Skip navigation.
Home kabah

Vipi Atubie Kiapo Cha Uongo?

SWALI:

Assalamu aleikum

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu mwingi wa rehma, naomba mnijulishe nini hukmu ya kiapo cha uongo na kama mtu aliapa uongo na anataka atubie basi atatubia vipi. jazzakumullah kheir

 

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani sana kwa ndugu aliyeulizwa swali hili kuhusu Yamini, hasa katika enzi hizi zetu ambamo huwa tunaapa sana hata ikiwa hakuhitajiki kufanya hivyo.

Yamini katika sheria ni kula kiapo kwa Majina ya Allah Aliyetukuka au sifa Zake. Kwa mfano kusema, “Wallahi nitafanya kitu kadhaa” au “Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake au Mgeuza nyoyo”. Inajuzu kuapa kwa njia hiyo. Lakini haijuzu kuapa bila ya majina ya Allah na sifa Zake, ni sawa kinachoapiwa kinatukuzwa na sheria au la. Kama vile kuapa kwa Ka‘bah, au kuapa kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Anayeapa aape kwa Allah au anyamaze” (al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad). Na kauli ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Msiape ila kwa Allah na msiape ila muwe wakweli” (Abu Daawuud na an-Nasaaiy).

Kuapa kwa asiyekuwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni haramu, nayo ni shirki. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Atayemuapia asiyekuwa Allah basi amemshirikisha Allah au amekufuru” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ahmad).

Yamini inagawanyika sehemu, nazo ni:

1.      Al-Ghamuus:

Maana yake ni mtu kula kiapo huku anakusudia kuongopa, kama vile kusema: “Wallahi nimenunua kitu kadhaa kwa shilingi mia moja”, naye hakukinunua hivyo. Au kusema: “Wallahi nimefanya kadhaa”, na hali hakufanya. Hii imepatiwa jina hilo kwa sababu yamzamisha mwenye yamini hiyo ndani ya dhambi na yamini hii ndiyo iliyokusudiwa katika kauli ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Atakayekula yamini hali yeye katika yamini hiyo anaongopa (anasema uongo) ili apate kwa yamini hiyo kumega mali ya mtu mwingine Muislamu basi mtu huyo atakutana na Allah hali Amemkasirikia” (Al-Bukhaariy na Muslim).

Kafara peke yake haitatosha kwa yamini hii, bali pamoja na kafara mhusika anafaa alete toba na kuomba maghfira (msamaha) kwani kosa hili ni kubwa sana. Hasa ikiwa yamini hiyo itamfikisha kwenye kumega haki ya mtu mwengine Muislamu kwa njia isiyo ya halali. Hii ndio kauli ya jamhuri (Wanachuoni wengi), lakini rai ya Imaam Shaafi‘iy ni kinyume na hivyo, kwani yeye anawajibisha kafara tu. Mtu katika kutaka msamaha na kutubia anafaa afanye hivyo kikweli kweli, kwani Allah Aliyetukuka Anatufahamisha: “Enyi mlioamini! Tubuni kwa Allah toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi Akakufutieni maovu yenu na Akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Allah hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja naye” (66: 8). Katika hayo aweke azma na nia thabiti ya kutorudia kosa hilo, ajute kwa kufanya kosa hilo, afanye mambo ya kheri, ajiepushe na maasiya hayo. Ikiwa amemdhulumu mja mwenziwe basi amrudishie haki yake pamoja na kumuomba msamaha.

 

2.      Laghwul Yamiyn:

Hii ni ile ipitayo ulimini mwa Muislamu bila kuikusudia, kama yule ambaye katika mazungumzo yake hujitokeza kwa wingi mno wa neno: “Wallahi hapana”. Hii ni kufuatia kauli ya mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): “Upuuzi katika yamini ni maneno anayozungumza mtu nyumbani mwake, “Wallahi hapana”” (Al-Bukhaariy). Jumla ya yamini ya upuuzi Muislamu akala kiapo juu ya jambo fulani akilidhania liko hivyo ikaja ikabainika tofauti na alivyodhania. Hukumu ya yamini aina hii ni kuwa haina dhambi wala kafara kwa mhusika, kwa kauli yake Allah Aliyetukuka: “Allah Hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi” (5: 89).

