Kutuma Ujumbe Wa Makumbusho Ya Dini Kwa Kutishana Au Kubashiria

SWALI

:

Assalam alaikum

Miaka ya karibuni kumekuwa na tabia ya baadhi ya waislamu kutuma ujumbe kwa simu kwa wenzao unaotaja dua, dhikri fulani au mafundisho fulani kisha kuomba ujumbe utumwe kwa watu wa 5,7 au10 na utapata ulitakalo au utaona miujiza, na pia huongezea kwamba usidharau. Je nini ukweli wa jambo hilo? Naomba ufafanunuzi kwa faida ya wengi kwani nimepata msg nyingi katika simu yangu na nadhani si mimi tu.

Wabillahi tawfiq

   

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunamshukuru ndugu yetu kwa swali hili muhimu ambalo limeenea sana siku hizi kupitia katika simu za mikono na mtandao.

Kukumbushana mambo ya Mwenyeezi Mungu kama kupelekeana du'aa au dhikr na kadhalika ni jambo jema baina ya Waislamu kwani Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

((وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَى تَنفَعُ الْمُؤْمِنِينَ))

((Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini))

[Adh-Dhaariyaat: 55] 

 

Ama kulazimisha mtu kufanya kitendo cha ibada kisichokuwa fardhi haifai. Kwanza inatupasa tutambue kuwa dini yetu haimlazimishi Muislamu kufanya kitendo zaidi ya zile fardhi alizofaridhiwa, anapofanya mtu zaidi hupata thawabu na asipofanya hapati dhambi.  Vile vile kumkirihisha mtu katika dini si jambo Alilotuamrisha Allaah سبحانه وتعالى.

 

Hatari zaidi ya mas-alah haya ni kulazimisha mtu na kumtisha kwamba atume kwa watu  kiasi fulani na kama hakutuma mtu atapata khasara fulani au kubashiria kuwa pindi akituma atapata bahati fulani. Kwa mfano mtu anaweza kusema:  "Kama hukuutuma ujumbe huu basi utafikwa na msiba au mambo mabalaa mbali mbali na kama utautuma basi utafanikiwa katika siku tatu au kama hivyo."

 

Hakika haya ni mambo ya shirki na kufru  yaliyopita mipaka, kwasababu watu wanajaribu kujitia sifa za Uungu kuwa wanajua mambo fulani yatayotokea katika siku tatu au siku kumi na mbili na kadhalika.  Haya ni  mambo ya ghayb (yasiyoonekana).   Na elimu hii ya ghayb hakuna aijuaye isipokuwa Mwenyewe Mola Mtukufu kama Anavyosema:

((وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لاَ يَعْلَمُهَا إِلاَّ هُوَ))

((Na ziko Kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu))

[Al-An'aam: 59

].

 

Na Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika Hadiythi iliyotoka kwa Ibn 'Umar رضي الله عنه   

((مفاتح الغيب خمس لا يعلمها إلا الله: إن الله عنده علم الساعة، وينزل الغيث، ويعلم  ما في الأرحام، وما تدري نفس ماذا تكسب غدا، وما تدري نفس بأي أرض تموت، إن الله عليم خبير)) أحمد

((Funguo za ghayb [mambo yasiyoonekana au kujulikana] ni matano ambayo hakuna ayajuwae isipikowa Allaah 

"Hakika kuijua Saa (ya Qiyaamha) kuko kwa Allaah. Na Yeye Ndiye Anayeiteremsha mvua. Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allaah Ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.”

(Surah Luqmaan: 34).

[Imesimuliwa na Imaam Ahmad].

 

Vile vile   Allaah سبحانه وتعالى Ametoa onyo kwa mtu mwenye kuingilia katika elimu yake ya ghayb.

((أَاطَّلَعَ الْغَيْبَ أَمِ اتَّخَذَ عِندَ الرَّحْمَنِ عَهْدًا ))

 

(( كَلَّا سَنَكْتُبُ مَا يَقُولُ وَنَمُدُّ لَهُ مِنَ الْعَذَابِ مَدًّا ((

((Kwani yeye amepata khabari za ghaibu, au amechukua ahadi kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema?))

((Hasha! Tutaandika anayoyasema, Tutamkunjulia muda wa adhabu))

[Maryam: 78-79

].

 

Kwa hiyo kama tunavyoona kuwa kuna hatari kubwa ya Muislamu kuingia katika kufru na shirk kwa kuingilia elimu ya ghayb ya Allaah سبحانه وتعالى .  Na Allaah سبحانه وتعالى Anasamehe madhambi yote ila shirk.

 

Jambo muhimu kabisa ni kuwa ni wajib wa kila Muislamu anapopata ujumbe wa aina yoyote wa dini, kwanza ahakikishe usahihi wa huo ujumbe.  Kama ni Hadiythi basi LAZIMA KWANZA ahakikishe kama ni Hadiythi Sahihi au dhaifu, na kama ni Sahihi basi inafaa kuwapelekea wenzake kuwakumbusha bila ya kumtisha mtu au kumbashiria mtu faida ya kutuma huo ujumbe kuwa atapata faida fulani wakati Hadiythi yenyewe haikusema hivyo.  Na kama Hadiythi ni dhaifu basi ni wajib wake kumnasihi mwenzake aliyemtumia kuwacha kuituma na yeye pia asiitume kwa mtu yeyote ili kusimamisha uzushi kuenea kwa Waislamu wenzetu kwa hatari ya uzushi ni moto wa Jahannam kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))

[Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Na Allaah Anajua Zaidi 

Share