inayokubalika zaidi kwa watu wa Madiynah. Ilikuwa kwa sababu hii ambapo Imaam Maalik aliegemeza hoja zake za kisheria kwenye mafundisho yao.

 

Namna hiyo, mawazo ya ‘Abdullaah bin Mas’uud na wafuasi wake, maamuzi ya Khaliyfah ‘Aliy, Shurayh (amefariki mwaka 77 H), na ash-Sha’abiy (amefariki mwaka 104 H), na Fataawa za Ibraahiym an-Nakha’iy (amefariki mwaka 96H), yalikuwa ni yenye kukubalika kwa watu wa Kuufah.

 

Akifafanua jambo hili, Shaah WaliyuLlaah ad-Dahlaawiy ameandika: Pale Masruuq (amefariki mwaka 63H) alipofuata mawazo ya Zayd bin Thaabit kuhusiana na mgawano wa mirathi baina ya babu na ndugu (wa merehemu), ‘Alqamah (amefariki mwaka 62 H) alimuuliza, “Jee yupo miongoni mwenu aliye mjuzi zaidi kuliko ‘Abdullaah bin Mas’uud?

 

Masruuq alijibu, “Hapana, lakini Zayd bin Thaabit na watu wa Madiynah wanagawa mirathi baina ya babu na ndugu…

 

Hivyo, kama watu wa Madiynah walikubaliana na jambo, wanazuoni wa kizazi wanaofuata, hao Taabi’uun walikubali kwa uthabiti. Hivyo ndivyo Maalik alivyoaamrisha pale aliposema: “Sunnah ambayo sisi, watu wa Madiynah, hatukutofautiana ni kadhaa na kadhaa.”

 

Ama ikiwa wanazuoni hao wa mwanzo kutoka Madiynah watakhitalifiana kuhusu jambo lolote, wanazuoni waliofuata watafuata mawazo yao ambayo yalikuwa na nguvu na yanaweza kutegemewa zaidi; aidha kwa mnasaba wa kwamba yanatumika na idadi kubwa ya wanazuoni wa mwanzo, au kwa kuwa ni toleo la mfanano wa kisheria wenye kuleta maana, al-Qiyaas, au ambayo imefikiwa kutoka maandiko fulani ndani ya Qur-aan au Sunnah. Ni mtindo huu ambapo Maalik anamaanisha pale anaposema: “Hili ni zuri zaidi kwa nilichosikia.” Baadaye, kama wanazuoni wanaofuata hawatopata suluhisho lolote kwenye tatizo ndani ya kazi ya mababu zao, wao wenyewe wataelekea kwenye maandiko yenye kufaa ili kutengeneza mawazo yao ya kisheria.

 

Kwa wakati huu, wanazuoni walishajiika kuanza kuweka vitu katika kumbukumbu kwa maandishi. Hivyo Maalik (amefariki mwaka 179)

Madiynah, Ibn Abi Dhi’ib (amefariki mwaka 158), Bin Jurayj (amefariki mwaka 150?) na Bin ‘Uyaynah (amefariki mwaka 196) Makkah, ath-Thawriy (amefariki mwaka 161) Kuufah, na Rabi’i bin Subayh (amefariki mwaka 160) Baswrah, walioanza kuandika vitu, na wote walifuata utaratibu huo.

 

Pale Khaliyfah, Mansuur, alipotekeleza Hajj na kukutana na al Imaam Maalik, alisema: “Nimeamua kuamuru kwamba nakala zitengenezwe za vitabu hivi ulivyoandika. Nitakutumia nakala kwa kila mkoa wa ulimwengu wa Waislamu na ili wanazuoni waendane kwa mujibu wa hivyo na sio kurudia kwenye kazi nyengine zozote.

