Utapokea Kitabu Chako Siku Ya Qiyaamah Kwa Mkono Gani?

Utapokea Kitabu Chako Siku Ya Qiyaamah Kwa Mkono Gani?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا ۚ وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا ﴿٤٩﴾

Na kitawekwa Kitabu, basi utaona wakhalifu ni wenye khofu kwa yale yaliyokuwemo ndani yake; na watasema: Ole wetu! Kitabu hiki kina nini, hakiachi dogo wala kubwa isipokuwa kimerekodi hesabuni. Na watakuta yale waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Rabb wako Hamdhulumu yeyote. [ Al-Kahf: 49]

 

Aayah hii inatupa picha ya hali itakavyokuwa Siku ya Qiyaamah kwamba matendo yetu yote tutayaona yamerekodiwa katika kitabu. Siku hiyo, ni Siku isiyo na shaka, Siku ya miadi, Siku ya inayosubiriwa, Siku ya majuto, Siku ya nyoyo kushituka na macho kukodoka, Siku ya mashaka, Siku ambayo hakuna budi kwa kila mmoja kuifikia! 

 

Ndugu Waislamu, hii ni Siku ya kulipwa mema au mabaya, Siku watakayosimama watu wote na majini mbele ya Rabb wa Ulimwengu, siku ambayo kafiri atasema:

 

  يَا لَيْتَنِي كُنتُ تُرَابًا

“Laiti ningelikuwa mchanga.” [An-Nabaa: 40]

 

Je, Umefikiria na kuwaza hali yako itakavyokuwa Siku hiyo utakaposimama mbele ya Rabb wako Mtukufu na huku unasubiri hesabu upewe kitabu chako?

 

Mwana Aadam anapoingia kufanya mtihani au anapokwenda mahakamani kuhukumiwa, moyo wake unajazwa na khofu au kiwewe kwa wazo la kutaka kujua atafanyaje au kuwaza yatakayomkabili.  Je, basi itakuwaje hali ya moyo siku hiyo wakati matokeo yake yatakuwa ni aidha kuingizwa Jannah adumu milele humo kwa amani na furaha na kila aina ya starehe na neema. Au aingizwe motoni ambako kuna kila aina adhabu khasa kwa yule ambaye ameishi umri wake wote katika maasi au ambaye ameshughulishwa  katika starehe za dunia bila kuchuma mema yoyote!    

 

Amiyrul-Muuminiyn amesema manenno ya busara kabisa:

 

"حاسبوا أنفسكم قبل أن تحاسبوا، وزنوها قبل أن توزنوا، فإن أهون عليكم في الحساب غدًا أن تحاسبوا أنفسكم اليوم، وتزينوا للعرض الأكبر، يَوْمَئِذٍ تُعْرَضُونَ لَا تَخْفَىٰ مِنكُمْ خَافِيَةٌ﴿١٨﴾

 

"Hesabuni nafsi zenu kabla ya kuhesabiwa, na zipimeni kabla ya kupimwa, kwani ni bora (wepesi) kwenu kupima (amali zenu) leo kabla ya (kupimwa) kesho kwenye Hesabu, na jipambieni kwa mhudhurisho mkubwa wa:  “Siku hiyo mtahudhurishwa, hakitafichikia kwenu kinachofichwa.” [Al-Haaqah: 18]

 

Jipime ndugu Muislamu na jiulize: Je, utakuwa miongoni mwa watakaopewa vitabu vyao mkono wa kulia kisha  ukakichukua kwa furaha kubwa na kukionyesha kwa wenzako kama vile mfano duniani unapopata shahada yako uliyofuzu vizuri sana ukatamani kila mmoja aione, ukaidhihirisha na kuwaambia wenzako kwa furaha: “Nnimefuzu! Nimefuzu!”

 

Hali hiyo ni kama hali itakavyokuwa Siku ya Qiyaamah pindi ukijaaliwa kuwa miongoni mwa wale watakaopokea Vitabu vyao upande wa kulia kama ilivyo Kauli ya Allaah Subhaanahu wa

Ta 'aalaa: 

 

 

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَءُوا كِتَابِيَهْ﴿١٩﴾ إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ﴿٢٠﴾ فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ﴿٢١﴾ فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ﴿٢٢﴾ قُطُوفُهَا دَانِيَةٌ﴿٢٣﴾ كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا أَسْلَفْتُمْ فِي الْأَيَّامِ الْخَالِيَةِ﴿٢٤﴾

“Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kuliani mwake; atasema: Hebu chukueni someni kitabu changu! Hakika mimi niliyakinisha kuwa hakiki mimi ni mwenye kukutana na hesabu yangu! Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhisha. Kwenye Jannah ya juu. Matunda yake ya kuchumwa ni karibu.  Wataambiwa): Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyoyatanguliza katika siku nyingi zilopita”. [Al-Haaqah: 19-24]

 

Na jiulize pia, je, utakuwa miongoni mwa wale watakaopewa kitabu chao mkono wa kushoto ukawa na majuto makubwa ambayo hutoweza tena kuyarekebisha? Na hali hii pia ni kama hali itakavyokuwa Siku ya Qiyaamah pindi utakapokuwa miongoni mwa wale watakaopokea kitabu chao upande wa kushoto kama ilivyo Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ﴿٢٥﴾ وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيهْ﴿٢٦﴾ 

“Na ama yule atakayepewa kitabu chake kushotoni mwake; atasema: Ee! Laiti nisingelipewa kitabu changu! Na wala nisingelijua hesabu yangu!”

