Kulala Kifudifudi Inafaa Ikiwa Ana Matatizo Ya Afya?

 

SWALI:

Nilisoma kwenye vitabu kuwa Mwenyeezi Mungu hampendi mtu anaye lala kitumbo, yaani kulalia tumbo lake. Nakua watu wa motoni ndio watakuwa wakilalia matumbo yao. Swali langu ni hili:

Mimi nilipata matatizo katika mazazi ya mwanangu, wakati wa kulala mara nyingi huwa tumbo linaniuma, najaribu kulala vile Mtume SAW alivyotuambia, yaani kwanza ubavu wa kulia kisha kushota n.k, lakini sipati usingizi mpaka nililalie tumbo ndio nitapata nafuu. Je nifanye nini ili nisilalie tumbo ama kuna hukmu gani katika hili jambo?

Naomba pia muniombe Mwenyeezi Mungu anipe Afya na aniepushiye haya maradhi. Amin

 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako ewe dada yetu. Hakika ni kuwa kulala kwa namna aliyotufundisha Mtume wa Allaah ni njia iliyo bora kiafya kwani madaktari wamegundua faida zake. Kulala kitumbo hakika kunaleta madhara kwani mara nyingine unaweza kuzuiia pumzi zako au kupumua kwa shida.

Uislamu ni Dini ya kimaumbile na inatazama sababu za kila mmoja wetu na haimkalifishi yeyote juu ya uwezo wake. Ukiwa unapata shida hiyo uliyosema basi unaweza kulala kwa njia nyingine lakini jaribu kulala kwa njia ya Sunnah na Allaah Aliyetukuka Atakusaidia. Allaah Aliyetukuka Anatueleza:

Na wale wanaoamini na wakatenda mema - hatumkalifishi mtu yeyote ila kwa kiasi cha uwezo wake - hao ndio watu wa Peponi” (7: 42

 

Tunavyotakiwa ni kujaribu tuwezavyo kutekeleza Sunnah ili tupate faida na fadhila zake, lakini mtu anashindwa basi nia yake inatosha kupata hata hizo fadhila na faida Insha Allaah.  

 

Pia soma makala hii ili uweze kujua faida za kulala kwa ubavu wa kulia kama alivyofundisha kipenzi chetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Nini Hikma Ya Kulala Upande Wa Kulia Kama Alivyotufundisha Mtume

Tunakuombea shifaa na maradhi yako na ponyo na haraka inshaAllaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share