Tafsiyr Ya Aayah “Na Arshi Yake Ikawa Katika Maji”

 

Tafsiyr Ya Aayah "Na Arshi Yake Ikawa Katika Maji"

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Naomba maelezo na mafundisho kutoka katika aayah "wakaana arshuhuu ala-lmaai" na

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Arshi ya Allaah Aliyetukuka.

 

Aayah hiyo inapatikana katika Suwrah Huwd (aayah 11). Aayah yenyewe inasema hivi:

 

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۗ وَلَئِن قُلْتَ إِنَّكُم مَّبْعُوثُونَ مِن بَعْدِ الْمَوْتِ لَيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ﴿٧﴾

Maana ya Aayah hiyo ni:

Na Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita; na ikawa ‘Arshi Yake juu ya maji; (kakuumbeni) ili Akujaribuni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Na kama ukisema: Nyinyi mtafufuliwa baada ya mauti; wale waliokufuru bila shaka watasema: Hakika haya si chochote isipokuwa ni sihiri bayana. [Huwd: 7].

 

Hebu tutazame hii ibara imefasiriwa vipi na Wanachuoni wetu wa tafsiyr.

 

Ibn Kathiyr naye amesema yafuatayo: “Allaah Aliyetukuka, Anatueleza kuhusu uwezo Wake na nguvu Zake, kuwa Ameumba mbingu na ardhi kwa siku sita. Ametaja kuwa 'Arsh Yake ilikuwa juu ya maji kabla ya hapo kama alivyonukuu Ahmad Amesimulia ‘Imraan Bin Huswayn (رضي الله عنه): Nilikwenda kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumfunga ngamia wangu jike mlangoni. Watu wa Bani Tamiym walikuja kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Enyi Bani Tamiym! Pokeeni bishara njema.” Wakasema mara mbili: “Umetupatia bishara njema, sasa tupatie kitu.” Kisha baadhi ya watu wa Yemen walikuja kwake, akasema: “Pokeeni bishara njema, enyi watu wa Yemen, kwani Bani Tamiym wamekataa.” Wakasema: “Tunaipokea ee Rasuli wa Allaah! Tumekuja kukuuliza kuhusu jambo hili (yaani mwanzo wa uumbaji).” Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Kwanza kabisa, hapakuwa na chochote ila Allaah (kisha Akaumba ‘Arshi Yake). ‘Arshi Yake ilikuwa juu ya maji, na Akaandika kila kitu katika Kitabu (cha mbinguni) na Akaumba mbingu na ardhi." 

Akanadi mtu mmoja kwa sauti: “Ee Ibn Huswayn! Ngamia wako jike amekimbia!” Nikaondoka mbio, lakini sikuweza kumuona ngamia wangu jike kwa sababu ya mazigazi. Naapa kwa Allaah! Natamani ningekuwa nimemuachilia mbali ngamia huyo jike (na sio kuacha kikao hicho).  [Al-Bukhaariy]

 

 

Muslim naye amenukuu kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Hakika Allaah Aliandika (kwenye Al-Lawh Al-Mahfuwdh) makadirio na hatima ya kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu khamsini na 'Arsh Yake ilikuwa juu ya maji".

 

 

Na Al-Bukhaariy amemkuu Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Je mumeona kilichotumiwa kuanzia kuumbwa mbingu na ardhi? Hakiko hicho (kilichotolewa) hakipunguzi kwa kilichomo Mkononi Mwake wa kuume (hata chembe) na 'Arsh Yake ilikuwa juu ya maji. Mkononi Mwake kulikuwa na mizani, Aliyokuwa Akiishusha na kuinyanyua" [Juzuu ya pili].

 

 

Al-Qurtwubiy amesema: “Allaah Amebainisha kuwa kuumbwa kwa 'Arsh na maji kulikuwa kabla ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi” [juzuu 5, uk. 8]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share