Ufafanuzi Wa Aayah Kuhusu Kupandishwa Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam) Mbinguni

 

SWALI:

 

Assalaamu Alaykum Warahmatullah.

 

Nashukuru kwa majibu yenu mazuri. Mungu awabariki kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kutuelimisha, Ahsanteni sana. Kuna Aya katika Qur-ani inaelezea kurufaishwa kwa Nabii Issa (kupandishwa mbinguni) lakini kuna nyengine inaelezea kuwa, Nabii Issa anamjibu Allah kuwa na uliponifisha wewe ulikuwa shahidi juu yao. Suala langu ni kuwa, nahisi Aya hizi zinapingana au sijazielewa

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ufafanuzi wa Aayah hizo mbili ulizozifupisha ambazo zinaonekana kuwa ni kinzani ilhali hazipingani kabisa.

 

Allaah Aliyetukuka Anatueleza:

 

Bali Allaah Alimnyanyua Kwake, na Allaah ni Mwenye nguvu na Mwenye hekima” (an-Nisaa’ [4]: 158).

 

Hii Aayah inatuonyesha kuwa vile vitimbi vya Mayahudi vya kutaka kumsulubu Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) havikufaulu kwani Allaah Aliyetukuka Alimrufaisha Kwake kwa wakati walipotaka kumshika. Hiyo inaonyosha nguvu Zake Aliyetukuka kufanya Analotaka, bila ya kuwa na wasiwasi wa aina yoyote.

 

Ama tukija katika Aayah ya pili uliyoitaja:

 

Na nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao; na uliponikamilisha muda wangu, Wewe ukawa mchungaji juu yao, na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu” (al-Maa’idah [5]: 117).

 

Tatizo kwa wengi kuhusu Aayah hii ya pili ni lile neno: “Tawaffaytaniy”. Neno hilo limetafsiriwa na Maqadiyani kumaanisha “uliponifisha”, ilhali Shaykh Abdallah Swaalih al-Farsiy amesema: “Wanavyuoni wanasema kwa tamko la Tawaffaa sio maana yake ya asili ‘kutoa roho’; na wao wanajua, basi tu. Na mwenye Ruuhul Ma’aaniy ambaye wanajidai wamemfuata; ameandika: ‘Uliponichukua kwa kunipeleka mbinguni’. Na akaendelea kusema kuwa neno hilo katika lugha ya Kiarabu ya asili ni kutekeleza” (Qurani Takatifu, uk. 169).

 

Na ukitazama Tafsiyr ya Fat-hul Qadiyr ya Imaam Ash-Shawkaaniy ameeleza: “Hiyo ina maana uliponinyanyua mbinguni, na hapa al-Wafaat haina maana ya mauti. Bali ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) alibaki mbinguni katika hali ya uhai kama alivyokuwa duniani mpaka arudi tena ardhini mwisho wa wakati kabla ya Qiyaamah. Uliponinyanyua mbinguni”.

 

Kwa hiyo, ufafanuzi huo utakuwa wazi inshaAllaah kuweza kuelewa Aayah hizo mbili.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo kupata manufaa zaidi:

 

Nini Ukweli Kuhusu Kupandishwa Nabii 'Iysa عليه السلام

 

Nani Aliyesulubiwa Badala ya Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam)?

 

Je, Nabii 'Iysa Alisulubiwa?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share