 

Maalik alisema: “Ewe Amiyrul Muuminiyn, usifanye hivyo! Watu tayari wamekwishasikia mawazo tofauti ya kisheria na kusikiliza Hadiyth na masimulizi; na wameridhika na chochote kilichowafikia mwanzo, kwa hivyo hili limechangia kwa khitilafu katika mtindo wa desturi zao miongoni mwa watu. Achilia mbali wale watu wa kila mtaa kwa kuwa na chaguzi ambazo wamekwishafanya.

 

Simulizi hiyo hiyo inatolewa kwa kumrudia Khaliyfah, Haaruun ar-Raashiyd, kwamba alitaka kuwalazimisha watu kuwafuata Muwattwaa’.

 

Lakini Maalik alimwambia: “Usifanye hivyo, kwa sababu Swahaabah wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walitofautiana kwenye Sunnah. Baadaye walitawanyika na kuketi sehemu tofauti za Ulimwengu wa Waislamu; na sasa njia zao za khitilafu zimesimamishwa madhubuti kabisa.

 

…Maalik alikuwa ni mwenye elimu bora kuhusu Hadiyth zilizosimuliwa na watu wa Madiynah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mfuatano wa wasimulizi wa Maalik ulikuwa wenye kutegemewa zaidi. Alikuwa pia ni mwenye elimu bora kuhusu maamuzi ya ‘Umar na matamko ya kisheria ya ‘Abdullaah bin ‘Umar na ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anhum) na wafuasi wao kutoka miongoni mwa Fuqaaha saba. Sayansi ya usimulizi wa Hadiyth na Fataawa ziliegemezwa kwenye elimu ya Maalik na mfano wake yeye.

 

Abuu Haniyfah alikuwa ni mbora wa kujitolea katika kutoa maana za kisheria za Ibraahiym an-Nakha’iy na, kwa mara chache watakhalifu hoja zao. Alikuwa ni mzuri mno katika kutoa maamuzi kwa kutumia mtindo wa Ibraahiym, vile vile katika kutumia utaratibu huo ili kufanyia kazi maelezo ya kesi za sheria.

 

Kama utapendelea kuelewa ukweli kuhusu tulichokieleza, basi fupisha mafundisho ya Ibraahiym na majeshi yake kama yalivyoandikwa kwenye kazi zifuatazo: Al-Aathaar “Desturi” cha Muhammad ash-Shaybaniy, Jaami’ “Muhtasari Uliokamilika” cha ‘Abdur-Razzaaq na Muswannaf “Mtungo wa maandiko” cha Ibn Abi Shaybah, na zilinganishe pamoja na maoni rasmi ya Abuu Haniyfah. Hakika, utakuta kwamba Abuu Haniyfah yupo mbali kidogo na njia zao, na hata hvyo maoni yake hayakutofautiana na maoni ya wanazuoni kutoka Kuufah[7].”

 

Hakika, maoni ya ad-Dahlawi yanahitaji kuangaliwa kwa makini. Alikuwa ni mwenye pupa kueleza kwamba al-Imaam Maalik na Abuu Haniyfah, na wafuasi wao, walikuwa wapo juu au chini zaidi kukubaliana na maoni ya Taabi’uun na Swahaabah kabla yao (kinyume na kufikia Ijtihaad yao), na hawakuruka mipaka ya misingi ya sheria za mababu zao. Hili, hata hivyo, ni hitimisho ambalo si rahisi kukubaliana.

 

Ni uwazi unaotambulika kwamba kuna njia tofauti za kuiendea Fiqh; na kila mmoja wa Maimamu alibuni njia tofauti kwa somo hilo. Sio jambo lililo rahisi kudai kwamba hizi zilichukuliwa kutoka kwa Swahaabah na Taabi’uun. Angalia, kwa mfano, utaratibu wa Maalik katika kutumia desturi na mila za watu wa Madiynah kama ni chanzo (kidogo) cha kutunga sheria; au matumizi ya Abuu Haniyfah katika Istihsaan na ‘Urf[8].

