Skip navigation.
Home kabah

Hadi Lini Utakuwa Mwenye Kughafilika?

7 Dhul-Qa'adah 08-12-2005

 

}}وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالإِنسِ لَهُمْ قُلُوبٌ لاَّ يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لاَّ يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لاَّ يَسْمَعُونَ بِهَا أُوْلَئِكَ كَالأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ أُوْلَئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ{{  

{{Na Tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walioghafilika}}  Al-A'araaf: 179

Ni ahadi ya kutisha kwa walioghafilika na Mwenyeezi Mungu.  Wale ambao wamepambika katika matamanio na starehe za dunia na ambao wameathirika nayo na wakaiuza akhera yao kwa dunia. Watu wasiomkumbuka Mola wao ila kidogo tu. 

Allaah سبحانه وتعالى Ametaja hapa, kuwa Jahannam itajaa watu na majini ambao amewafananisha kama wanyama, bali Amewaona kuwa wao ni wapotofu zaidi kuliko wanyama kwani wanyama angalau wanajua yepi ya manufaa na huyatafuta na yepi ya kuwadhuru na hujiepusha nayo.

Basi ewe ndugu Muislamu unayelala na Swalah za fardhi zikakupita au ukazichelewesha bila ya sababu, mpaka lini utakuwa katika kughafilika?  Haukushituka moyo wako kwa kitisho kama hiki cha Mola wako? Haushituki kusikia maneno ya Allaah سبحانه وتعالى  

((فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ))

(( الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ))

((Basi, ole wao wanaoswali) 

 ((Ambao wanapuuza Swalah zao))

Al-Maa'uun :4-5

Ewe Muislamu uliyeuweka moyo wako ukawa mbali na dhikr (ukumbusho wa Allaah سبحانه وتعالى) na ukaihama Qur'aan, mpaka lini utakuwa katika usingizi wa kughafilika?

Na ewe Muislamu uliyetega sikio lako kwa kusikiliza nyimbo na maneno ya umbea, mpaka lini utakuwa katika kughafilika? 

Na ewe Muislamu unayetazama mambo yaliyoharamishwa mpaka lini utakuwa katika kughafilika?

Na mwisho, ewe Muislamu unayeyasoma haya na ukatambua mabaya yako na tukatambua sisi mabaya yetu, tujiulize sote  mpaka lini tutakuwa katika kughafilika? 

Basi na tuamke na kujikurubisha kwa Mwenyeezi Mungu ili kuepukana na maradhi haya ya kughafilika kabla haijafika siku ya majuto, siku ambayo kila mtu atatamani irudi nyuma ili apate kujirekebisha lakini haitowezekana! 

 

************