Uteremsho Wa Qur-aan Kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

SWALI:

 

Asalaam alaykum

 

Nina suala-Tunaamini kuwa Quraan tukufu imeteremka katika mwezi huu mtufu wa ramadhan, suala langu ni ikiwa ni hivyo vipi yale matukio ambayo Quraan pia imeteremka maalum kwa ajili ya hayo kama vile suratul Mujadilah, pia kisa cha mama wa waislam bi'Aisha na Zainab binti Jahsh etc, ina maana matukio yote hayo yalitokea katika mwezi mtukufu?

Wabillah Tawfiq 

Kuna suala linanisumbua bado kidogo kuhusu uteremsho wa Quraan tukufu. Nimefahamu Alhamdulillah kuwa ilishikuka yote katika laylatul Qadr na pia ikashuka kidogo kidogo kwa muda wa miaka 23 kutokana na matukio mbali mbali, kwa mfano kisa cha bi Aisha (radhiyallahu'anha) alivyosingiziwa kuwa amezini na tunajua kabisa mtume (swalallahu alayhi wasallam) ilimsumbua sana akili yake mpaka akamwambia aende kwanza kwao akapumzike, huku mama yetu wa waislamu akiwa na huzuni kubwa kwamba hajafanya hayo. Suali ni, naamini itakuwa ilitokea kabla ya ramadhan chache ambazo zilishapita ila sina uhakiki ni wakati gani kilitokea hichi kisha na Allah (Subhanah wa ta’ala) ndiye mjuzi, mtume angekuwa amekwisha jua kua sio kweli hakufanya mama yetu kitendo hicho kwani Quraan ilishatemshwa kwake yote, na atakuwa alikuwa anajua matukio yote hayo, ilikuwaje asijue hayo na qura'an nzima alikuwa nayo? 

Wabillah Tawfiq,


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani kwa swali lako kuhusu uteremsho wa Qur-aan kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Kulingana na maelezo yako, unaelekea kuwa umehisi kuwa kuna utata na tatizo katika suala hilo, lakini kiuhakika hakuna tatizo lolote wala utata wowote juu ya suala hilokama utakavyosoma hapa chini. 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hajui hayo yote kwa kuwa Qur-aan haikuteremshwa kwake yote kwa wakati mmoja.

Qur-aan yote iliteremshwa kutoka Lawhul Mahfuudh (Ubao Uliohifadhiwa) ambao uko wingu wa saba na kuteremshwa katika wingu wa dunia (wa kwanza). Kutoka kwa wingu huo Qur-aan ikawa inateremshwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kidogo kidogo kulingana na matukio yalivyokuwa yakitokea na haja mbalimbali. 

Ndio ukaona alipokuwa Makkah Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa swali akasema nitawajibu kesho bila ya kusema InshaAllaah, wahyi ulizuiliwa kwa muda mrefu. Na ilipoteremshwa Suratul Kahf [18], akaagiziwa yeye na pia kuagiziwa sisi na Allaah Aliyetukuka tuwe ni wenye kusema InshaAllaah tutakapokuwa tunataka kufanya jambo la baadaye. 

Kwa muhtasari, Qur-aan yote iliteremshwa mpaka wingu wa kwanza. Na kutoka hapo ikashushwa kidogo kidogo kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa muda wa miaka 23.

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

Qur-aan Maana, Majina na Kuteremshwa Kwake -

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share