Vipi Kutupa Karatasi Zenye Aayah Za Qur-aan?

 

 

Vipi Kutupa Karatasi Zenye Aayah Za Qur-aan?

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Aleykum. natanguliza shukrani zangu kwenu na In Shaa Allaah, Allaah akulipeni ujira kwa kujitolea kwenu.amma baad, napenda kuuliza...mimi nilipewa kalenda ya sala ya mwaka mzima  na ndani yake ina aya za Qur-aan na majina ya Allaah ,na sasa kalenda hii imemaliza  nataka kwenda kuchukua mpya.. suali..je hii ya zamani natakiwa niihifadhi kila ninapokwenda  au naruhusika kuitupa na kama naruhusika basi naomba nifafanulie ni kwa namna gani? shukran.. samahani kama sikufahamika maana kidogo nina matatizo ya ufasaha wa lugha.. wabillahi ttawfik.

 

  

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Inafahamika vyema kuwa Qur-aan ni Kitabu kitukufu chetu na Aayah zake ni Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na (Tabaaraka wa Ta’aalaa).

 

Kitabu hiki ambacho hakina shaka ndani yake, na ni mwongozo  wa wamchao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kinafaa kitukuzwe kwa kusomwa, kuhifadhiwa na kufuatwa maagizo yaliyomo ndani yake. Hivyo, Aayah hizo zikiwa kwenye kalenda, fremu, picha, ukuta ni lazima ziwe ni zenye kupatiwa taadhima  inayostahili. Ifahamike kuwa Qur-aan haikuteremshwa ili kutiwa katika kalenda bali inatakiwa itiwe ndani ya vifua vya wana Aadam na kusomeshwa kama inavyotakiwa.

 

Zikiwa Aayah hizo tayari zipo katika kalenda ambayo umepatiwa na muda wake umeisha inafaa uzihifadhi sehemu ambayo ni nzuri au uzichome moto kurasa za kalenda hiyo ili zisiwe ni zenye kukanyangwa, kuchezewa au kutupwa ovyo bila ya kuwekewa heshima inavyopaswa.

 

Au kuziweka hizo karatasi hizo zenye Aayah za Qur-aan au jina la Allaah ('Azza wa Jalla)  katika  nidhamu ya urejelezaji (recylcing) ya karatasi n.k.  Kwa kuzipa heshima zaidi, ni bora kuziweka katika mfuko wa karatasi pekee kuliko kuzichanganya na makaratasi mengineyo na waziweke juu ya hizo zote nyingine.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share