Fadhila Za Surat Yaasiyn Na Al-An'aam
SWALI:
Naomba kupewa faida za SURA YASIN na ANAAM, kwani nimeambiwa usome ukiwa na shida au dhiki,ama nitokio
gani lilitokea kuteremshwa sura hizi? Shukran,ALLAHU BARIK,isnhl.
JIBU:
Bismillah, Waswalaatu Wassalaamu 'alaa RasuuliLLaah, waba'ad
Fadhila za Surat Yaasiyn
Tunakushukuru kwa kuuliza swali hili muhimu ambalo litatufanya tuweke wazi zile hadiyth zinazotumika ambazo zimeenea sana kuonyesha fadhila na utukufu wa surah hii. Tunaona katika jamii zetu jinsi watu wanavyotumia na kuitukuza surah hii pekee kuliko surah zingine katika Qur'an, vilevile pahala inapotumika ambapo si sahihi, kama vile mtu akiwa anakufa au hata baada ya kufa kwake tunaona wengi wakiisoma makaburini n.k.
Inatupasa tujue kwamba Mtume صلىالله عليه وآله وسلم ametuonya kuhusu kumsingizia maneno ambayo hajayasema na pia hatari ya kufanya hivyo. Tutazame hadiyth ifuatayo:
((عن أبي هريرة قال :قال رسول الله صلى الله عليه وسلم من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) مسلم و أحمد , وإبن ماجة
((Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Mwenye kunizushia uongo kwa makusudi, basi aandae makazi yake motoni )) Muslim, Ahmad na Ibn Maajah
Hapa chini tutabainisha hadiyth mbalimbali zisizo sahihi zinazozungumzia fadhila za surat Yaasiyn kama zilizobainishwa na Maulamaa wa Hadiyth:
(( )عن أبي هريرة رضي الله عنه) إن الله تبارك وتعالى قرأ طه و يّس قبل أن يخلق آدم بألفي عام ، فلما سمعت الملائكة القرآن قالوا طوبى لأمة ينزل هذا عليهم ، وطوبى لألسن تتكلم بهذا ، وطوبى لأجوف تحمل هذا )) ابن القيسراني سلسلة الأحاديث الضعيفة / 1248
(({Kutoka kwa Abi Hurayra رضي الله عنه } Allaah سبحانه وتعالى amesoma Sura Twaaha na Yasiin kabla ya kumuumba Adam miaka elfu, na waliposikia malaika Qur'aan wakasema "pongezi kwa umma inayowashukia (surah) hii, pongezi kwa ulimi utakaoizungumza surah hii, pongezi kwa tumbo (mwili) utakaobeba (surah) hii ) Imesimuliwa na Ibn Al-Qiysaraaniy
Imechambuliwa kuwa ni dhaifu kutoka katika kitabu cha 'Silsilatul Ahaadiyth Dhwa'iyfah' /1248
)) (عن أنس بن مال رضي الله عنه ) من دخل المقابر فقرأ سورة يّس خفف عنهم يومئذ ، وكان له بعدد من فيها حسنات )) السخاوي (( موضوع )) / سلسلة الأحاديث الضعيفة / 1246 ..
(( (Kutoka kwa Anas Bin Malik رضي الله عنه ) Atakayeingia makaburini na akasoma Surat Yasiyn atawafanyia wepesi (maiti) siku ya masiku, na ataandikiwa mema idadi ya walio humo makubirini)) Imesimuliwa na As-Sakhaawiy
Imechambuliwa kuwa dhaifu kutoka katika kitabu cha 'Silsilatul Ahaadiyth Dhwa'iyfah' /1246
(( (عن أنس بن مالك رضي الله عنه ) إن لكل شيء قلبا ، وقلب القرآن يس ، ومن قرأ يس ؛ كتب الله له بقراءتها قراءة القرآن عشر مرات)) الذهبي (( موضوع )) / ضعيف الترغيب و الترهيب / 885 ..
(( {kutoka kwa Anas Bin Malik رضي الله عنه} Kila kitu kina moyo, na moyo wa Qur'aan ni Surat Yasiyn, atakayesoma Yasiyn ataandikiwa thawabu za kusoma Quraan yote mara kumi )) Imesimuliwa na Adh-Dhahabiy
Imechambuliwa kuwa ni Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'At Targhiyb wat-Tarhiiyb' /885
)) من قرأ يس ابتغاء وجه الله ، غفر الله له ما تقدم من ذنبه ، فاقرؤوها عند موتاكم )) ضعيف الجامع الصغير/ 5785
((Atakayesoma Yasiyn kwa kutaka Ridhaa ya Allaah ataghufuriwa madhambi yaliyomtangulia, basi isomeni kwa maiti wenu ))
Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'Aj Jami'i Asw Swaghyr'/5785
)) من قرأ يس في صدر النهار قضيت حوائجه)) ضعيف مشكاة المصابيح / 2118
((Atakayesoma Yasiyn katikati ya mchana atakidhiwa haja yake)) Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'Mishkaat Al-Maswaabiyh'/2118
Naye Imam Daaraqutniy kasema hakuna katika fadhila za
Surah Yaasin hadithi yeyote iliyosihi
Kutokana na uchambuzi wa hadithi hizo dhaifu, inatupasa tuepukane na makosa yanayotendeka kama vile kusoma Yasiyn anapotaka kukata roho au baada ya kufariki mtu, au kuisoma zaidi ya mara moja kwa nia ya kukidhiwa haja, au utakuta mtu anaishikia kuisoma sura hii peke yake kila siku na kuziacha surah nyingine kwa kuamini kuwa ni kama kinga, wakati Qur'aan yote nzima ni kinga na ni wajibu wetu kuisoma yote na sio kuchagua sura fulani fulani tu kila mara.
