Tafsiyr Ya Aayah Kuhusu Uadilifu Wa Yatima

SWALI:

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi.

Tafadhal naomba uniasaidie kutanzua mushkel nilionao.

1. Katika Aya ifuatayo (4:3) nashindwa kuelewa ni vipi uadilifu kwa mayatima unaunganishwa na kuowa wake zaidi ya mmoja.

 3. Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana.

 Katika Aya hii hapa juu sehemu ya mwisho inayosema “Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana". Hii ina maana gani?

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa maswali yako 3, na tunatarajia kuwa tutaondoa mushkila wako kwa majibu yetu yafuatayo:

Mushkila uliopo kwa ibara uliyotuandikia ni kuwa umetumia tafsiri moja bila kutizama ima maelezo yaliyopo chini au kutazama Mufasirina wengine wamesema nini. Je, Mufasirina wameafikiana kwa hilo au? Tafsiri uliyotumia ni ile ya al-Muntakhab iliyotarjumiwa na Sh. Ali Muhsin Al-Barwaaniy. Hebu tutazame tafsiri nyingine zinasemaje kuhusu Aayah hiyo.

  • Shaykh Al-Amiyn ‘Aliy Mazrui amesema: “Hilo ni karibu zaidi na kutofanya dhuluma” (Tafsiri ya Qur’ani Tukufu, Mjalada 2, uk. 89).

  • Mwenye Tafsiyr Jalalyn amesema: “Huko ni karibu zaidi ili musipindukie mipaka” (uk. 77).

  • Shaykh Abdallaah Swaalih al-Farsy amesema: “Kufanya hivi ndiko kutapelekea kutofanya jeuri” (Qur’ani Takatifu).

  • Dkt. ‘Aliy ‘Abdul-Haliym Mahmuud amesema: “Yaani huko ni karibu zaidi kutopindukia kwa haki na ujeuri. Na hili ndilo chaguo la Mufasirina wengi.

  • Dkt. Muhammad Sulaymaan al-Ashqar amesema: “Kubaki na mke mmoja ni salama zaidi kwa kutokuwa na ujeuri wa mmoja wao juu ya mwingine. Na amesema ash-Shaafi‘iy: ‘Allaa Ta‘uuluu’ ili msikithirishe wana. Na amesema Sufyaan: ‘Allaa Ta‘uuluu’ ili msikose” (Zubdatut Tafsiyr min Fat-h al-Qadiyr, uk. 98).

Tutaona kuwa ibara hiyo ya Aayah ina maana nyingi sana lakini yote haya yanalenga upande mmoja tofauti na tarjuma ya Sh. Barwaaniy. Hata hivyo maelezo ya mwenye al-Muntakhab ni kuwa: “Na ni afadhali msije mkawa na watoto wengi bila ya kiasi hata mshindwe kuwatazama. Wafasiri wengi wamependelea kufasiri, ‘Allaa Ta‘uuluu’ kuwa ‘Kutofanya jeuri au dhuluma’. Lakini tafsiri hii imekhiari tafsiri ya ‘Msikithirishe wana’, ambayo ndiyo aliyofuata Imaam ash-Shaafi‘iy na watangu wema wengine (Mj. 1, uk. 157 – 8). Hivyo, utaona kuwa hii tafsiri uliyoinukuu inatumiwa na wachache miongoni mwa wanazuoni tofauti na ile nyingine.

Hata hivyo Shaykh Al-Amiyn ‘Aliy Mazrui amesema katika maelezo yake: “Hilo ni karibu zaidi na kutofanya dhuluma” maana yake ni kuwa kuoa mke mmoja au kuweka suria tu ni bora zaidi kwa asiyeweza kusimamisha uadilifu baina ya wake. Wafasiri wengine wamefasiri kipande hiki kwa maana haya: ‘Hilo litawazuia zaidi kuwa na watoto wengi’. Na hapana shaka kuwa wingi wa watoto ndio wingi wa mayatima. Kwa maneno mengine, kila watoto wakipungua na mayatima watapungua” (Tafsiri ya Qur’ani Tukufu, Mjalada 2, uk. 90). Kwa maelezo hayo ya Shaykh Mazrui ibara hiyo ya al-Muntakhab inaeleweka kwa uwazi zaidi.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share