Vipi Kutekeleza Umrah
SWALI:
ASALAM ALAYKUM.
TAFADHALI NAOMBA MNIJULISHE YANAYOPASA KUFANYA KTK UMRA TOKA KUKUSUDIA KWENDA MAKKA DUA ZA KUSOMA
SHUKURAN
JIBU:
Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza tunatambua kutokana na barua yako kuwa wewe ni mwanamke hivyo haikupasi kwenda ‘Umrah peke yako bila ya kuwa na Mahram (mumeo au kaka zako au baba au ‘ami au yeyote mwenye undugu wa damu na wewe ambaye kisheria hawezi kukuoa)
‘Umrah kawaida unaweza kuikamilisha kwa siku moja tu, bali ni masaa machache tu utakuwa umemaliza ‘Umrah yako na sio
Yafutayo ni ya kufanya kwa mpangilio:
NIA
Nia ya ‘Umrah au ya ibada yoyote inakuwa moyoni na haitamkwi kwa ulimi. Kwa hiyo unapofika Miyqaat (sehemu ya kuanzia ibada yako hiyo, ambapo atakoga na kuvaa ihraam) utakapomaliza ndio utakuwa umetia nia yako moyoni kisha utaleta talbiyah ifuatayo:
لبيك عمرة، لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك.
Labbayka '‘Umrah, Labbayka-Llaahumma Labbayk. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk. Innal-Hamda Wan-Ni'imata Laka Wal-Mulk Laa Shariyka Lak.
"Nimekuitikia Ewe Mwenyeezi Mungu '‘Umrah, Nimekuitika Ewe Mwenyezi Mungu nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika Wako nimekuitika, hakika Sifa njema na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshrika"
Sehemu hiyo ya Miyqaat inategemea usafiri wako,
TWAWWAAF
Ni kuzunguka mara saba kuanzia Hajarul-Aswad (jiwe jeusi) na kuanza kwa kusema:
بسم الله والله أكبر
Bismillahi Wa-Allaahu Akbar
Unapozunguza Twawwaaf, unaweza kusoma Qur-aan au kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) yaani Subhaana Allah, au Kumshukuru, yaani Alhmadulillah, au Tahliyl yaani Laa Ilaah Illa Allah, au kuleta takbiyr yaani Allaahu Akbar, au kumswalia Mtume (Swallah Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), au kusoma duaa zozote unazotaka. LAKINI sio kusoma vile vitabu ambavyo vinauzwa na vimeandikwa duaa za kila Twawwaaf na du’aa yake, vitabu hivyo vimeandikwa na watu na havina ushahidi kutoka katika Hadiyth za Mtume kuwa alifundisha du’aa hizo zilizopangiliwa kwenye hivyo vitabu, bali ni mambo ya uzushi na juu ya hivyo yanasababisha zahma za watu kwa kutembea pole pole huku wakisoma vitabu kwa sauti. Ni bora kusoma du’aa zako mwenyewe unazohitajia kwa matatizo yako na shida zako, kwani hiyo ni fursa ya kuomba kila unachokitaka na kutamani kuliko kusoma vitabu hivyo ambavyo wengi hawajui hata maana ya yaliyoandikwa ndani yake.
Na kila unapofika katika Rukn (nguzo) ya Yamani hadi katika jiwe jeusi unasema:
رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الاَخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ
((Rabbanaa Aatinaa Fid-Duniyaa Hasanataw-Wafil-Aakhirati Hasanataw-Waqinaa 'Adhaaban-Naar)).
"Mola wetu Mlezi, Tupe duniani mema, na Akhera mema, na Utulinde na adhabu ya Moto”
Ukifika katika Hajarul-Aswad (jiwe jeusi) utaashiria kwa mkono wako kuelekea jiwe
بسم الله والله أكبر
Bismillahi Wa-Allaahu Akbar
Utakuwa umemaliza Twawwaaf moja. Utaendelea hivyo hadi umalize Twawwaaf (mizunguko) zote saba.
Haifai kujilazimisha kwenda kuligusa au kulibusu Hajarul-Aswad na kusababaisha zahma na kusongamana zaidi na watu kwani inatosheleza kuashiria kwa mkono na thawabu ni zile zile, bali pengine ni zaidi kuliko mwenye kusababisha kusukumana na wenzake kwa ajili ya kutaka kuligusa jiwe.
RAKAA MBILI KATIKA MAQAAMU IBRAHIYH
Ukimaliza Twawwaaf ya saba utasogea upande wa Maqaamu Ibraahiym na utaswali Rakaa mbili, Rakaa ya kwanza utasoma Suratul-Kaafiruun (Qul Yaa Ayyuhal-Kaafiruun) na ya pili utasoma Suratul Ikhlaasw (Qul-Huwa Allahu Ahad).
Kwa hali ilivyo hivi sasa sehemu hiyo imekuwa ni zahma sana, hivyo haikupasi kujilizamisha kuswali karibu kabisa na Maqaamu Ibraahiym, bali unaweza kusogea mbali kabisa almuradi umeelekea hiyo Maqaam ya Ibraahiym. Ni makosa kusababisha zahma zaidi na msongamano na kuswali sehemu ambazo zina zahma kuzidi kuleta mashaka kwa Waislamu wengine.
SA’Y
Utakwenda Swafaa na kuanza Sa’y kwa kupanda juu ya kilima cha Swafaa na utaelekea Kaaba na kusema:
لا إِلهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لا إِلَهَ إلا اللهُ وَحْدَهُ أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ
Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu Laa Shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr. Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu, Anjaza Wa'dahu Wanaswara 'Abdahu Wahazamal-Ahzaaba Wahdahu))
“Hapana Mola Apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa peke Yake, wala Hana mshirika Wake, ni Wake Ufalme na ni Zake sifa njema. Naye juu ya kila kitu ni Muweza. Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke Yake, Ametekeleza ahadi Yake, na Amemnusuru mja Wake, na Amevishinda vikosi peke Yake”
Utaomba du’aa zako unazotaka kisha utaanza Sa’y ukifika Marwa utakuwa umemaliza Sa’y moja, utapanda kilima na kusema hivyo hivyo na kuomba kwa kuelekea vile vile Ka’abah. Kuanzia Swafaa na kufika Marwa unahesabu kuwa ni moja, na kutoka Marwa na kufika tena Swafaa ni mbili hivyo hivyo hadi utamalizia Sa’y yako ya saba katika kilima cha Marwa.
Kama ni mwanamme atanyoa au kukata nywele, na wewe utakata tu kidogo nywele zako
KUNYWA MAJI YA ZAMZAM
Utakunywa maji ya zamzam na kuomba du’aa unayotaka na hapa utakuwa umemaliza ‘Umrah yako.
YA KUZINGATIA:
Du’aa hizo ni kuzisoma kwa Kiarabu tu.
Unaweza kunywa maji ya Zamzam kabla ya Sa’y au baada yake upendavyo.
Kwa maelezo zaidi tafadhali soma mada hii ifuatayo ambayo iko www.alhidaaya.com katika kiungo kifuatacho:
Bonyeza hapa:
Na Allah Anajua zaidi
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


