Maisha Ya Kaburini (Yanapoanza Maisha Ya Barzakh)

 

Imekusanywa na Ummu ‘Abdillaah

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Leo in shaa Allaah tutaangalia ukurasa mpya wa maisha ya baadaye; maisha baada ya haya tuliyonayo hivi sasa hapa duniani. Na leo tutazungumzia maisha baada ya mja kufariki.

 

Maisha hayo kuanzia mtu anapokufa huitwa ni ‘Maisha Ya Barzakh’. Barzakh ni kipindi baina ya wakati wa mauti na Qiyaamah. Na kila maiti atapitia katika maisha hayo, awe Muislam au kafiri, mwema au mwovu, na katika kipindi hicho kunakuwa na fitna ya kaburi ambako mtu anajiwa na Malaika wawili na kuhojiwa na kisha hufuatia neema au adhabu za kaburini. Inajulikana kuwa kuna makazi matatu; makazi ya Dunia (Daarud Duniya), makazi ya Barzakh (Daarul Barzakh) na makazi ya kudumu (Daarul Qaraar).

 

Maisha ya Barzakh ni maisha yanayotofautiana kabisa na maisha ya dunia, na hakuna ajuaye hakika kamili ya maisha haya na namna yalivyo isipokuwa Allaah pekee.

 

Maisha ya kaburini ni kile kipindi anachokaa mtu baada ya kufa kwake mpaka kufufuliwa kwake. Kipindi kati ya parapanda la kwanza ambalo ni amri ya kufa viumbe vyote na parapanda la pili ambalo ni amri ya kufufuliwa viumbe vyote vitakavyotakiwa vifufuke, Huitwa Barzakh. Tunajulishwa kuhusu Barzakh katika Aayah ifuatayo:

 

“Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Nirudishe”,

“Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyoyaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapofufuliwa”. [Al-Mu-uminuwn: 99-100].

 

Katika kipindi hichi cha maisha ni mambo gani yanayoendelea katika nafsi ya mwenye kufa? Wengi kwa kujiliwaza katika wakati huo hufikiria kuwa watu wanakuwa mapumzikoni. Na watu ambao hawaamini siku ya mwisho huamini kuwa kifo ndio mwisho wa maisha ya watu na iliyobaki ni kuoza na kuwa chumvi chumvi zitakazotumika ardhini.

 

Katika kipindi cha Barzakh roho za watu wema zitakaa pahali pazuri kungojea malipo yao ya Peponi, Ama zile za watu waovu zitakuwa mahabusu zikingojea siku ya hukumu yao. Hivi ndio tunavyojifunza katika Hadiyth zifuatazo:

 

 

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesimulia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambae alisema: “Hakika maiti hupelekwa kaburini na hukaa kaburini bila ya khofu wala fadhaa. Baada ya hapo ataambiwa: “Ulikuwa katika nini? Atajibu: “Muhammad Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitujia na hoja zilizokuwa wazi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) na kwa hivyo tulimuamini. Ataulizwa tena “Umemuona Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala)?, Atajibu: “Si katika uwezo wa yeyote kumuona Allaah (‘Azza Wa Jalla). Kisha patawekwa uwazi utakaomuonyesha moto unaofoka. Kisha ataambiwa angalia kile ambacho Allaah Amekuokoa (Amekukinga nacho). Kisha patawekwa uwazi utakaomuwezesha kuiona Pepo na pia vyote vilivyomo ndani yake. Ataambiwa: “Hii ni sehemu yako kutokana na Uthibiti wa Iymaan uliyoishi nayo hadi kufa nayo na ambayo utafufuliwa nayo in shaa Allaah”.

