Mke Kazini Kisha Kakanusha Kwa Mumewe Kwa Kuapa Nini Hukmu Yake?

 

SWALI:

Mme yuko ulaya kaowa afrika kwa kuwakilishwa na ndugu, sasa katika hali yakusubiri safari yakuletwa Ulaya mke katokea kuzini; alipokuja kufika ulaya mme akawa na kapewa habari zote na ushahidi wote wa zina ya mkewe lakini pamoja na ushahidi mke kakataa hadi akalazimishwa kuichukuwa Qu'ran na akapa kwa ajili yakuokoa ndowa na aibu. Kuna kosa hapa? Kwa pande zote mbili. Asalam alaykum warrahmatullahi wabarra



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuzini kwa mke wa mtu. Zinaa ni kitendo kibaya kwa Muislamu mwanamme au mwanamke kufanya na inabidi kila Muislamu kufanya juhudi ya kutoingia katika dimbwi hilo la maasiya. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amuepushe kila Muislamu na madhambi hayo na mengine.

Zinaa si jambo rahisi mtu tu kusema kuwa mtu Fulani amezini bali kunatakiwa ushahidi kama Alivyosema Allaah Aliyetukuka:

Na wanaowasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu” (24: 4).

Hapo juu umetuelezea kuwa upo ushahidi wa kuzini kwa huyo mke bila kutuambia ushahidi wenyewe ni upi na kama ni wa kuonekana kitendo hicho kufanyika, je, ni wa watu wangapi walioshuhudia?. Je, walipatikana mashahidi wanne kama inavyotakiwa? Je, mashahidi hao walikuwa wakimvizia na kumdadisi dadisi? Je, mashahidi walimuona mke huyo akiwa na mwanamme kitandani na uchi wa mume ukaingia katika uchi wa mke kama piston inavyoingia katika engine ya gari? Au ni vipi?

Maelezo hayo yote hayapo katika swali lako. Na kama mlituma watu wakumchunguza mjue ya kwamba mmefanya makosa kisheria. Ikiwa mashahidi hawakufika wanne pia ushahidi wenyewe haukubaliwi kisheria hadi wapatikane wanne. Na ikiwa mnamsingizia tu basi mtakuwa na dhambi kubwa zaidi linahitajia mpigwe bakora themanini kwa ajili ya hilo.

Hakika ni kuwa huwa tunafanya makosa kwa kuoa kisha kumuacha mke mbali ilhali mume yuko Ulaya kwa muda mrefu kabla ya kumchukua. Hiyo inampatia matamanio msichana ambaye yuko peke yake, na shetani wa kijini na wanaadamu ndio huwa wamepata fursa ya kumghilibu mpaka aingie katika madhambi.

Ama kuhusu ibara yako kuwa aliapa kwa kulazimishwa ili kuondoa aibu haifai kamwe kusemwa na Muislamu. Je, ulimfunua kifua chake na ukaona ni hivyo? Sisi tunatakiwa kuhukumu yalio dhahiri na ya siri tumuachie Allaah Aliyetukuka. Ikiwa mke ameapa kuwa hakufanya kitendo hicho basi chukueni dhahiri hiyo. Ama masuala ya kutumia msahafu kuapia, ni mas-ala yasiyo na dalili, msahafu haukuletwa kuapia, bali kinachoapiwa ni jina la Allaah, tena kiapo kiwe cha dharura na si utani utani. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa mwenye kubidi kuapa basi aape kwa jina la Allaah. Hakusema aape kwa jina lake (Mtume) au kwa msahafu au kwa chochote kingine.

Ingia katika kiungo kifuatacho upate Swali na Jibu kuhusu kukatazwa kuapia msahafu:

Kuapa Kwa Qur-aan Inafaa?

Na ikiwa mume alikuwa na wasiwasi akaona hataweza kuishi na mke huyo alikuwa afanye hivyo kabla ya kujamiiana naye na kumuachia nusu ya mahari.

Mas-ala ya zinaa tusiyachukulie kwa wepesi kama tunavyofanya kwani ni jambo zito sana.

Twawatakia kila la kheri bwana na bibi ikiwa wameamua kuishi pamoja na kusahau yaliyosemwa kabla.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share