Sababu ya Aya Kutaja Kwa Wingi Ni Kutukuka Kwa Allaah

 

SWALI

 

Assalam alaykum Mashehe wetu

 

Namshukuru Allaah kwa kila kitu, na pia natarajia kuwa mnaendelea kwa afya njema na uzima kamili pamoja na shughuli zote za dawa.

 

Nimefurahi kujibiwa lile suali langu la chakula cha halali. Pia leo nna masuali haya

 

1. Tunasoma katika Qur'an l karim, katika Aya kadhaa Allaah SWT kwa hekma yake anataja katika aya nyengine kwa uwingi, yaani anasema TUME na sio NIME. Tumeziumba mbingu na ardhi au kama hivyo kama sikosei. Sisi Waislam Alhamdulillah kwa mapenzi yake Allaah kutuchagua katika waja wake tunaoamini kuwa Allaah ni mmoja na hana mshirika, Jee suali langu pana hekma gani Allaah kusema TUME...?

 

Ahsanteni sana na Allaah akuwafikishieni kheri Duniani na Akhera AMIN


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kumpwekesha Allaah katika ‘Ibaadah, katika Ubwana wake na Ufalme na katika majina na sifa Zake ni msingi wa Uislamu. Na hivyo alipoulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na Mu‘adh bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu): Nipe khabari ya amali itakayonitia Peponi na kuniepusha na Moto”. Alisema: “Umeuliza jambo kubwa nalo ni sahali kwa aliyesahilishiwa na Allaah Aliyetukuka: Ni kumuabudu Allaah wala usimshirikishe na chochote …” (at-Tirmidhy na akasema ni Hadith Hasan Sahiih). Hii ambayo Allaah anatumia katika Qur’ani kwa njia ya wingi inatumika katika lugha nyingi na katika Kiarabu ni Jam‘u Lita‘dhiim (Majestic or Royal Plural au wingi wa ukubwa na utukufu au wingi wa kifalme). Oxford Advanced Learner’s Dictionary inafasiri We (Sisi) kwa kusema: “Formal used instead of I by a king, queen or pope or by the writer of an editorial article in a newspaper, etc. The ROYAL WE (Inatumika rasmi badala ya Mimi na mfalme, malkia, papa au na mwandishi wa tahariri katika makala ya gazeti na kadhalika. Hii ni Sisi ya kifalme” (uk. 1443). Na Allaah ni Mkuu zaidi na Mtukufu na kwake ipo mifano ya juu zaidi na ni aula katika kutumia utukufu wake katika hilo, hivyo ‘TUME’ au ‘SISI’ inapotumika katika Qur’an inaonyesha Utukufu wake akiwa Yeye ni Yeye tu wala hana mwendani.

 

 

Na Allaah Anajua Zaid

 

 

Share