House Girl Sio Wale Waliomiliki Mikono Yetu Ya Kuume

SWALI:

ASSALAM ALEIKUM.  JE, NI KWELI KUWA TUMERUSIWA TENDO LA NDOA KWA WAKE ZETU NA ILIYOMILIKI MIKONO YETU YA KIUME? MIMI NIKIFANYA TENDO HILO NA KIJAKAZI (HOUSE GIRL) NIPO SAHIHI. SHUKRAN.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Shukrani kwa swali lako hili muhimu. Si tu tendo hilo la ndoa bali matendo yote anayofanya Muislamu yanatakiwa yaende sambamba na Qur-aan na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ikiafikiana na machimbuko hayo, Muislamu huyo atakuwa anapata thawabu na ikitoafikiana basi atakuwa anapata dhambi.

Katika mas-ala ya tendo la ndoa, Qur-aan ipo wazi kabisa: “Na ambao wanazilinda tupu zao, isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa” (23:5-6). Hivyo, Muislamu akifanya kitendo cha ndoa na mkewe au iliyowamiliki mikono yao ya kuume inakuwa yuko katika misingi ya sheria na hivyo kuwa yuko katika ‘Ibadah. Ndio Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Na kujamiiana kwenu ni sadaka”. Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah, mmoja wetu huyajia matamanio yake na akawa atapata thawabu?” Akasema: “Mwaonaje lau aliiweka (tupu yake) katika haramu, angekuwa na dhambi? Basi ni kama hivyo akiiweka tupu yake pa halali atakuwa na thawabu” (Muslim kutoka kwa Abu Dharr).

Huenda kukawa na utata kuhusu wale ambao mikono yetu ya kuume imewamiliki. Lakini ni jambo ambalo liko wazi kabisa katika Dini yetu. Waliomilikiwa na mikono yetu ya kuume ni wale wanawake ambao wameshikwa kama mateka katika Jihaad baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Hawa kawaida walikuwa wakipatiwa Waislamu ili kuweza kuwatunza lakini walikuwa na haki kama kuvishwa, kulishwa na mambo mengineyo ya msingi kupatiwa.

Uislamu ukaweka mfumo wa hawa watumwa kujipatia uhuru wao ili wasibaki katika hali hiyo daima kama ilivyokuwa ada katika Ujahiliya. Katika njia hizo ni kuandikiana ikiwa mtumwa ana ujuzi wa kufanya kazi na kupata pato awe atalipa kiwango fulani mpaka atakapomaliza kiwango hicho. Njia ya pili ni kule kuhimizwa Waislamu kuacha huru, nalo likawa ni lenye fadhila na thawabu nyingi mbele ya Allah Aliyetukuka au pia kwa mwenye kufanya kosa fidia yake ilikuwa ni kuacha mtumwa huru. Na Uislamu ukaweka kuwa hata pesa za Zakah zinaweza kutumiwa kununua watumwa na kuwaacha huru. Mwenye mtumwa alikuwa anaweza kumfanyisha kazi bila ya malipo, isipokuwa isiwe ni kazi ambayo ni ngumu unatakiwa hapo umsaidie.

Ukija katika mas-ala ya mfanya kazi wa nyumbani (house girl) si mateka bali ni mfanya kazi kama wafanya kazi wengine. Na hawa ma-house girl wanalipwa mshahara kwa wiki, mwezi au ujira wa siku na kazi yake inajulikana kuwa ni kadhaa na kadhaa, naye wakati wowote anaweza kukwambia ya kuwa hataki tena kazi au wewe mwenyewe ukamfuta kazi kwa sababu moja au nyingine. Kwa tofauti hii Muislamu hana ruhusa ya kumuingilia house girl kama alivyopatiwa ruhusa na Allah Aliyetukuka kumuingilia yule ambaye mikono yake ya kuume inayommiliki.

Hivyo, utakapofanya kitendo hicho na mfanyakazi wa nyumbani utakuwa umefanya makosa na utaingia dhambini kwa hilo. Hiyo itakuwa ni zinaa ambayo umeifanya, na ikiwa ulikuwa una mke katika Shari'ah ya Kiislamu utastahiki upigwe mawe uuliwe na ikiwa hujaoa basi utapigwa mijeledi mia moja. Basi ikiwa umefanya kitendo hicho kwa wakati huu tusio na dola yenye kufuata Shari'ah ya Kiislam ambayo inaweza kutekeleza hukumu hiyo, ukiache mara moja, utubie na urudi kwa Mola wako Mlezi, uweke azma ya kutorudia kitendo hiko na ufanye mambo mema.

Nasaha zetu kwa walio na house girl katika majumba yao wasiwe ni wenye kufanya kitendo hicho cha haramu. Bali wanatakiwa hasa ikiwa hao si Waislamu wawaonyeshe uzuri wa Uislamu na muamala bora ili waweze kusilimu.

 

Na Allaah Anajua  zaidi

 

Share