Ipi Bora Kuhifadhi Qur-aan Yote Bila Ya Kujua Maana Au Kuhifadhi Kidogo Kwa Maana?

SWALI:

assalam alikum warhmatulahi wabarakayuhu nataka nipate ufumbuzi kuhufadhi koran ni kusoma zwahiri ,ao nikuhifadhi bila ya kujuwa mana yake ao ni kuhifadhi na mana yake? Kwa sababu nilisikia kama mtu akihifadhi koran hataingiya motoni.

Na nani kahifadhi kati ya yule anasoma koran yote bila kuifam mana yake na yule anae juwa sura kumi na mana yake? barakalahu ghair wasalam alikum warhamatulahi wa barakatuhu

 

 

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hakika ambayo haipingiki na yeyote mwenye akili timamu ni kuwa Qur-aan imeteremshwa na Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutimiza malengo fulani kwa wanaadamu. Lengo kubwa zaidi ni kuwaongoza watu wote katika njia nyoofu na ya sawa kama alivyosema Allah:

Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi” (2: 185) na hivyo hivyo kwa wacha Mungu, “Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uongofu kwa wacha Mungu” (2: 2).

Kwa minajili hiyo ni bora na muhimu zaidi kwa Muislamu kuisoma Qur-aan, kwa kuizingatia maana yake pamoja na kufuata kimatendo yaliyomo ndani. Hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya watangu wema. Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) alikuwa akisoma ayah kumi, anazihifadhi na kutekeleza kimatendo maagizo yaliyomo ndani yake. Kwa njia hiyo alichukua miaka kumi kuihifadhi Suratul Baqarah (Maalik).

Maswahaba nao ndivyo walivyokuwa wakifanya walikuwa hawachukui ayah nyengine hata kama zimeteremka leo mpaka zile walizokuwa nazo kuzihifadhi pamoja na kutwabikisha amri zilizomo ndani.

Haifai mtu kuhifadhi tu Qur-aan kama kasuku ijapokuwa kwa kusoma kila herufi utapata thawabu kumi. Huenda mtu akawa anasoma Qur-aan na huku inamlaani lakini hajui wala hatambui hilo. Pia sisi hatutakiwi tuwe na ile sifa ya Mayahudi kama Alivyosema Allah Aliyetukuka:

 “Mfano wa waliobebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu waliokadhibisha Ishara za Allah, na Allah hawaongoi watu madhaalimu” (62: 5).

Udhalimu unakuwa mkubwa ikiwa tutaibeba Qur-aan vifuani mwetu lakini hatuitilii maanani. Ndio Allah Aliyetukuka Akasema: “Je! Hawaizingatii hii Qur-aan? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?” (47: 24).

Nasiha zetu za dhati kwa ndugu zetu ni kuwa mtu asome juzuu au hizbu au hata ukurasa mmoja wa Qur-aan kila siku bila kuacha pamoja na kufanya bidii kuhifadhi surah au baadhi za Aayah anazoweza. Hivyo hivyo atenge wakati wa kusoma tafsiri kuanzia mwanzo wa Suratul Faatihah kidogo kidogo na kufanya juhudi kutekeleza hayo kimatendo.

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share