Anaweza Kuoa Kisiri Kwa Sababu Mke Wa Mwanzo Kasema Atajiua Akioa?

SWALI:

 

Assalam Alaikum Warahmatullahi Wabarakatu, Suala langu lipo katika kutaka kuoa mke kwa siri hii ni kwa kutokana mimi ninataka kuoa lakini mke wangu yeye hataki uke wenza, na nilijaribu kuoa kwa siri yeye alijaribu kutaka kujiua kwa kula vidonge kwa vile nimezaa nae ninashindwa kufanya nae lolote katika masuala ya kumuacha na amenitishia kuwa kama nitaoa basi yeye pamoja na watoto wote atawaua na kwa mtazamo wangu ninahisi kweli anaweza kufanya jambo kama hilo kwani kama nilivyoeleza kuwa amewahi kula vidonge suala lipo hapa kweli mimi ninaweza kuoa kwa siri kwa makubaliano baina ya mimi na huyo mwanamke ninaetaka kumuoa kuwa tuweke siri na kama huyo mwanamke ataridhika na hayo yote je ninaweza kumuoa?

Ninawaombeni nipate jawabu kwa faida ya wote wasomaji wenzangu Inshaallah ALLAH atawalipa kwa kazi yenu hii ya kutuelimisha na sisi tunaimani kubwa kwenu na tunayafuata yote maelekezo yenu Asallam alaikum


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa ya siri.

 

Tufahamu ndugu zetu kuwa ndoa ni katika sheria ya Dini. Na kwa kuwa ni hivyo itakuwa ina masharti yake kama mambo mengine yote.

 

Masharti ya ndoa ni kama yafuatayo, na ndoa ikikosa sharti moja haitasihi Kiislamu:

 

  1. Mwanamke unayetaka kumuoa aridhike kuolewa.

  2. Walii wa mwanamke akubali na kutoa idhini.

  3. Wewe pia uridhie pamoja na kutoa mahari mtakayokubaliana.

  4. Kuwepo na mashahidi wawili waadilifu.

 

Sasa ikiwa ni siri kwa kuwa mtaelewana wewe na yeye peke yake jambo hilo halitasihi kisheria. Na pia tutatoka katika kanuni aliyoiweka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema: “Itangazeni ndoa”. Na pia tufahamu kuwa kuoa mke wa pili au watatu, mume hahitaji ruhusa ya mkewe wa kwanza.

 

Tuseme umefanya ndoa kwa masharti ya hapo juu, kisha kwa sababu moja au nyengine mke wako akajua utafanya nini? Na huwezi kumficha mkeo kwani mabadiliko yataonekana tu na hivyo kumtafutia madhara huyo mkeo wa pili. Je, mkeo akijua utamuacha huyo wa pili? Ikiwa nia yako ni hiyo utakuwa umemdhulumu mkeo, na dhuluma ni jambo ambalo halitakikani katika Dini hii yetu. Kufanya hivyo utamtia mashakani yake mke wa pili, kwani pengine huenda akashika uja uzito, ambao itabidi alee pekee mimba na mtoto. 

 

Ushauri ambao tunaweza kukupa ni kuwa usiingie katika dhuluma kwa njia yoyote ile. Ima watumie watu wa kuzungumza na mkeo wa kwanza au zungumza naye mwenyewe au mtafutie kanda za mawaidha au vitabu vinavyozungumzia suala hilo la uke wenza. Huenda hayo yakamlainisha na kuridhia bila kuleta matata. Na hatari kubwa uliyonayo nyumbani ni kuwa inaonyesha mkeo Dini yake ni chache sana ikiwa anaweza kujiua jambo ambalo litamuingiza motoni basi anaweza kufanya lolote. Ubaya zaidi atakuwa amekanusha hukmu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyoruhusu wake wanne.  Inabidi umpeleke katika madarasa ambako kunafundishwa Dini au hasara utakayoipata ni kubwa. Huenda akiwa atasomeshwa Dini akabadilika kwa kiasi kikubwa.

 

 

Tunakuombea tawfiki katika uzito uliokufikia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share