Surah Saba Ziitwazo Sabaa Munjiyaat Ni Swahiyh Kuzisoma Kila Siku?

SWALI:

 

Nashkuru sana kwa kupata nafasi kama hii yakuweza kusoma na kuskiza mawaidha na manufaa mengi kutoka kwa hii website. Mungu awajazi kheri na awajaalie muzidi kutupa faida, amin.

 

Kama mwezi uliopita nilikwenda dukani kununua kitabu cha dini, nikamkuta dada mmoja tulisalimiana vizuri baada ya kumaliza akaniambia, kuna sura jumla yake ni saba akazitamka "SABAA MUNJIYAATI" na akaniandikia hizo sura nazo ni: Surat sajida, yasiin, Dukhan, Waqia, Hashry, Tabaraka na hal-ataa. Akaniambia sura hizi ni nzuri unatakiwa kuzisoma baada ya sala ya magharibi mpaka Ishaa. Suali langu ni nini faida au uzito wa sura hizi?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hizo ulizosema ni Sab‘ah Munjiyaat. Hakika isiyopingika ni kuwa yapo mambo mengi sana ambayo yamezoeleka kwetu ambayo si sahihi kwa kiasi kuwa mambo kama hayo kufutika inakuwa vigumu. Mara nyingi huwa tunajitia mashakani kwa mambo ambayo hayapo na hivyo tunatoka katika usahali na wepesi wa Dini hii yetu ya kweli.

 

Tumejaribu kutafiti sehemu mbalimbali hilo lakini hatukupata popote. Na hadi kutazama katika CD mbili moja ya tafsiyr ya Qur-aan na nyingine ya Hadiyth na ufafanuzi wake. Tumejaribu kuingiza neno Munjiyaat kutazama katika CD hizo mbili, tukapata kuwa katika vitabu 320 vya Hadiyth neno hili linapatikana katika Hadiyth 55, nyingine zikiwa ni dhaifu na maudhui lakini hakuna hata moja yenye neno saba. Na katika vitabu vya tafsiri 25, tumepata neno hilo lipo katika sehemu 6 pekee kwa maelezo yasiyohusiana na Sab’ah Munjiyaat. Hii ni ishara kuwa jambo hilo halipo katika Dini yetu.

Labda tukadhani huenda ikawa imeashiriwa katika fadhila za Surah kwa hivyo tukaanza kutazama katika tafsiyr za wanazuoni wetu. Yale tuliyoyapata ni kama yafuatayo:

 

1.      Mwanzo tuelewe kuwa zipo Surah as-Sajdah mbili, moja ni Alif Laam Miym as-Sajdah (32) na nyingine ni Haa Miym as-Sajdah kwa jina lingine Fuswilat (41). Ama kuhusu ya mwanzo, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Swalah ya Alfajiri ya siku ya Ijumaa Alif Laam Miym as-Sajdah na Suratul Insaan (76)” (al-Bukhaariy na Muslim). Ama kuhusu Ha Miym as-Sajdah hakuna chochote kuhusu fadhila yake.

 

2.      Ama kuhusu Surah Yaasin (36) Hadiyth nyingi zilizokuja ni dhaifu, ngeni na maudhui.

 

3.      Ama kuhusu ad-Dukhaan (44) ipo Hadiyth inayosema: “Mwenye kusoma Haa Miim ad-Dukhaan usiku ataamka akiwa ameombewa msamaha na Malaika 70,000”. Hii ni Hadiyth ngeni na al-Bukhaariy amesema kuwa ni Munkar (isiyo julikana).

 

4.      Ama Suratul Waaqi‘ah (56), imepokewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kusoma al-Waaqi‘ah kila usiku hatapatwa na ufakiri milele”. Hata hivyo, Hadiyth hii na nyenginezo ni dhaifu kama alivyosema Sh. Muhammad al-Albaaniy.

 

5.      Ama kuhusu Suratul Hashr (59) hakuna fadhila iliyotajwa kuhusu hilo ila ubora wa ayah tatu za mwisho ambazo zinasomwa asubuhi na jioni lakini Hadiyth kuhusu hilo ni ngeni.

 

6.      Ama Tabaaraka (Suratul Mulk – 67) zipo Hadiyth nyingi ambazo ni dhaifu na munkar sana kama ile ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ni kiokozi na kuwa ni moyo wa Qur-aan na nyingine ni ngeni. Ile ambayo ni Sahihi ni: “Hakika Surah ya Qur-aan ina ayah thelathini (30) itamuombea sahibu wake mpaka asamehewe: Tabaarakal Ladhiy Biyaadihil Mulk” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

 

7.      Hadiyth iliyo sahahi katika haya ni ile iliyopokewa kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa halali usiku mpaka asome Alif Lam Miim Tanziil (as-Sajdah) na al-Mulk” (Ahmad, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, ad-Daarimiy na kusahihishwa na al-Haakim).

 

8.     Ipo Hadiyth nyingine ambayo imetajwa na ash-Shawkaaniy katika Tafsiyr yake ya Fat-hul Qadiyr kuhusu fadhila ya baadhi ya hizi Surah. Hadiyth yenyewe inasema: “Mwenye kusoma usiku Suratul as-Sajdah, Yaasin, al-Qamar (54) na al-Mulk basi itakuwa ni nuru na kukingwa na Shetani na atanyanyuliwa daraja na kukingwa hadi Siku ya Qiyaama” (Marduwiyah). Tumejaribu kuitazama Hadiyth hii katika vitabu na tovuti zenye Hadiyth pamoja na usahihi wake lakini hatukuipata na pia tukaitazama katika CD yenye Hadiyth ya huyu mpokezi lakini pia hatukuipata. Hivyo usahihi wa Hadiyth kama hii haujulikani.

 

 

Muislamu mzuri ni yule ambaye anafanya bidii kusoma Qur-aan kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa kuelewa na kufuata. Ikiwa zipo Hadiyth Sahihi kuhusu fadhila ya Surah yoyote ile basi tutaikubali na tutaifanyia kazi na ikiwa hakuna Hadiyth sahihi basi ni vizuri kujiepusha na hayo yenye utata na turidhike kwa zile chache sahihi tulizozipokea kutoka kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share