Mafunzo Kutoka Kisa Cha Nabii Ayyuub

 

SWALI:

Considering kisa of nabii zakaria (AS) and nabii Ibrahim (AS) who with ALLAHS grace has bestowed to them children at an old age and nabii Ayub (AS) got other children after a long illness. What are the lessons do we get from these kisaa of nabii AS with this respect.

Thanks, 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Mtume yeyote usiandike (AS) bali unadike kwa urefu (‘alayhis-salaam). Au pia unapondika Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mafunzo tunayopata katika kisa cha Nabii Ayyuub ('Alayhis Salaam). Hakika ni kuwa visa vyote vilivyotajwa na Allaah Aliyetukuka katika Qur-aan vina mazingatio kwa Ummah huu ikiwa ni visa vya watu wema na Manabii au watu wabaya. Visa vyote vinavyosimuliawa katika Qur-aan ni vizuri kama Anavyotueleza Aliyetukuka:

"Sisi Tunakusimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur-aan hii" (12: 3).

Ama kuhusu darsa na mafundisho tunayopata katika visa hivi Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Bila shaka katika hadithi zao hizi limo fundisho kwa wenye akili. Si maneno yaliyozuliwa, bali ni hakikisho ya yale yaliyokuwa kabla yake na ni maelezo pia ya kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini" (12: 111).

Ama tukiangazia mafunzo tunayopata katika kisa cha baba wa Mitume, Nabii Ibraahiym ('Alayhis Salaam) tunaona ya kwamba alijitolea mhanga kwa kiasi kikubwa mpaka Allaah Aliyetukuka Akamchagua kuwa Imaam kwa watu. Anasema Aliyetukuka:

"Hakika Ibraahiym alikuwa Imaam (mfano mzuri wa wema wa kuigwa), mnyenyekevu kwa Allaah, mtii kamili, wala hakuwa miongoni mwa washirikina" (16: 120).

Alipita mitihani mikubwa yote aliyopatiwa kama Alivyoeleza Allaah Aliyetukuka kama ilivyo katika Surah 2: 124. Kwa wepesi aliokuja nao katika Dini ndio Allaah Aliyetukuka Akatuamuru tufuate mila hiyo yake (22: 78).

Ama Nabii Zakariya ('Alayhis Salaam) alikuwa ni mnyenyekevu wa hali ya juu wala hakufa moyo akijua hakika kuwa Allaah Aliyetukuka yupo na Atamwitikia du’aa yake aliyoomba. Na tukisoma katika Surah Maryam mwanzoni tutapata hayo.

Ama tukija kwa Nabii Ayyuub ('Alayhis Salaam) naye pia tunapata mafunzo kemkemu kwani uvumilivu wake ni wa kuigwa na kupigiwa mfano kwa Ummah wote. Daraja yake kwa mpangilio tunapata katika Aayah ifuatayo:

"Tumekuletea wahyi kama Tulivyowapelekea Nuuh na Manabii wengine baada yake.  Na kama Tulivyompelekea Ibraahiym na Ismaa'iyl na Ishaaq na Ya'quub na kizazi chake. Na pia 'Iysaa na Ayyuub na Yuunus na Haaruun, Sulaymaan na Daawuud Tukampa Zaburi" (4: 163).

Kuhusu madhara aliyopata Nabii Ayyuub ('Alayhis Salaam) na kuyavumilia hadi kumuomba Allaah Aliyetukuka Amuondoshee, na Aliyetukuka Akawa ni mwenye kumuondeshea hilo. Anasema Aliyetukuka:

"Na Ayyuub, alipomwita Mola wake akasema: 'Mimi imenipata dhara, Nawe Ndiwe Unayerehemu kuliko wote wanaorehemu. Basi Tukamkubalia wito wake na Tukamuondolea dhara aliyokuwa nayo, na Tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao. Ni rehema inayotoka Kwetu, na ukumbusho mzuri kwa wafanyao Ibadah" (21: 83 – 84).

 

Na Allaah Aliyetukuka Anamtaja Nabii Ayyuub ('Alayhis Salaam) kuwa ni mja Wake pindi alipomrudia Yeye baada ya kupata madhara na udhia kutoka kwa shetani. Haya yaliyotokea kwa kurudishiwa watu wake ni mawaidha kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa wenye akili. Baada ya hapo tunaambiwa kuwa alikuwa mja mwenye kusubiri (38: 41 – 44). Kwa mwenye akili hakika atapata mawaidha makubwa sana katika maneno ya Allaah Aliyetukuka tuliyoyaeleza.

Kwa muhtasari tunapata fundisho katika maisha ya Nabii Ayyuub ('Alayhis Salaam) la kusubiri, unyenyekevu, kumuomba Allaah Aliyetukuka katika matatizo, kuendelea kufanya Ibaadah katika hali zote na shetani hawezi kumghuri mja mwema, na kadhalika.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share