Dhul-Hijjah: Nini Sababu Ya Swawm Ya 'Arafah?

 

 

Nini Sababu Ya Swawm Ya 'Arafah?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum

Namshukuru Allah Suhaanahu Wataalah, nawashukuru nanyi kwa kutoa taaluma kwa nia hii. Maswali yangu ni: Ni ipi historia ya funga ya arafa? Jee, Mtume Muhammad (Swalla Allah alayh wassalam) alianza kufunga arafa kuanzia lini?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

  

Historia ya Swawm ya 'Arafah ni kwa ile fadhila kubwa iliyo nayo siku hiyo. Kwa kuwa walio katika Hijjah tarehe 9 Dhul Hijjah huwa katika wanga tukufu wa 'Arafah. Kwa hiyo, kwa wale ambao hawakwenda Hajj wanatakiwa wawe na ndugu zao Waislamu waliokuwa wamesimama hapo kwa Swawm. Ama wale ambao wako katika Hijjah wao hakuna ushahidi wa kufunga siku hiyo. Hiyo ni siku kwa utukufu Wake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anawaacha huru watu wengi na Moto.

 

Ama fadhila na ubora wa siku kumi za Dhul Hijjah pamoja na 'Arafah ni kama zifuatazo. Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Naapa kwa Alfajiri, Na kwa masiku kumi" (89: 1-2).

 

Na masiku kumi hayo ni siku kumi za mwanzo za mwezi wa Dhul Hijjah. Na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakuna masiku ambayo amali njema zinampendeza Allaah kuliko siku hizi", yaani masiku kumi. Akaulizwa: "Ee Rasuli wa Allaah! Hata Jihadi katika Njia ya Allaah?" Akasema: "Hata Jihadi katika Njia ya Allaah isipokuwa mtu atakayetoka kwa nafsi na mali yake, kisha asirudi na chochote kati ya hizo" (al-Bukhaariy, Abu Daawuwd na at-Tirmidhiy).

 

Na amepokea Abu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa aliulizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu swawm ya 'Arafah. Akasema: "Inafuta madhambi ya mwaka uliopita na unaofuata" (Muslim).

 

Kwa faida zaidi bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah - 01 - 10 Dhul-Hijjah

 

 Fadhila Za Siku Ya 'Arafah Na Yawmun-Nahr (Siku Ya Kuchinja)

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share