Qur-aan Inasemaje Kuruhusiwa Kufanya Utafiti Wa Mas-ala Mbali Mbali?

SWALI:

 

Assalaam alaykum.

Qur-aan inasema nini kuhusu utafiti? Inatoa muongozo wowote kuhusu namna ya kufanya utafiti wa vitu mbali mbali? Kwa mfano kufanya utafiti wa chanzo cha tatizo fulani, au kujua jambo fulani, au utafiti wa chanzo cha ugonjwa fulani. Kuna utaratibu au muongozo wa namna ya kufanya utafiti wa mambo haya katika Qur'an? (Samahani, si utafiti wa Qur'an, bali Qur-aan inasema nini kuhusu kufanya utafiti wa mambo mbalimbali, utaratibu upi utumike.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu inavyosema Qur-aan kwa mas-ala ya kufanya utafiti. Uislamu ni Dini ya pekee iliyohimiza utafiti katika masomo yote kwa kutumia akili na vifaa vinavyohitajika katika mazingira na maadili ya Kiislamu. Hivyo, katika Uislamu hakukupatikana wataalamu waliochomwa au kuuliwa kwa sababu ya nadharia zao kama ilivyotokea katika karne za kati huko Ulaya. Kina Galileo na wengineo ni mfano mzuri kwa hilo.

 

Allaah Aliyetukuka katika Qur-aan Tukufu Anabisha ndani ya nyoyo zetu kwa nguvu na kutupigia ukulele ili tuzindukane. Ibara kama amkeni! Tazameni pembezoni mwenu! Fikirieni! Kuweni na tafakuri! Yupo Muumbaji!

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Hebu mtu na atazame chakula chake" (80: 24).

Na tena,

"Hebu na ajitazame mwanaadamu ameumbwa na kitu gani?" (86: 5).

Na pia,

"Je, hawamtazami ngamia jinsi alivyoumbwa?" (88: 17).

 

Hizi ni baadhi ya Aayah, zinazomhimiza Muislamu atumie akili na hisia zake katika kufanya utafiti. Maurice Bucaille anaandika katika kitabu chake: The Bible, the Qur'an and Science: "Hakuna Dini yoyote inayompwekesha Mungu inayoshutumu sayansi. Lakini hakika ni kuwa, kwa karne nyingi, ulimwengu wa Kikristo, ukuuzi wa kisayansi ulipingwa vikali sana. Kesi ya Galileo iko mbele ya kila mmoja wetu. Katika Uislamu mtazamo na msimamo wa sayansi ulikuwa tofauti. Qur-aan ilipokuwa inatuita kukuuza sayansi, yenyewe ina miono mingi ya kimaumbile, iliyo sambamba na maalumati ya kisayansi ya sasa".

 

Kwa hiyo, Uislamu unatuhimiza kufanya tafiti ili tuweze kuwahudumikia walimwengu kwa njia ya ufanisi na nzuri kabisa. Na hivi leo wasiokuwa Waislamu ndio wenye kufuata yaliyoelezwa katika Qur-aan na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika zile zenye kuelezea mas-ala ya sayansi na utafiti na kuitilia maanani na kuitumia katika uvumbuzi na tafiti zao, na huku Waislam wameacha mafundisho hayo.

 

Qur-aan ina takriban Aayah 750 zinayoelezea kuhusu maalumati tofauti katika masomo ya kiutafiti na sayansi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share