Kusujudu Baada Ya Kusoma Aayah Yenye Sajdah (Sijdah At-Tilaawah)

SWALI:

Suala la pili kuhusu sijida ya kisomo, nataka kujua ulazima wake:  jee ni lazima mara tu ukizisikia ayah hizo kusujudu hata kama huna udhu japo kwa ishara. jee kuna ushahidi wowote.

    


 

JIBU:

 

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Sajdah ya Tilaawah (ya kisomo) ni sijda ambayo husujudiwa wakati wa anaposoma mtu Qur-aan na kukutana na ayah inazungumzia kusujudu au pia mtu anaposikia Aayah inasomwa ambayo inahusiana na kusujudu.

 

Fadhila zake:

Hadiyth iliyoelezwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘Anhu) ambayo anasema: Amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): ((Anaposoma mwanaadam (ayah) ya kusujudu kisha akasujudu, shaytwaan atajitenga na kulia, atasema: Ole wake (akijiambia yeye), ameamrishwa (mwanaadam) kusujudu akasujudu na ana pepo, nami niliamrishwa kusujudu nikaasi na nina moto)) Muslim, Ibn Maajah na Ahmad

 

Ama fadhila za kusujudu kwa ujumla, ziko hadiyth nyingi ila tutatosheka na hiyo inayohusu swali.

 

Kila mwenye kusoma au kusikia kisomo cha ayah yenye sijdah anafaa asujudu, ili kutoa dalili ya kimatendo kwa kuonyesha unyenyekevu na utiifu kwa Allah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na kwenda sambamba na Malaika Wake. Katika Qur’an zipo sehemu (15, na wengine katika Maulamaa wamesema ni 14 kwani ipo tofauti katika ile sijdah ya Suratu Swaad. Tazama hapo chini kwa majina ya Surah na nambari ya ayah ambamo Muislamu anapaswa kusujudu anaposoma au kusikia zikisomwa) ambapo Muislamu anafaa kusujudu. Wanachuoni wote wamekubaliana kuwa sijdah ifanywe katika sehemu hizo, lakini wametofautiana kuhusu hadhi yake ya ulazima. Kulingana na Maimam Ath Thawry, Abu Haniyfah ni wajibu (lazima) na moja ya kauli ya Imam Ahmad, na Imam Ibn Taymiyah kaendana na msimamo huo vilevile. Lakini wanachuoni wengine pamoja na Maimamu wakubwa waliobaki wamesema kuwa ni pendekezo (si lazima). Inatakiwa ifahamike kuwa kitendo cha kupendezwa kufanya  hakina hadhi sawa na faradhi lakini kukiacha kwa makusudi japokuwa si dhambi inachukuliwa ni makosa kwa Muislamu mwema na mzuri na kukiacha kabisa ni makosa.

 

Namna ya kusujudu kwake ni sijdah moja tu. Anasujudu mtu kama anavyosujudu kwenye sijdah ya Swalah kwa viungo vyake saba; kuweka viganja viwili ardhini (vidole vikiielekea Qiblah), magoti mawili, na matumbo ya vidole vya miguu (akijitahidi vidole vielekee Qiblah), na kipaji cha uso na pua (vikihesabika ni kitu kimoja) na ahakikishe kapanua viwiko vyake (asiibane mikono yake kwenye mbavu zake) na tumbo lisigusane na mapaja yake.

Hakujawekewa sheria kupiga takbiyrah ya ihram ukitaka kusujudu sijdah hiyo wala kutoa salaam baada ya kusujudu.

Kunapendezwa kupiga takbiyr wakati wa kusujudu na wakati wa kunyanyuka baada ya kusujudu kwa kauli ya wanachuoni wengi.

 

Ni bora anayetaka kusujudu sijdah hiyo asimame kwanza kisha ashuke kusujudu sijdah hiyo ya kisomo, nah ii ni rai ya madhehebu ya Hanbali, wanachuoni wa kihanafi na moja ya muono wa Imaam Shaafi’iy, na wamechukua msimamo huo kuegemea katika Ayah ifuatayo:

((Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale waliopewa ilimu kabla yake, wanaposomewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu.))  [Al Israa:107]

Na ingawa wanachuoni wengi wanaonelea kuwa ni sharti mtu kuwa na wudhuu anapotaka kusujudu sijdah ya tilaawah kwa hoja kuwa masharti ya Swalah ndiyo masharti ya sijdah hiyo, lakini Imaam Ibn Hazm, Shaykhul Islaam Ibnu Taymiyah, Imaam Al Bukhaariy na Ash Sha’aby wanatoa hoja ya kuwa haiwezi kuwekewa sharti ya twahaarah kwa sababu sijdah ya kisomo si Swalah bali ni tendo la ibada na kwa hivyo halihitajii ulazima wa twahaarah. Na huo ndiyo msimamo wa Swahabah Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Na dalili ni hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kuwa Mtume (([Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam] alisujudu kwenye (kisomo cha) surah ya An Najm na wakasujudu pamoja naye waislam, washirikina, majini na binaadam)) [Al Bukhaariy na At Tirmidhy]

 

Hata hivyo, pamoja ni kuwa si lazima kuwa na wudhuu au kuelekea Qiblah kwa sijdah hiyo, lakini ni bora na afadhali zaidi kusujudu ukiwa na wudhuu na kuelekea Qiblah, na haipendezi kuacha kufanya hivyo ikiwa huna udhuru ingawa kama ilivyotajwa nyuma kuwa si sharti.