 

3.      Yamini Iliyofungika:

Hii ni yamini inayochukuliwa kwa kukusudia jambo la baadaye. Kama vile Muislamu kusema: “Wallahi nitalifanya jambo kadhaa.. au Wallahi sitalifanya…” Hii ndio yamini atakayoadhibiwa atakaye fanya kinyume chake kwa kauli ya Aliyetukuka: “Lakini Atakushikeni kwa mnavyoapa kweli kweli kwa makusudio” (5: 89).

Hukumu ya yamini aina hii ni kuwa atakaye kwenda kinyume na alivyoapa atapata dhambi na atawajibika afanye kafara, kama atafanya kafara dhambi itaanguka na kumuondokea.

Kafara na dhambi itaondoka kwa mwenye kula yamini kwa mambo mawili:

1. Kutoweza kutekeleza yamini kwa kusahau au kwa bahati mbaya au kwa kulazimishwa. Hii ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Limeondolewa dhambi kwa Ummah wangu walilofanya kwa bahati mbaya, kusahau au kulazimishwa” (Ibn Maajah).

2. Avue wakati wa kuapa kwa kusema InshaAllah (Allah Akitaka) au pindi atakapotaka Allah, kama kuvua huko kutafanyika katika kikao cha yamini, kwa kauli ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Atakayekula yamini akasema InshaAllah hakwenda kinyume na yamini yake” (Ahmad, at-Timidhiy na an-Nasaaiy).

Yasuniwa kwa Muislamu kama atakula yamini ya kuacha jambo fulani miongoni mwa mambo ya kheri basi asifanye, na afanye kafara la yamini yake, kwa kauli ya Allah Aliyetukuka: “” (2: 224). Na kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kama utakula yamini ukaona lingine ni bora kuliko hilo basi lifanye hilo bora na fanya kafara la yamini yako” (Muslim).

Muislamu anapomlia yamini Muislamu mwenzake kuwa atafanya kitu, basi inamuwajibikia atekeleze kama alivyokula yamini, na asiende kinyume na yamini yake, na kufanya kafara muda upo uwezekano wa kutekeleza yamini yake. kinachozingatiwa katika kwenda kinyume na yamini na kutovunja ni nia na kusudio la mla yamini, kwa sababu matendo huthibitishwa na nia, na kila mtu atakipata alichokusudia.

Kafara ya yamini ni vitu VINNE, kama ilivyo katika kauli ya Aliyetukuka: “Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnachowalisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiyepata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu” (5: 89).

1.      Kulisha masikini kumi kwa kuwapa kila mmoja kibaba cha ngano, au kuwakusanya wote katika chakula cha mchana au usiku wale mpaka washibe.

2.     Kuwavisha nguo inayotosheleza katika Swalah, na kama atampa mtu mwanamke ampe kanzu (nguo ndefu) na mtandio kwa sababu huo ndio uchache wa vazi linalomtosheleza katika Swalah.

3.      Kumuacha huru mtumwa Muislamu.

       4.     Kufunga siku tatu mfululizo kama ataweza na     asipoweza basi atazifunga mbali mbali.

Hafungi ila baada ya kushindwa kulisha au kuvisha au kuacha mtumwa huru kwa mujibu wa ayah iliyopo hapo juu.

Tumeonelea tutaje vipengele kadhaa kuhusu yamini ili iwe ni faida kwa wengi wengine ambao mambo haya huwatokea. Na jibu la muulizaji lipo katika kigawanyo cha awali kabisa. Tunamuomba Allah Atufaidishe sote na Atupatie hima ya Dini Yake.

Na Allah Anajua zaidi