Nataka kujua matumizi ya Surah Yaasiyn na Ayatul Kursiy

SWALI:

Nataka kujua matumizi ya Surah Yaasiyn na Ayatul Kursiy

NAFIKIRAI KWA LEO NDIO MWISHO wa maswali ninamatumiani nitaafahamishwa vizuri nawatakia kila la kheri waislam wenzangu

 
 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

.

Shukrani zetu kwa swali lako .

hilo

Hakika ni kuwa watu wanaifanyia vishindo Surah Yaasiyn. Hivyo wakabuni na kutumia Hadiyth dhaifu. limewafanya Waislamu kuipa nyongo Qur-aan nzima na wakawa wanaisoma Surah hii peke yake na nyingine chache. Hii ni kinyume na agizo la kuisoma Qur-aan pole pole na kidogo kidogo kuanzia Suratul Faatihah hadi an-Naas. Hadyith nyingi kuhusu fadhila za Surah hii ni dhaifu na za uwongo (kubuniwa).

 

Miongoni mwa Hadiyth hizo kuhusu fadhila ya Surah hii ni ile ya at-Tirmidhiy inayosema: “Kila kitu kina moyo wake, na moyo wa Qur-aan ni Yaasin. Atakayeisoma mara moja, Allaah Atamuandikia thawabu za kwamba ameisoma Qur-aan yote mara kumi”. Mwenyewe at-Tirmidhiy papo hapo alipoitaja alisema kuwa hii ni Hadiyth ngeni, yaani aina ya Hadiyth dhaifu. Nyingine ni ile inayosema: “Kuisoma Yaasiyn kunampa msomaji alilolikusudia”. Hii ndiyo kabisa haina nguvu hata chembe wala tamko hili si la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ama Aayatul Kursiy (2: 255) ni Aayah Tukufu . Anahimizwa kila Muislamu kuihifadhi na kuisoma nyakati nyingi kwani zimekuja Hadiyth nyingi juu ya fadhila zake. Miongoni mwa Hadiyth ni:

 

v      Kabla ya Kulala: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kuisoma anapokuwa kitandani (kwa ajili ya kulala) hakika atakuwa katika hifadhi ya Allaah wala hatakaribiwa na shetani mpaka kupambazuke” (al-Bukhaariy). Na Hadiyth nyingine ni kule kufundishwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na shetani na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Amesema kweli japokuwa yeye ni muongo ” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

v      Shetani hutoroka: Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Musiyajaalie majumba yenu kuwa makaburi, hakika shetani anatoroka kwa nyumba inayosomwa Suratul Baqarah” (Muslim). Na Hadithi nyingine ni ile inasema: “Mwenye kusoma ayah kumi za Suratil Baqarah, haitaingia shetani”. Mojawapo ni ayatul Kursiy.

v      Kusomwa asubuhi na jioni: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kuisoma asubuhi huepushwa na jinni mpaka jioni, na mwenye kuisoma jioni huepushwa na jinni mpaka asubuhi” (al-Haakim na kusahihishwa na al-Albaaniy).

v      Baada ya Swalah ya faradhi: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kuisoma baada ya kila Swalah hakitomzuia kuingia Peponi isipokuwa kifo”.

Kwa hivyo hizi ni baadhi ya Hadiyth zinazoonyesha fadhila za Ayatul Kursiy. Hakika itakuwa ni muhimu kwetu kuweza kuihifadhi na kuisoma kila wakati ambao umesuniwa kufanya hivyo ili tupate ulinzi kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share