 

Juu ya hivyo, hamna hata mmoja wao aliyeegemeza hoja zake kwenye Fataawa za Taabi’uun, lakini badala yake walishindana nao, wakisema “Walikuwa ni watu (wa elimu) na sisi pia.”

 

Kwa kuongezea, tofauti na yeyote kabla yao, kila mmoja ameweka wazi kifungu cha masharti ya kukubaliana na Hadiyth kuwa sahihi.

 

Juu ya hivyo, tokeo la kuongezeka usambazaji wa Hadiyth wakati huo, kwa kuongezea na kutokea kwa Hadiyth ambazo hazijapata kusambazwa hata siku moja, zimepelekea, kwa upande mwengine wa maamuzi ya kisheria na nafasi ambayo ni tofuati kabisa na zile zilizokamatwa na Swahaabah.

 



[1] Ibn Hajar, Al-Iswaabah, IV, 112; na Ibn ‘Abdul Barr, Al-Isti’aab (juu ya mstari wa Al-Iswaabah) uk. 145.

[2] Ibn Abdul Barr, Jaami’ Bayaan al ‘iIlm, I, uk. 33.

[3] Al-Maqriizi, Khuttat, IV, uk. 143.

[4] Barua hii ilisimuliwa na al-Imaam al-Bukhaariy ndani ya Swahiyh yake bila ya mfuatano wa wasimulizi ulio rasmi (yaani Ta’liqa kama ni Mu’allaq Hadiyth). Pia, iliingizwa na al-Imaam Maalik ndani ya Muwattwaa yake; Angalia maoni ya Zarqaani, I, uk. 10.

[5] Al-Musnad: Ni Hadiyth yenye mfuatano uliokatika wa wasimulizi kwendea nyuma hadi kumfikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

[6] Al-Mursal: Ni Hadiyth ambayo mfuatano wake wa wasimulizi mwishoni umekatika, yaani ni ile inayoelezwa na Tabi’i kama imetoka moja kwa moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakika, kama upo uwezekana wa Tabi’i kutoisikia Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi Hadiyth aliyoisimulia kwa mtindo huu, hakika imesimuliwa kwake aidha na Tabi’i mwengine, au kutoka kwa mmoja miongoni mwa Swahaabah. Lakini kwa vile mwanachuoni Tabi’i hana mashaka kuhusiana na uadilifu wa mmoja kutoka kwa yule aliyemsimulia Hadiyth ameona haina haja ya kumtaja jina. Kwa vizazi vinavyofuata vya wanazuoni wa Fiqh na Hadiyth. Hata liwe suala la ama Hadiyth Mursal kuweza kukubalika lilikuwa ni jambo gumu. Sababu ya umakini wao ni kwamba; mfuatano wa Hadiyth hiyo ni, kubwa lao, mfuatano uliokatika; na hakuna shaka kwamba, kama msimulizi wa Tabi’i amepokea Hadiyth kutoka kwa kizazi chake chengine, kwamba huyo Tabi’i ni msimuliaji anayetegemewa. Hata hivyo, kwa hao wanazuoni wa Fiqh na Hadiyth wa kizazi cha mwanzo, halikuwa ni tatizo kubwa sana, kwani walikuwa wamewazoea wasimuliaji wa Tabi’i na Shuyuukh kutokana na yule waliyemsikia na kuipokea Hadiyth. Hivyo, ma-Imaam wawili Abuu Haniyfah na Maalik wanaikubali Hadiyth ya Mursal; ilhali Maimamu wawili waliofuata, yaani ash-Shafi’i na Ahmad, wanaikataa hiyo Mursal.

[7] Imefupishwa kwa ruhusa kutoka kwenye kitabu cha ad-Dahlawiy, HujjatuLlaah al Baalighah, (Egypt), I, uk. 205-308.

[8] Anachoeleza hapa mwandishi ni kwamba hizi njia zilizozuka ni zana za mtindo usiojulikana kwa Swahaabah, lakini bado zilitumika kwa mapana na kufungiwa kazi na Maimamu hawa wawili.

Share