Mwanamume Niliyezini Naye Ananitangazia Nami Nimetubu Nifanyeje?

  SWALI:

naomba ushauri kuhusu matatizo ya liyo nikabili hapo awali .maana kila mja anaenifaham na asie nifaham ananiona mchafu.kwasa babu nilitembea na mume wa rafikiyangu ila nijambo ambalo owo nikitendo ambacho kilinihuzunisha sana na kujutia maisha yangu kwanza ninafaham ni dhambi ila sikuona hayo nilijitahidi kumuomba mwenzangu msamaha akanissamehe ila mumu wake ananichafuwa na kuzidi kunitia aibu hayoyote sababu nilimkatalia kwenda nae maranyingine ikaleta chuki.sasa nifanyeje iliniyaepuke hayo mwenyeezimungu anisaidie.naomba msada wenu maulam wabillahi taufiq.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunasikitika kusikia hali yako hiyo ya majuto kufanya maovu kisha mtu uliyefanya naye maovu anakupaka sifa mbovu. Hii ndivyo hali ya kawaida inavyokuwa kwa kila mwanamke anayezini kwani bila ya shaka mwenye kuzini naye atakudharau na ataendelea kukudharau hadi atakavyo mwenyewe na hakuna wa kumzuia. Hili ni zingatio kubwa lipasalo kuzingatiwa na kila mwanamke Muislamu.

Haya makosa hutokea sana kwa dada zetu kutokana na kudanganywa na wanaume ambao ni mahodari kabisa katika kazi hii ili tu apate maslahi yake kuzini na mwanamke kisha amtupilie mbali na kumkashifu. Na yote yanatokana kutokufuata amri za Mola wetu Mtukufu na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) zilizojaa katika Qur-aan na Sunnah:

Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 ((وَلاَ تَقْرَبُواْ الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاء سَبِيلاً))

((Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya)) [Al-Israa: 32]

Uchafu na njia mbaya ndiyo kama hayo yaliyokusudiwa kuwa baada ya kuzini hubakia mja katika hali ya uchafu hiyo na matokea maovu ni kama hayo yaliyokufika kuwa na doa la kuzini na kuharibu heshima na stara yako.

Shaytwaan pia naye yuko karibu kabisa na waja kuwaingiza katika maovu hayo, na hutafuta kila njia za kukukaribisha katika maovu hayo. Kama ilivyokuwa katika hali yako ulikuwa hupasi wewe kuishi na mume wa rafiki yako katika nyumba moja kwani hilo ni katazo katika dini yetu kuchanganyika wanawake na wanaume wasio maharimu wao. Mada ifuatayo ni muhimu kabisa isomwe na kila Muislamu mwanaume na mwanamke mwenye kutaka kufuata haki na mwenye kutaka kujiepusha na maovu kama hayo:

Ikhtilaatw (Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake)

Lakini kwa vile sisi ni binaadamu na kufanya makosa ni jambo la kawaida basi la muhimu ni kuwa pale mtu anapokosea inampasa   kurudi kwa Mola wake Ambaye Yuko tayari kabisa kupokea tawbah yake. Na hivyo ndivyo inavyoelekea kwako kutaka kurudi, hivyo nayo ni neema kutoka kwa Mola wako kuwa umewahi kutambua makosa na dhambi zako kabla ya kufikia wakati ambao tawbah hazipokelewi tena au kabla ya kuondoka duniani.

Sasa iliyobakia ni kufanya tawbah ya kweli na uzidishe mema mengi, khaswa uzidishe ibada kama kuswali na kufunga Sunnah kwani mema kufuta maovu kama Anavyosema Allaah (Subahaana wa Ta’ala):

((وَاَقِمِ الصَّلاَةَ طَرَفَیِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّیْلِ اِنَّ الْحَسَنَاتِ یُذْهِبْنَ السَّیِّئَاتِ ذَلِکَ ذِکْرَی لِلذَّاکِرين))

((Na simamisha Swalah katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka)) [Huud: 114]

Ingia katika kiungo kifuatacho usome mada muhimu zilizomo humu:

Tawbah

Yaliyopita yote maovu ya mja, husamehewa madhambi yake ila ajitahidi asirudie tena kwani kurudia tena itakuwa ni kupata ghadhabu za Mola kama Anavyosema:

((عَفَا اللّهُ عَمَّا سَلَف وَمَنْ عَادَ فَيَنتَقِمُ اللّهُ مِنْهُ وَاللّهُ عَزِيزٌ ذُو انْتِقَامٍ))

((Allaah Amekwishayafuta yaliyopita; lakini atakayefanya tena Allaah Atamuadhibu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu)) [Al-Maaidah: 95]

Ama kuhusu huyo mwanaume kukufedhehesha, hilo hakika ni jambo ovu kabisa alifanyalo kwani kakosa kutambua kuwa naye pia ameshiriki katika maasi hayo, hivyo naye pia yuko katika sifa ya uchafu huo. Ingawa kwa wanaume huwa mara nyingi aibu haionekani kubwa kwa jamii kama ilivyo aibu kwa mwanamke. Lakini hilo lisiwe jambo la kukuvunja sana moyo wewe ingawa ni zito. Linalokupasa kufanya ni kuvuta subira na kuzidi kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akusitiri, Akuhifadhie siri zako na Azidi kukuongoza.

Naye kupita kukuchafua pia kwa upande mwengine ni kheri yako kwani kila anapokutaja nyuma yako ambayo huwa ni kusengenya, basi anakubebea dhambi zako. Na kila anapoendelea huwa hivyo hivyo hatimaye itakuwa ni kupewa wewe thawabu zake hadi abakishwe hana amali njema bali madhambu matupu.

Nasaha yetu ya mwisho na ya dhati ni kuwa endelea kushika dini yako sawa sawa, kufuata amri za Mola wako, na kujieupusha kabisa na Shaytwaan asikutelezeshe tena ukapotea na zidisha sana ucha Mungu. Kufanya hivyo utabakia katika ridhaa ya Mola wako ambalo ndilo jambo muhimu kuliko yote mengine kama hayo mwanamume kukutangazia uovu, na pengine hatimaye uje kuwa ni mja mwema kabisa au kipenzi kikubwa cha Allaah Mola Mtukufu.

Na Allaah Anajua zaidi  

 

 

Share