Kusoma Qur-aan Kwa Maandishi Ya Kilatini Atapata Thawabu Sawa Na Mwenye Kusoma Qur-aan Kwa Kiarabu?

SWALI:

 

ASSALAAMU ALAYKUM WARAHMATULLAHI WABARAKATUH.

Sifa njema zote in za Allaah. Namshukuru Allah Subhannah Wataallah kuniongoza kujiunga na uanachama na AL HIDAAYA. Nimekuwa napata makala zenu kupitia kwa wenzangu kwa muda mrefu na nimefaidika sana kielimu katika dini yetu tukufu ya Kiislamu. Allaah Subhannah Wataallah awajaze kila la kheri wahusika wote wanaojitahidi kuelemisha jamii ya kiislam kupitia mtandao huu.

 

Nina swali naomba msaada maana mie sikujaliwa kusoma Qurani kwa Kiarabu ila naisoma sana kwa Kiswahili.

 

Mwisho, je sisi tunaosoma Kitabu hiki Kitukufu kwa Kiswahili au kiingereza tutapata thawabu kama anayekisoma kwa Kiarabu?  Hasa wale ambao hata hawajui maana yake? Mie nina miaka zaidi ya 50 nashindwa kuimudu na kukariri isipokuwa sura fupi fupi ambazo zinaniwezesha kutimiza masharti ya swallah na duaah.

 

Jazaakum Allahu Khaira.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wanaomilkiwa na mikono yetu ya kuume. Hakika ni kuwa Aayah hizi ambazo umezitaja zinatupatia sifa za Waumini wa kihakika.

 

 

Kuhusu kupata thawabu katika kusoma ni kusoma Qur-aan katika lugha yake ya asili nayo ni kwa Kiarabu. Hii ni kwa mujibu ya Hadiyth iliyonukuliwa na at-Tirmidhiy, ambamo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Yeyote mwenye kusoma herufi moja ya Qur-aan anapata thawabu kumi wala sisemi Alif Laam Miym ni herufi, bali Alif ni herufi, Laam ni herufi na Miym ni herufi" (at-Tirmidhiy).

 

Hivyo, mwenye kusoma Alif Laam Miym anapata thawabu 30. Ama katika kusoma huko inafaa ieleweke kuwa inafaa tusiwe ni wenye kusoma kama kasuku bali tunahitajika kutilia maanani, kuzingatia, kujua maana na kufuata yaliyomo ndani. Ndio Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatueleza kuwa huenda tukawa tunasoma Qur-aan nayo inatulaani nasi hatuna habari kabisa.

 

Ama ukisoma Qur-aan kwa lugha nyingine hiyo haisemekani kuwa umesoma Qur-aan bali umesoma tafsiri ya Qur-aan. Kwa sababu hiyo tafsiri ni elimu utakuwa unapata thawabu ya kusoma mema na kusoma mambo mazuri. Tufahamu kuwa tunapata ujira kwa kusoma elimu na hakuna iliyo njema kama kusoma tafsiri ya Qur-aan.

 

Hata hivyo ndugu yetu tunakusihi bado unao muda wala hujakuwa mzee hivyo. Na lau utafanya bidii basi utaweza kusoma Qur-aan kwa Kiarabu bila ya matatizo yoyote kwa muda mfupi kabisa usiozidi hata miezi mitatu ikiwa utafanya bidii. Mfano mzuri ni hivi majuzi tu kulitoka habari za kuaminika za mama mwenye umri wa miaka 70 amekamilisha kuhifadhi Kitabu cha Allaah na habari hizo zikaenea kwenye tovuti mbalimbali za kuaminika, japo inaweza kuonekana kuwa hiyo ni kesi ya nadra, lakini hakuna kisichowezekana kwa uwezo wa Allaah na juhudi za mja. Kinachotakiwa ni wewe kuwa mkakamavu na mwenye bidii na hilo utaliweza bila ya shida. Kwa wakati huu wetu, zipo kaseti za Qur-aan nzima ikisomwa na wasomaji mahiri zenye kufunisha usomaji wa Qur-aan, zipo CD na njia nyingine za kuweza kujifunza, kinachotakiwa ni wewe kufanya bidii, kupanga muda, kufanya mazoezi ya kusoma na InshaAllaah utaweza kufikia malengo na kufanikiwa.

 

Pia tufahamu kuwa kujifunza Lugha ya kiarabu ni jambo muhimu sana kwa Muislam na kuna fadhila kubwa katika hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share