Ama kuhusu jinsi ya kufanya sijdah hii, tunajifunza kutoka kwenye Hadiyth kuwa ilikuwa tofauti katika hali na sehemu tofauti. Wakati mwengine Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) alipokuwa akisoma ayah inayohitajia sijdah, alikuwa anasujudu papo hapo na kila mmoja katika kikao hicho alikuwa akifanya hivyo, kwa kiasi kwamba wapo watu ambao walikuwa wanakosa nafasi ya kusujudia kwayo hivyo kumfanya asujudu kwenye mgongo wa mwenziwe. [Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Ibn ‘Umar [Radhiya Allaahu 'Anhu] 

 

Pia tunakuta Hadiyth kuwa wakati wa kutekwa kwa Makkah, Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)  alikuwa akisoma kisomo na akafika katika ayah inayohitaji sijdah. Wale waliokuwa wamesimama walisujudu kwenye sakafu na wale waliokuwa juu ya vipando (farasi na ngamia) waliitekeleza hapo hapo juu ya wanyama wao.

Wakati mwengine alipokuwa akihutubu na akafika katika ayah ya sijdah alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) anateremka chini ya minbar kusujudu kisha akapanda tena na kuendelea na khutbah. Na ‘Umar (Radhiya Allaahu 'Anhu) naye alikuwa anafanya hivyo hivyo wakati mwengine na maamuma wote nao wakimfuata na mara nyengine alikuwa hasujudu (Al-Bukhaariy). 

 

Waislamu wengi wana rai kuwa masharti ya kufanya sijdah hii ni kama yale ya kutekeleza Swalah, lakini hakuna dalili kwa rai hii kutoka kwenye Hadiyth. Tunapata kutoka kwao (Maswahaba) kuwa alipokuwa akisikia ayah mojawapo ya sijdah ikisomwa basi akiinamisha kichwa chake katika hali yoyote ile. Alikuwa hajali kama ana wudhuu au la; ikiwa anaweza kuelekea Qiblah au la; ikiwa anaweza kusujudu juu ya sakafu au ardhini au la. Tunapata mifano ya wasomi na watangu wema wakifanya hivyo. Kulingana na Imam Al-Bukhaariy, ‘Abdullah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu 'Anhu) alikuwa akisujudu akiwa na wudhuu au hata bila ya wudhuu. Imenukuliwa katika Fat-hul Baari kuwa Abu ‘Abdur-Rahmaan as-Sulaamiy (Radhiya Allaahu 'Anhu) alikuwa akisoma Qur’an katika hali ya kuwa anatembea na alikuwa akiinamisha kichwa chake tu anaposoma ayah ya sijdah, hakukuwa na tofauti akiwa ana wudhuu au hapana, na wala akiwa ameelekea Qiblah au popote.

 

Kwa haya tunahitimisha kuwa japokuwa wengi wanakubaliana katika njia ya kusujudu lakini mtu asikemewe akifanya njia nyengine iliyofanywa na watangu wema (salafu swaalih) kama tulivyoona hapo juu kwani hii njia ya wengi haina dalili katika Sunnah.

 

Hadiyth kadhaa za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)  zinatufundisha kusujudu papo hapo unaposoma au unaposikia ayah hiyo ya sijdah. Al-Bukhaariy na Muslim wametaja Hadiyth ya Ibn ‘Umar, Abu Hurayrah na Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu 'Anhu) kuhusu hilo. Ndio Sayyid Saabiq katika Fiqhus Sunnah akasema ikiwa mtu hakusujudu baada ya kuisoma au kuisikia mojawapo ya ayah hizo basi hakuna kulipa baada ya muda kupita.

 

Katika sijdah hiyo, mtu atasema Allaahu Akbar wakati anataka kusujudu na akisujudu atasema Subhaana Rabbiyal A‘alaa.  

 

Kisha akinyanyuka atasema Allahu Akbar.  

 

 

Surah pamoja na Ayah zake ambazo inampasa Muislamu asujudu kwayo ni kama zifuatazo:

1.  Suratul A‘raaf (7) ayah ya 206.

2.  Suratul Ra’ad (13) ayah ya 15.

3.  Suratul An-Nahl (16) ayah ya 50.

4.  Suratul Israa’ (17) ayah ya 109.

5.  Suratu Maryam (19) ayah ya 58.

6.  Suratul Hajj (22) ayah ya 18.

7.  Suratul Hajj (22) ayah ya 77.

8.  Suratul Furqaan (25) ayah ya 60.

9.  Suratun Naml (27) ayah ya 26.

10. Suratus Sajdah (32) ayah ya 15.

11. Suratusw Swaad (38) ayah ya 24.

12. Suratu Fuswswilat (41) ayah ya 38.

13. Suratun Najm (53) ayah ya 62.

14. Suratul Inshiqaaq (84) ayah ya 21.

15. Suratul ‘Alaq (96) ayah ya 19.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share