Fadhila za Suratul-An-aam
((عن ابن عمر قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم" نزلت علي سورة الأنعام جملة واحدة وشيعها سبعون ألفا من الملائكة لهم زجل بالتسبيح والتحميد )) رواه الطبراني في " الأوسط
(( Kutoka kwa Ibn 'Umar ambaye amesema: Kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم imeteremka sura ya Al-An'aam kwa mteremko mmoja na imefuatana na malaika elfu sabiini wakimtukuza Allaah سبحانه وتعالى kwa kumsabihi na kumhamidi kwa sauti za juu )) At-Twabraaniy
Sura hii pia hakuna zaidi ya fadhila iliyotajwa isipokuwa hadithi hiyo ambayo haikuleta maana kuwa isomwe ukiwa na dhiki na shida.
Unapofikwa na shida na dhiki ni bora kabisa kuamka usiku kuswali Swalah ya Tahajjud katika thuluthi ya mwisho ya usiku wakati Allaah سبحانه وتعالى anataremka katika mbingu ya kwanza kutusikiliza shida zetu na kututakabalia kama ilivyothibiti katika hadithi ifuatayo:
((عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له ))
((Imetoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وسلم amesema: Allaah سبحانه وتعالى Huteremka kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba nimtakabalie? Nani ana shida nimtekelezee? Nani ananiomba maghfira nimghufurie?))
Vile vile zifuatazo ni dua za kukuondoshea shida na dhiki kama zilivyothibiti katika Sunnah:
Dua ukiwa na hamu na huzuni
اللّهُـمَّ إِنِّي عَبْـدُكَ ابْنُ عَبْـدِكَ ابْنُ أَمَتِـكَ نَاصِيَتِي بِيَـدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤكَ أَسْأَلُـكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ سَمَّـيْتَ بِهِ نَفْسَكَ أِوْ أَنْزَلْتَـهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ عَلَّمْـتَهُ أَحَداً مِنْ خَلْقِـكَ أَوِ اسْتَـأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الغَيْـبِ عِنْـدَكَ أَنْ تَجْـعَلَ القُرْآنَ رَبِيـعَ قَلْبِـي، وَنورَ صَـدْرِي وجَلَاءَ حُـزْنِي وذَهَابَ هَمِّـي
“Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi ni mtumwa wako, mtoto wa mtumwa wako, mtoto wa kijakazi chako, utosi wangu uko mikononi mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu yako, ni usawa kwangu kunihukumu kwako, nakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako ulilojiita kwako mwenyewe au Uliloliteremsha katika kitabu chako, au Ulilomfundisha yoyote yule kati ya viumbe vyako, au Ulilolihifadhi Wewe mwenyewe (na kujihusisha kulijuwa) katika ilimu iliyofichika kwako, nakuomba ujaalie (uifanye) Qur’an kuwa ni raha na uchanuzi wa roho yangu na nuru ya kifua changu, na utatuzi wa huzuni yangu, na sababu ya kuondoka majonzi yangu”
Du'a hiyo hapo juu na zifuatazo hapa chini, utazipata kwenye kitabu cha 'Hisnul Muslim' kilichopo ndani ya tovuti hii.
اللّهُـمَّ إِنِّي أَعْوذُ بِكَ مِنَ الهَـمِّ وَ الْحُـزْنِ، والعًجْـزِ والكَسَلِ والبُخْـلِ والجُـبْنِ، وضَلْـعِ الـدَّيْنِ وغَلَبَـةِ الرِّجال.
“Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi najilinda kwako kutokana na hamu na huzuni na kutoweza kwa uvivu na ubakhili na uoga na uzito wa deni na kushindwa na watu”
Dua ya kupatwa na janga au balaa
لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ الْعَظـيمُ الْحَلِـيمْ، لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ رَبُّ العَـرْشِ العَظِيـمِ، لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ رَبُّ السَّمَـوّاتِ ورّبُّ الأَرْضِ ورَبُّ العَرْشِ الكَـريم
“Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu aliye Mtukufu Mpole, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu Mola wa 'Arshi tukufu, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu Mola wa mbingu na Mola wa ardhi na Mola wa 'Arshi tukufu" .
اللّهُـمَّ رَحْمَتَـكَ أَرْجـوفَلا تَكِلـني إِلى نَفْـسي طَـرْفَةَ عَـيْن، وَأَصْلِـحْ لي شَأْنـي كُلَّـه لَا إِلَهَ إِلَّا أنْـت
“Ewe Mwenyezi Mungu rehema zako nataraji, usinitegemeze kwenye nafsi yangu japo kwa muda wa kupepesa jicho, na unitengenezee mambo yangu yote, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe”
Hii ni dua iliyomtoa Nabii Yunus katika tumbo la samaki wakati alipodhikika humo
لاَ إِلَهَ إِلَّا أنْـت سُـبْحانَكَ إِنِّي كُنْـتُ مِنَ الظّـالِميـن
“Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, kutakasika ni Kwako. Hakika mimi ni miongoni mwa waliodhumu nafsi zao”
اللهُ اللهُ رَبِّي لا أُشْـرِكُ بِهِ شَيْـئاً
“Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu , Mola wangu simshirikishi na kitu chochote kile"
Hizi ndizo du'a zilizothibiti na zisizo na mashaka, ama hizo ulizouliza kuhusu surah hizo, ni bora kuziepuka kwani hazina usahihi na ni kujiweka katika utata. Dini yetu haimtaki mtu kuifuata kwa kubahatisha na kwa mambo ya utata. ((Mtume anasema: "Acha lenye shaka, na fuata lisilo na shaka")) At Tirmidhy
wa Allaahu A'alam
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