 

Majuto yatazidi kuwa makubwa hadi kwamba mtu atatamani mauti!  Kauli ya Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ﴿٢٧﴾ مَا أَغْنَىٰ عَنِّي مَالِيَهْ ﴿٢٨﴾ هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيَهْ﴿٢٩﴾

 “Ee! Laiti yangelikuwa (mauti) ndio kumalizika kwangu. Haikunifaa mali yangu. Madaraka yangu yamenitoweka.”

 

Wataamrishwa Malaika wamchukue mtu muovu huyo wamtupilie mbali motoni! 

 

 خُذُوهُ فَغُلُّوه﴿٣٠﴾ ثُمَّ الْجَحِيمَ صَلُّوهُ﴿٣١﴾ ثُمَّ فِي سِلْسِلَةٍ ذَرْعُهَا سَبْعُونَ ذِرَاعًا فَاسْلُكُوهُ﴿٣٢﴾

 “(Ataambiwa): Mchukueni, na mfungeni pingu! Kisha kwenye moto uwakao vikali mno muingizeni aungue. Kisha katika minyororo yenye urefu wa dhiraa sabini mtieni pingu.”

 

Sababu ni kwa kuwa:

 

﴿٣٣﴾ إِنَّهُ كَانَ لَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ الْعَظِيم

“Hakika yeye huyo alikuwa hamuamini Allaah Adhimu, Mkuu kabisa”

 

Na pia:

﴿٣٤﴾  وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ

“Na wala hahamasishi kulisha masikini.”

 

Ikiwa mtu alishughulishwa duniani kuwa mbali na kumdhukuru Allaah (‘Azza wa Jalla) na kutenda mema, ikiwa  ndugu au jamaa au Rafiki ndio waliomshughulisha, basi Siku hiyo hakuna hata mmoja atakeyemfaa mwenziwe kwani kila mmoja atakuwa analo lake la kukhofia. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

فَلَيْسَ لَهُ الْيَوْمَ هَاهُنَا حَمِيمٌ﴿٣٥﴾

“Basi leo hapa hatokuwa na Rafiki wa dhati.”

 

Chakula cha humo motoni ni usaha unaotoka katika miili ya watu na mti wa Zakkuwm ulio mchungu ajabu, na ambao una miba na unaokirihisha kabisa!

 

﴿٣٦﴾ لَّا يَأْكُلُهُ إِلَّا الْخَاطِئُونَ﴿٣٧﴾ وَلَا طَعَامٌ إِلَّا مِنْ غِسْلِينٍ

 “Na wala chakula isipokuwa maji ya vidonda vilooshwa (vya walio motoni). Hawakili chakula hicho isipokuwa wenye hatia.” [Al-Haaqah: 25-37]

 

Nani atakayeridhika kuwa katika hali hiyo? Kwanini basi mtu aache kutekeleza amri za Allaah (‘Azza wa Jalla) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na akatenda mema kwa wingi ili iwe akiba zake huko Aakhirah? Kwanini mtu apoteze  wakati wake kwa mambo ya upuuzi? Au kumuasi Rabb wake Aliyemuumba ilhali siku ya Qiyaamah mtu atasimama mbele Yake kujibu kila baya alilolitenda?

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Hadiyth Al-Qudsiyy:

 

((ياعبادي إنما هي أعمالكم  أحصيها لكم فمن وجد خيراً فليحمد الله ومن وجد غير ذلك فلا يلومن إلا نفسه)) مسلم

 ((Enyi waja Wangu, ni vitendo vyenu Ninavyovihesabu, kwa ajili yenu Nikakulipeni.  Kwa hivyo anayekuta wema amshukuru Allaah na yule anayekuta yasiokuwa mema (basi) ajilaumu mwenyewe)) [Muslim].

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atujaalie miongoni mwa watakaopokea vitabu vyao kuliani kama Anavyosema katika Suwrah nyengineyo:

 

 فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ ﴿٧﴾ فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا ﴿٨﴾ وَيَنقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًا﴿٩﴾

“Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kwa mkoni wake wa kulia. Atapewa hesabu nyepesi. Na atageuka kwa ahli zake mwenye kufurahi.” [Al-Inshiqaaq: 7-9]

 

Na Asitujaalie tukawa miongoni mwa wale watakaopewa vitabu vyao katika mkono wa kushoto au nyuma ya migongo yao kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاءَ ظَهْرِهِ ﴿١٠﴾ فَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًا ﴿١١﴾ وَيَصْلَىٰ سَعِيرًا﴿١٢﴾

“Na ama yule atakayepewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake. Ataomba kuteketea. Na ataingia aungue moto uliowashwa vikali mno.”  [Al-Inshiqaaq: 10-12]

 

*******

 

 

 

Share