Kulia Wakati Wa Kusoma Qur-aan Kunamaanisha Nini?

SWALI:

Ningependa kuuliza swali kuhusu quran,unaposoma na ukawa unalia je nini?maana yake ni nini?

 


 

 

JIBU:  

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

Unaposoma Qur-aan ukalia, bila shaka ni nyongeza ya imani katika moyo wa msomaji, kwani hayo ni maneno ya Mola Mtukufu, maneno ambayo nafsi zilimtambua kabla ya kuumbwa duniani na kumuitikia kuwa zitamtii. Dalili ya kuwa ni imani ni kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

 ((إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا))

((Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allah nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aayah Zake huwazidisha imani)) [Al-Anfaal:4] 

Vile vile Anasema:

 ((وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَذِهِ إِيمَانًا فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُواْ فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ))

((Na inapoteremshwa Surah wapo miongoni mwao wasemao: Ni nani miongoni mwenu Surah hii imemzidishia imani? Ama wale walioamini inawazidishia imani, nao wanafurahi)) [At-Tawbah:124]

 

Anasema pia Allaah سبحانه وتعالى kwamba kuzidishiwa imani hiyo ni uongofu kutoka Kwake.

 ((اللَّهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُّتَشَابِهًا مَّثَانِيَ تَقْشَعِرُّ مِنْهُ جُلُودُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ ثُمَّ تَلِينُ جُلُودُهُمْ وَقُلُوبُهُمْ إِلَى ذِكْرِ اللَّهِ ذَلِكَ هُدَى اللَّهِ يَهْدِي بِهِ مَنْ يَشَاء))

((Allaah Ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Allaah. Huo ndio uongofu wa Allah, na kwa huo Humuongoa Amtakaye)) [Az-Zumar: 23] 

Kama tunavyoona katika Aayah hiyo tukufu, kwamba kusoma Qur-aan husisimua ngozi na kutia khofu nyoyo na kuulainisha hadi imsababishe mja kutokwa machozi.  Na aghalabu humtokea mja mwema khaswa mwenye elimu ya Qur-aan anapofahamu maneno ya Mola Wake na kutambua uzito  wa maneno Yake Allaah سبحانه وتعالى yenye khofu, bishara na hikma, kama wale ambao Allaah سبحانه وتعالى  Aliowataja katika Aayah ifuatayo:

 ((إِنَّ الَّذِينَ أُوتُواْ الْعِلْمَ مِن قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَى عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلأَذْقَانِ سُجَّدًاً ))  

 ((وَيَقُولُونَ سُبْحَانَ رَبِّنَا إِن كَانَ وَعْدُ رَبِّنَا لَمَفْعُولاً )) 

  ((وَيَخِرُّونَ لِلأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا ))

((…hakika wale waliopewa ilimu kabla yake, wanaposomewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu))

((Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola wetu! Hakika ahadi ya Mola wetu lazima itimizwe!))

((Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu)) [Al-Israa:107-109]

Ndio maana vile vile Anatuambia  Allaah سبحانه وتعالى kuwa inaposomwa Qur-aan tuwe tunaisikiliza ili tuifahamu na tupate Rahma Yake:

 ((وَإِذَا قُرِىءَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُواْ لَهُ وَأَنصِتُواْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ))

((Na isomwapo Qur-aan isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemewa)) [Al-A'raaf:204] 

Na ndipo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipomuomba Swahaba 'Abdullah bin Mas'uud رضي الله عنه  amsomee Qur-aan, akamsomea hadi alipofika Aayah fulani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akatokwa na machozi:

 عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه  قال: قال لي النبي صلى الله عليه وسلم ((اقرأ علي)) قلت: يا رسول الله، أقرأ عليك وعليك أُنزلَ؟ قال: ((نعم، إني أحب أن أسمعه من غيري)) فقرأت سورة النساء، حتى أتيت إلى هذه الآية: (( فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِنْ كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَى هَؤُلاءِ شَهِيدًا )) قال: ((حسبك الآن)) فإذا عيناه تَذْرِفَان.

Imetoka kwa 'Abdullah bin Mas'uud رضي الله عنه ambaye amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliniomba ((Nisomee [Qur-aan])). Nikasema: Ewe Mjumbe wa Allah, nikusomee na hali imeteremeshwa kwako? Akasema: ((Ndio, mimi napenda kuisikia [ikisomwa] kutoka mtu mwingine)). Nikasoma Suratun-Nisaa hadi nilipofika Aayah hii: ((Basi itakuwaje pindi tukiwaletea kutoka kila umma shahidi, na tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa?)). Akasema: ((Inakutosheleza sasa)) [yaani basi inatosha hadi hapo]. Nikaona macho yake yanatoka machozi. [Al-Bukhaariy]  

Mja Kulia anaposoma Qur-aan akiwa peke yake na akatokwa na machozi, pia ni bishara ya kwamba yeye atakuwa miongoni mwa watu saba waliotajwa kuwa watakuwa katika kivuli cha Allaah سبحانه وتعالى  siku ya Qiyaamah, siku ambayo hakutakuweko kivuli ila kivuli cha Allaah سبحانه وتعالى kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ   ((سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمْ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لا ظِلَّ إِلا ظِلُّهُ: الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَشَابٌّ نَشَأ فِي عِبَادَةِ رَبِّهِ، وَرَجُلٌ قَلْبُهُ مُعَلَّقٌ فِي الْمَسَاجِدِ، وَرَجُلَانِ تَحَابَّا فِي اللَّهِ اجْتَمَعَا عَلَيْهِ وَتَفَرَّقَا عَلَيْهِ، وَرَجُلٌ طَلَبَتْهُ امْرَأَةٌ ذَاتُ مَنْصِبٍ وَجَمَالٍ فَقَالَ إِنِّي أَخَافُ اللَّهَ، وَرَجُلٌ تَصَدَّقَ بِصَدَقَةٍ فَأَخْفَاهَا حَتَّى لا تَعْلَمَ شِمَالُهُ مَا تُنْفِقُ يَمِينُهُ، وَرَجُلٌ ذَكَرَ اللَّهَ خَالِيًا فَفَاضَتْ عَيْنَاهُ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watu saba Allaah  Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: Imaam muadilifu, kijana ambaye amekulia katika ‘Ibaadah ya Rabb wake, Mtu ambaye moyo wake umeambatana na Misikiti, watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah; wanakutana kwa ajili Yake na wanafarikiana kwa ajili Yake, mwanamme aliyetakwa na mwanamke mwenye hadhi na mrembo wa kuvutia akasema: "Mimi namkhofu Allaah!" Mtu aliyetoa Swadaqah yake akaificha hadi kwamba mkono wake kushoto usijue nini ulichotoa mkono wa kulia, na mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Kwa hivyo ndugu yetu tunakupa bishara njema na tunakuombea Allah Akuzidishie ungofu na Imani katika moyo wako pamoja na sisi sote.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share