Mazungumzo Ya Nabii Musa Na Al-Khidhwr Katika Suratul-Kahf

 

SWALI:

MIMI NINGEPENDA KUULIZA SUALA MOJA TU. KATIKA SURAT KAHF KUNA MASUALA AMBAYO NABII MUSSA ALIKUWA ANAULIZA NA AKIPEWA MAJIBU NA YULE ALIYEFATANA NAE. TAFADHALI NAOMBA UFAFANUZI WA MASUALA ALIYOKUWA AKIULIZWA. NA ALIYEMUULIZA NI NANI YULE?

WABILLAHI TAUFIK.

 


 

 

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola   wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo. Hakika masuala hayo yanapatikana katika Suratul Kahf (18) ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka tuwe tunaisoma kila Ijumaa ili tuepukane na fitina za Dajjaal. Masuala ambayo Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) aliyomuuliza Khidhwr ni kama yafuatayo: Kwa nini akalitoboa jahazi, kumuua kijana asiye na hatia na kuusimamisha ukuta. Majibu ya masuala haya matatu yalikuwa:

Ama ile jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu, kwani nyuma yao alikuwako mfalme anaghusubu majahazi yote. Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa ni Waumini. Tukahofu asije watia mashakani kwa uasi na ukafiri. Basi tulitaka Mola wao Awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma. Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako hazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Aitaka wafikie utu uzima na wajitolee hazina yao wenyewe, kuwa ni Rehma itokayo kwa Mola wako  . Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria” (Al-Kahf: 79 – 82).

Aliyekuwa akimuuliza Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) ambaye ni Khidhwr wanazuoni wametofautiana kuhusu yeye alikuwa nani. Wengine wamesema kuwa alikuwa ni mja mwema kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Mja katika waja Wangu Tuliyempa Rehma kutoka Kwetu” (Al-Kahf: 65).

Na wengine wakasema kuwa alikuwa Nabii kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria” (Al-Kahf: 82).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share