Baba Amefariki Ameacha Mjane, Ndugu, Watoto Na Anamiliki Nyumba

 

SWALI:

 

Asalaam aleykum, mzee amefariki kaacha nyumba 1, ndugu wa kike 2, wa kiume 1, watoto wa kike 2 na mjane 1, nyumba itagawanywaje?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mirathi. Awali ya yote ni kuwa lazima mwanzo ikiwa mzee ana madeni basi alipiwe na ikiwa aliacha wasiya basi pia utekelezwe lakini kiwango cha kutolewa kisizidi thuluthi (1/3).

 

Kwa hakika, inakuwa shida kuigawa nyumba kwa warithi hivyo wanaweza kuitia thamani hiyo nyumba kisha wakagawa kulingana na kiwango cha kila mmoja. Ikiwa si hivyo basi inatakiwa igawanywe vyumba na jambo hilo linakuwa ni vigumu ila tu iwe na vyumba vingi ambapo kila mmoja atapata sehemu yake. Kwa kuwa warithi ni wengi kiasi mara nyingi hutokea mtafaruku na hubidi nyumba ima kutiwa bei na kuuzwa au kununuliwa na mrithi mmoja kisha kila mmoja akapata sehemu yake.

 

Ama mjane kiwango chake kinafahamika vilivyo nacho ni thumuni kama Alivyobainisha Allaah Aliyetukuka:

Na wake zenu watapata robo mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumuni ya mlichokiacha, baada ya wasia mliousia au kulipa deni” (Qur-aan 4: 12).

Ndugu wa kiume na wa kike wa aliyefariki watarithi pia kwa kuwa aliyefariki hakuacha mtoto wa kiume. Kwa hiyo, binti 2 wa aliyefariki watapata kila mmoja thuluthi.

 

Jadwali ya wirathi itakuwa kama ifuatavyo:

 

Namba

Uhusiano na Aliyefariki

Kiwango

Asilimia

1

Mjane

Thumuni (1/8)

12.5

2

Binti 1

Thuluthi (1/3)

33.33

3

Binti 2

Thuluthi (1/3)

33.33

4

Kaka

 

10.42

5

Dada 1

 

5.21

6

Dada 2

 

5.21

 

Jumla

 

100.00

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share