Hekma Ya Kuteremshwa Qur-aan Kidogo Kidogo Na Kutokana Na Matukio

 SWALI:

 

Kuna mantiki gani kwa Quran kushushwa kidogo kidogo, na tena mpaka kitokezee kisa ndio aya za Qura zinashuka?

 JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Qur-aan ni kitabu cha mwisho kilichoteremshwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni uongofu kamili wa binaadamu wote na majini. Ni tofauti na vitabu vinginevyo ambavyo viliteremshwa kwa watu fulani au mataifa fulani kama mfano Tawraat imeteremshwa kwa Nabii Muusa na watu wake Bani Israaiyl na Injiyl kwa Nabii 'Iysa na wafuasi wake.

kama

 

Tofauti nyingine baina ya vitabu hivyo na Qur-aan ni kwamba hivyo vya kabla vimeteremshwa vitabu kwa mteremsho mmoja. Ama Qur-aan haikuteremshwa kitabu bali ni Wahy (ufunuo) katika moyo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na pia Wahy huo haukuteremshwa wote pamoja bali kidogo kidogo, na kila kunapotokea jambo fulani ndipo Aayah zilikuwa zikiteremshwa.  

kama
kama

 

Kuna Hikma nyingi kubwa katika aina ya uteremshwaji wa Qur-aan, tunazinukuu baadhi yake:

 

Kwanza:

 

Moja ya hikma ni kwamba kwa sababu ya kuwavutia watu kuingia katika dini kwa kufuata maamrisho yake na makatazo yake pole pole, na hii ni njia itumikayo na yenye matunda katika da'awah.  Kwani ingelikuwa ni kufuata makatazo yote na kufuata maamrisho yote kwa pamoja, basi ingelikuwa ni vigumu sana watu kufuata, na ndio maana kwa muda wa miaka kumi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa Makkah hakukuwa na zaidi ya kuwaita watu kuingia katika dini, neno la ‘Laa ilaah illa Allaah’, ndilo lililokuwa lengo, hakukuwa na amri za fardhi yoyote wala hukmu zozote.

 

Mfano, makatazo ya ulevi, kwa vile ulevi ulikuwa ni moja ya maasi makuu na hata baada ya kuja Uislamu, baadhi ya Maswahba walikuwa bado wakilewa. Hii ni kwa sababu ilikuwa ni ada na desturi zao walizozirithi katika ujaahiliyyah kama zilivyo desturi nyinginezo walizokuwanazo mfano kuwaua watoto wa kike, kuwanyima urithi wanawake n.k.. Ukaja Uislamu na kuondosha dhulma zote hizo.  Hivyo jambo kama ulevi lilihitajika hikma ya kuukataza kwa pole pole na ndio maana tunaona kwamba kuna Aayah tatu zinazohusiana na makatazo ya ulevi ikianza kwanza kwa kutaja madhara yake na manufaa yake, kisha pole pole hadi kukataza kabisa.

 

'Umar ibn Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alikuwa mmoja wa Maswahaba aliyekuwa akilewa, siku moja alisema: "Ewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)! Tupe hukmu kuhusu Al-Khamr (ulevi), hapo ikateremka Aayah:

 

((يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَآ أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا))

 

((Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake)) [Al-Baqarah: 219]

 

Wakaendelea kunywa ulevi hadi siku moja katika Swalah, Swahaba mmoja alikosea kusoma Suratul Kaafiruun ndipo ikateremshwa Aayah:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَقْرَبُواْ الصَّلاَةَ وَأَنتُمْ سُكَارَى حَتَّىَ تَعْلَمُواْ مَا تَقُولُونَ))

 

((Enyi mlioamini! Msikaribie Swalah, hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema)) [An-Nisaa: 43]

 

Wakaacha kulewa nyakati za Swalah na wakaendelea nyakati nyingine hadi kukatokea maovu mengine ndipo 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema tena: 'Ewe Allaah! Tupe Aayah iliyo wazi kabisa kuhusu Al-Khamr. Ndipo Aayah ya mwisho kuhusu makatazo ya ulevi ikateremshwa [Tafsiyr ibn Kathiyr]

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ))

 

((Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya shaytwaani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa)) [Al-Maaidah: 90]

 

Hikma ya pili:

Hikma nyingine ya kuteremshwa kidogo kidogo ni kwa sababu ya kuithibisha Qur-aan katika kifua cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani ingelikuwa vigumu kwake kuipokea yote mara moja. Hii ni kwa sababu Qur-aan ni maneno mazito ya Mola Mtukufu Anavyosema Allaah Mwenyewe:

kama

((إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا))

((Hakika Sisi tutakuteremshia kauli nzito)) [Al-Muzammil: 5]

Makafiri katika kejeli na ukaidi wao wa kukanusha Qur-aan walileta swali hili, "Kwa nini Qur-aan isiteremshwe mara moja?"   

))وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَة((

((Na wakasema waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur-aan kwa jumla moja?))   [Al-Furqaan:32]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Akawajibu kwa kuwapa Hikma Yake ya kuiteremsha kidogo kidogo kwa muda wa miaka ishirini na tatu kutokana na matukio na hali ilivyokuwa ikitokea,  kuwa ili Qur-aan ithibitike katika moyo wa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama Aayah ilivyomalizikia kusema.

))وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَة كَذَلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ وَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلًا ((

((Na wakasema waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur-aan kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili Tuuthibitishe moyo wako, na ndio Tumeisoma kwa mafungu ))  [Al-Furqaan: 32]

Vile vile Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)    

))وَقُرْآناً فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَى مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلاً((

((Na Qur-aan Tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na Tumeiteremsha kidogo kidogo)) [Al-Israa:106]

 

Hikma ya Tatu:

Hikma nyingine haikuwa tu kwa ajili ya kuithibitisha kwa ajili ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pekee bali kwa ajili ya Maswahaba ambao walikuwa wakipokea Aayah zinapotremeshwa, kuzisoma na kuzihifadhi na kuzifanyia kazi. Hawakuwa wakihifadhi Aayah  nyingine hadi wahakikishe wamezifahamu vizuri hizo chache, na kutekeleza maamrisho na makatazo yake.   

 

Hikma ya nne:

Kwa vile baadhi ya Aayah za Qur-aan zilikuwa zikiteremshwa kutokana na sababu ya matukio mbali mbali mfano; 'Kisa cha Watu watatu waliokhalifu katika vita vya Taabuuk', 'Kisa cha Ifk (kusingiziwa Mama Wa Waumini)' n.k. hivyo kulihitaji kuweko na hukmu zake, ndio maana Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

  ((وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَى لِلْمُسْلِمِينَ))

((Na Tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uongofu, na Rehma na bishara kwa Waislamu)) [An-Nahl: 89]

Matukio mengine yalimhitaji Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asubiri wahy kutoka kwa Allaah, mfano mmoja mzuri kabisa ni kisa cha Bibi Khawlah bint Khuwaylid aliposhindwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumpa hukmu ya mumewe inavyoelezewa katika Aayah zifuatazo:

kama

  بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ  

((قَدْ سَمِعَ اللَّهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّهِ وَاللَّهُ يَسْمَعُ تَحَاوُرَكُمَا إِنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ بَصِير))

 ((الَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِنكُم مِّن نِّسَائِهِم مَّا هُنَّ أُمَّهَاتِهِمْ إِنْ أُمَّهَاتُهُمْ إِلَّا اللَّائِي وَلَدْنَهُمْ وَإِنَّهُمْ لَيَقُولُونَ مُنكَرًا مِّنَ الْقَوْلِ وَزُورًا وَإِنَّ اللَّهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ))

 (( وَالَّذِينَ يُظَاهِرُونَ مِن نِّسَائِهِمْ ثُمَّ يَعُودُونَ لِمَا قَالُوا فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مِّن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا ذَلِكُمْ تُوعَظُونَ بِهِ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِير))

 ((فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ مِن قَبْلِ أَن يَتَمَاسَّا فَمَن لَّمْ يَسْتَطِعْ فَإِطْعَامُ سِتِّينَ مِسْكِينًا ذَلِكَ لِتُؤْمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيم))

 

KWA JINA LA ALLAAH MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

((Allaah Amekwishasikia usemi wa mwanamke anayejadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Allaah, Na Allaah Anayasikia majibizano yenu. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona))

((Wale miongoni mwenu wanaowatenga wake zao, hao si mama zao. Hawakuwa mama zao ila wale waliowazaa. Na hakika hao wanasema neno linalo husha, na la uongo. Na Allaah ni Mwenye kughufuria, Mwenye kusamehe))  

((Na wale wanaojitenga na wake zao, kisha wakarudia katika yale waliyoyasema, basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa maonyo kwa hayo. Na Allaah anayajua yote mnayo yatenda))

((Na asiyepata mtumwa kumkomboa, basi na afunge miezi miwili mfululizo kabla hawajagusana. Na asiyeweza hayo basi awalishe masikini sitini. Hayo ni hivyo ili mumuamini Allaah na Mtume wake. Na hiyo ndiyo mipaka ya Allaah. Na kwa makafiri iko adhabu iumizayo)) [Al-Mujaadalah: 1- 4].  

 

Tukio kama hili na mengineyo, ni hikma ya kuteremshwa Qur-aan kidogo kidogo pamoja na hukumu yake ili watu wafahamu pia hizo hukmu zake pole pole. Kadhaalika matukio mengineo ambayo pia yametokea kisha zikateremshwa Aayah pamoja na hukmu zake na ndipo ikawa wepesi Maswahaba kuisoma, kuihifadhi na kuifanyia kazi maamrisho na makatazo yake yote.

Tunatumai kwa hayo yataleta fahamu nzuri kuhusiana na Swali la muulizaji.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share