Kuvaa Nywele Za Bandia Kufunika Nyewele Kwa Sababu Ya Kukatazwa Hijaab Katika Chuo Anachosoma

 

Kuvaa Nywele Za Bandia Kufunika Nywele Kwa Sababu

Ya Kukatazwa Hijaab Katika Chuo Anachosoma

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Asalaam aleykum, ALLAAH akuridhieni kwa kutufundisha uislam. suala la kuweka nywele za bandia,  mfano sisi tupo TURKEY na tunasoma katika mazingira magumu sana ya kiuslam, kwa mfano wasichana haturuhusiwi kuingia na hijabu shuleni na hata darasani. kwa hiyo huwa wanavaa mawigi na wachache wao huwa wanavaa makofia fulani ambayo huwa yanaficha nywele zao but walimu wengine huwa wanjua kwamba kwamba lengo la kuvaa lile kofia ni kuficha nywele kwa hiyo huwa wanawavua au wnawatoa darasani.kutokana na shida hii huwa wanaamua kuvaa nywele za bandia, naomba fatwa kuhusu hili....!

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  amekataza Muislamu kuvaa nywele za bandia na anayefanya hivyo atapata laana ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama ilivyokuja dalili katika Hadiyth ifuatayo:

 

Mwanamke wa Ki-Answaariy aliyemuozesha binti yake ambaye nywele zake zilianza kung'ooka.  Mwanamke huyo wa Ki-Answaariy alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kumtajia kwamba "Mumewe (mume wa mwanangu) ameona kwamba nimwachie avae nywele za bandia." Nabiy   (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Usifanye hivyo kwani Allaah Huteremsha laana Yake kwa  wanawake kama hao wanaoongeza nywele za bandia)) [Al-Bukhaariy 7:133  kutoka kwa Mama Wa Waumini 'Aaishah Radhwiya Allaahu 'anhaa]   

 

Ikiwa kama kuna dharura yoyote ile na ambayo itapelekea kukosekana kwa maslahi fulani ya mtu kujisaidia katika maisha yake basi ataruhusiwa kwa dharura. Ama kwa ambaye chuo chake kimemkataza kutekeleza Shariy’ah ya Allaahs  atalazimika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  na atafute Chuo ambacho anaweza kutekeleza Shariy’ah ya Allaah    na huku akiendelea na masomo yake, kwa sababu haifai kumridhisha kiumbe yeyote katika maasi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama alivyosema  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  

 

  ((على المرء المسلم السمع والطاعة فيما أحب وكره إلا أن يؤمر بمعصية، فإن أمر بمعصية فلا سمع ولا طاعة)   رواه مسلم  

((Muislamu inampasa asikie na atii katika anayoyapenda na anayoyachukia isipokuwa anapoamrishwa katika maasiya. Anapoamrishwa kufanya maasiya basi asisikie wa kutii)) [Muslim]

 

Na Allaah  Anajua zaidi

 

 

 

 

Share