Bima Ya Maisha (Life Insurance) Inaruhusiwa Katika Uislamu?

SWALI:

 

Assalaam alaikum warahmatu llaahi wabarakatuhu,ningependa kuuliza swali ambalo baadhi yetu latutatiza,je yafaa kwa muislamu kuwa na life insurance, assalaam alaikum

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu life Insurance katika Uislamu.

 

Katika miongo iliyopita, wanachuoni maarufu wamejadili suala la Ta’miyn (insurance) kwa kina na kufikia uamuzi au fatwa tofauti. Kuna rai tatu katika mas-ala haya ya insurance (bima), nazo ni:

  1. Wapo wanaosema kuwa bima ya maisha ni haramu. Hoja yao ni kuwa kuna riba ndani yake, kamari, gharar (kuuzwa bidhaa isiyojulikana) na bahatisho na ulanguzi wa matakwa ya Allaah.

  2. Kuna gharar ndani yake kwa sababu hakuna anayejua dhamana inayochukuliwa na kampuni itapatikana lini. Hii ni gharar kubwa ambayo inaleta kasoro, hivyo kuifanya kuwa haramu.

  3. Rai ya tatu ni ile ya wanaosema kuwa gharar katika mkataba inaondolewa kwa elimu ya juu na wazi za takwimu na kufanyiwa kazi nadharia ya makisio. Kwa hiyo hakuna gharar kwa mwenye kuchukua bima na mkataba huo unaruhusiwa kwa masharti mawili: kuwe hakuna kipengele cha riba na kinachowekewa bima ni halali. Ama kuhusu gharar anasema kuwa kima chenyewe ni kidogo sana hivyo kuweza kupuuzwa. Ikiwa imewekwa kama sharti na mwajiri au na serikali hiyo inakuwa ni dharura inayokubaliwa na sheria lakini baada ya kufanya juhudi kuiondoa na ikiwa ni mwajiri wako tu amekupatia bila kuitaka hiyo inakubalika.

Zipo bima za maisha (life insurance) aina mbili: term policy na endowment policy. Ya awali inamaanisha kuwa mwenye kuweka bima atakuwa anatoa kiwango maalumu kwa miaka wanaokubaliana, mfano miaka 20, kwa kupata faida kwa familia yake kwa kiwango kikubwa anapoaga dunia katika muda huo. Ikiwa atabaki hai baada ya muda huo, inakuwa imekwisha na hatapata chochote. Anachonunua mwenye bima ni utulivu wa akili kwa kule kujua kuwa lau atakufa, watu wake watapata pesa nyingi kuwawezesha kuishi maisha ya raha, na watoto wataweza kujitizama wenyewe.


Ama aina ya pili, endowment (wakfu) policy inahitaji malipo makubwa zaidi ambayo yataingizwa katika biashara na kampuni ya bima. Policy ikiwa tayari, aliyeweka bima atapata pesa zake alizoweka na faida juu ambayo atapata kulingana na biashara na mkataba wenyewe waliowekeana.

 

Lakini tukiitazama hii bima kwa mtazamo halisi wa Kiislamu tutakuta ya kwamba haifai kwa Muislamu kujiingiza kwa sababu ya utata uliopo na mara nyingi kampuni inachukua pesa kutoka kwa wateja kisha kwa sababu moja au nyengine inafungwa na watu kukosa haki zao. Na kisha hali ya kuwa katika bima huwa kuna riba ndani yake na gharar inafanya isiwe halali kwa Waislamu. Na katika Uislamu inatakiwa biashara iwe nipe nikupe, haiwezekani kuwa wewe unatoa bila kupata huduma aina yoyote ile. Na pia hakuna biashara katika dunia ambayo inapata faida kuna kupata na hasara, hii faida maalumu mnayoandikia iko kinyume na Uislamu.

 

Kisha unaweka akiba katika bima kama hizo kwa kuwa watoto wako wafaidike kumaanisha kuwa bila kufanya hivyo hawawezi kufaidika. Huo ni utovu wa Imani kwa Allaah Aliyetukuka, kwani ukiwa na Imani utakuwa ni mwenye kumtegemea Allaah kwa kila hali na hutababaishwa na chochote.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atutengenezee mambo yetu na Atuepushe na haramu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share