Ama kuhusu mtu muovu yeye atakaa katika kaburi lake kwa khofu na fadhaa. Ataulizwa: Ulikuwa katika nini? Atajibu sijui. Kisha ataulizwa tena: Ni nani huyu? Atajibu nilisikia watu wakisema kama nilivyosema. Kisha utawekwa uwazi kwa kumuwezesha kuiona pepo ataangalia na kuona uzuri wake na vilvyomo ndani yake. Ataambiwa: Angalia kile ambacho Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Amekukosesha (Kutokana na Iymaan yako mbovu). Kisha utawekwa uwazi wa kumuwezesha kuona na ataambiwa hii ndio sehemu yako ambayo uliendesha maisha yako kwa kuwa na mashaka nayo, Na umekufa ukiwa na mashaka nayo na utafufuliwa ukiwa katika hali hiyo hiyo, in shaa Allaah”. [Ibn Maajah].

 

 

Pia tunapata Hadiyth nyingine kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesimulia kuwa:

“Mwanamke wa kiyahudi alimwendea na kumsimulia adhabu ya kaburi, Akamwambia; Allaah Akukinge na adhabu ya kaburi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) akajibu; “ndio”, Adhabu ya kaburini ni jambo la kweli: ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alisema: Sikumuona Mtume baada ya hapo kuswali Swalah yoyote bila ya kumuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Amkinge na adhabu ya kaburini”. (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

 

Pia tuangalie katika Hadiyth ifuatayo inatueleza nini juu ya maisha ya Kaburini.

 

Bara’a bin ‘Aazib amesimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) akisema:

“Malaika wawili watamjia (maiti), Watamkalisha na kumuuliza: Ni nani Bwana wako? Atajibu: Allaah pekee Ndiye Bwana wangu. Kisha watamuuliza tena, Ni nani huyo aliyeletwa kwenu? Atajibu: Alikuwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam). Watamuuliza tena; Amekuleteeni habari gani? Nimesoma kitabu cha Allaah nikaamini kutokana nacho na nikaithibitisha ‘Iymaan hiyo (katika matendo)”.

Na pia tuangalie Kauli Yake Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Asemavyo katika Kitabu Chake kuwa:

“Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika Aakhirah. Na Allaah Huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Allaah Hufanya Apendavyo” [Ibraahiym: 27]

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) akasema:

“Mtangazaji (mwenye kunadi) atatangaza (atanadi) kutoka mbinguni: Hakika mja Wangu amesema ukweli. Mtengeeni sehemu Peponi na mvisheni mavazi ya Peponi, Na mfungulieni mlango wa Peponi. Kisha utafunguliwa. Akasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) na hewa ya Peponi na harufu yake nzuri ya manukato itamjia na Pepo itakurubishwa kwake kiasi cha upeo wa macho. Ama kwa kafiri asiyeamini, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) alitaja kifo chake na akasema: Roho yake itarudishwa katika kiwiliwili chake na Malaika wawili watamjia, Watamkalisha na kumuuliza: Ni nani Bwana (Mola) wako? Atajibu: Haa! Haa! Sijui! Watamuuliza tena: Ni ipi dini yako? Atajibu: Haa! Haa! Sijui! Kisha watamuuliza ni nani huyo aliyeletwa kwenu? Atajibu Haa! Haa! Sijui! Kisha mwenye kunadi atanadi kutoka mbinguni: Hakika amesema uongo, Kwa hiyo mkunjulieni kitanda cha motoni. Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) Kisha joto lake na upepo wa moto utamjia na kaburi lake litakuwa jembamba sana kwake mpaka mbavu zake mbili zitapishana.

Kisha atakabidhiwa kwa Malaika kipofu na kiziwi mwenye pande (rungu) la chuma, Kama mlima ungelipigwa na chuma hicho ungelikuwa vumbi. Atampiga kwa chuma hicho kwa kipigo ambacho kitasikika kwa kila aliye mashariki na magharibi ispokuwa viumbe wa aina mbili (Majini na Watu) hawatasikia. Atakuwa vumbi na kisha roho itarudishwa tena kwake.” (Ahmad na Abu Daawuwd).

 

In shaa Allaah siku zijazo tutaendelea na maisha baada ya kufufuliwa.

 

Share