Anataka Tafsiri Na Ufafanuzi Wa Suwratun Nisaa Aayah Ya 15 - (Wafanyao Machafu)

 

Anataka Tafsiri Na Ufafanuzi Wa Suwratun Nisaa

Aayah Ya 15 - (Wafanyao Machafu)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam aleykum warahmatuLLahi wabarakaatuh. Shukrani sana ndugu zetu katika imani, inshALLAH Mola awalipe kheri kwa jitihada zenu za kututatulia yenye kututatiza katika dini yetu hii tukufu, namuomba ALLAH awalipe kheri hapa duniani pamoja na akhera nyinyi na sisi pia, amiin. Ammma ba'ad. Suali langu ni kwamba naomba ufafanuzi wa aya ya 15 suratul NNISAA (surat 4 verse 15), ningeomba tafsiri yake na ufafanuzi wake walau kidogo Biidhni LLAHI ta'ala. Shukran

 

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu tafsiyr ya Suwrah An-Nisaa 4: 15. Kabla ya kutoa maelezo tungependa kukuekea tafsiyr yake hapa chini, nayo ni kama hivi:

 

وَاللَّاتِي يَأْتِينَ الْفَاحِشَةَ مِن نِّسَائِكُمْ فَاسْتَشْهِدُوا عَلَيْهِنَّ أَرْبَعَةً مِّنكُمْ ۖ فَإِن شَهِدُوا فَأَمْسِكُوهُنَّ فِي الْبُيُوتِ حَتَّىٰ يَتَوَفَّاهُنَّ الْمَوْتُ أَوْ يَجْعَلَ اللَّـهُ لَهُنَّ سَبِيلًا ﴿١٥﴾

 

Na wale wanaofanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, basi washuhudisheni mashahidi wanne kati yenu. Na wakishuhudia basi wazuieni majumbani mpaka mauti yawafishe au Allaah Awajaalie njia (nyingine)”.

 

Aayah hii imefungamana na Aayah inayofuatia ya 16.

 

 

Maelezo yake ni kuwa: “Hizi ni Aayah zinazotaja kutiwa adabu wale,

 

(a) Wanawake wanaofanya machafu wao kwa wao, yaani kusagana na

 

(b) Wanaume wanaofanya machafu, yaani ya liwati na

 

(c) Wanawake wanaofanya machafu na wanaume.

 

Yote haya ni mabaya kabisa; na zaidi ni yale ya wanaume kwa wanaume, na baadaye wanawake kwa wanawake.

 

Maoni ya wanachuoni wa Tafsiyr wengi ni kuwa Aayah mbili hizi ni juu ya wazinifu. Hukmu zilotajwa zilinasikhiwa (zilifutwa) na kubadilishwa na zile Aayah 2-3 Suwrah An-Nuwr:

 

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ ۖ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢﴾

Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamme mpigeni kila mmoja katika wawili hao mijeledi mia. Na wala isiwashikeni huruma kwa ajili yao katika hukmu ya Allaah mkiwa nyinyi mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na washuhudie adhabu yao kundi la Waumini.

 

الزَّانِي لَا يَنكِحُ إِلَّا زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً وَالزَّانِيَةُ لَا يَنكِحُهَا إِلَّا زَانٍ أَوْ مُشْرِكٌ ۚ وَحُرِّمَ ذَٰلِكَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ ﴿٣﴾

Mwanamme mzinifu hafungi nikaah isipokuwa na mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina; na mwanamke mzinifu haolewi isipokuwa na mwanamme mzinifu au mshirikina. Na imeharamishwa hivyo kwa Waumini. [Suwrah An-Nuwr: 2-3]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share