Kusoma بسم الله (BismiLLaah) Katika Kila Suwrah

 

Kusoma  بسم الله  (BismiLLaah) Katika Kila Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam Alaykum, na kheri ya mwezi mtukufu wa Ramadhwaan, na fadhila zake In shaa Allaah zitushukie sote - Amin. Amma ba'ad:

 

Je, usomapo Qur-aan, ni kweli kuwa kusema Bismillahi ni Sunna na siyo faradhi? Kwa hiyo tunaweza kuswali na kusoma Quraani bila ya Bismillahi kama kwenye Suwrah Tawba, kwa kuwa Bismillahi ni sunna? Naomba mnijibu haraka, In shaa Allah.

Wabilahi Tawfiq, ndugu yenu katika imaan.

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Unapoanza kwanza kusoma Qur-aan inakupasa ujikinge na Shaytwaan kwa kusoma al-Isti'aadhah (A'wudhu Billaahi Minash-shaytwaanir-Rajiym). Kwa sababu hivyo ndivyo tulivyoamrishwa: 

 

فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ﴿٩٨﴾

Unaposoma Qur-aan basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa. [An-Nahl: 98] 

 

Kujikinga huko unatakiwa usome ikiwa ni mwanzo wa Suwrah au hata katikati ya Suwrah. Na ikiwa mwanzo wa Suwrah basi lazima isomwe na BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym ilivyo katika kila mwanzo wa Suwrah. Isipokuwa Suwrah-Tawbah pekee ambayo haina BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym. Kwa hiyo hakuna hapa chaguo isomwe BismiLLaahi au isisomwe bali Suwrah zote zenye kuanzwa na BismiLLaah zinapaswa kuisoma BismiLLaah.   

Ikiwa umeanza katikati ya Suwrah unaweza kusoma Isti'aadhah pekee ukaendelea na Suwrah, au pia unaweza kusoma zote mbili Isti'aadha na BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym. Na pia wakati ukindeleza Suwrah japokuwa haina katikati BismiLLaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share