Kuna Maneno Kwenye Khutbah Ya Ijumaa Ambayo Hayakuwepo Wakati Wa Mtume, Je, Ikiwa Mawlid Ni Bid’ah, Hayo Pia Sio Bid’ah?

 

Swali:

 

kuna mambo hayakuweko zama za mtume lakini yamekubalika baada ya kupasishwa na ulamaa. Mfano ni maneno ya mwisho katika khutba za ijumaa, INNA LLAHA YAAMURU BIL ADLI...khutba ya ijumaa ni nguzo ya kusimisha faradhi ya swala.Je,kwanini wapingwa ulamaa walo pasisha kumkumbuka mtume (mawlid)wala si kwenye faradhi ya swala,wala hawapingi sunna ya funga ?

 


 

 

Jibu:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Khutbah ya Ijumaa ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Sunnah ilikuwa ni mkusanyiko wa Aayah za Qur-aan, dhikruLlaah na kuwakumbusha watu kwa maana kuwa hakuna tofauti na wanavyohutubu watu siku hizi na wakati mwengine husoma Suurah kamili –hili siku hizi ni nadra kupatikana- kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na khutbah mbili hukaa baina yao husoma Qur-aan na kuwakumbusha watu –na katika riwayah ya an-Nasaaiy, kitabu cha Ijumaa, mlango wa kisomo katika khutbah ya pili na dhikr ndani yake- husoma Aayaat na kumdhukuru Allaah” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Ijumaa, mlango wa khutbah mbili kabla ya Swalah na yaliyomo katika hizo khutbah mbili.

 

 

“Nimeihifadhi Suurat Qaaf wal Qur-aanil Majiyd kutoka katika mdomo wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hali ya kuwa yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yu juu ya Minbar siku ya Ijumaa” Imepokelewa na an-Nasaaiy, kitabu cha Ijumaa, mlango wa kisomo katika khutbah.

 

Ndugu yetu, hayo mambo unayodai kuwa yamekubalika kwakusema ‘kuna mambo hayakuweko zama za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini yamekubalika; ukiyaangalia kwa macho ya kawaida na akili ya kawaida utaona kuwa ni yale yale yaliyokuweko katika khutbah za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Hadiyth hizo hapo na nyingine nyingi tu; hivyo hakukuwa wala hakuna wala haitokuweko haja hii ya kusema kwako ‘baada ya kupasishwa na ulamaa; na hata kama tukisema kuwa khutbah zote zinamazika hivyo basi ni vyema uelewe kuwa hayo si maneno ya hao Maulamaa bali ni Aayah katika Aayah za Qur-aan Suuratun Nahl.

 

Hata hivyo tungependa tuelewe kuwa katika sehemu nyingi za ulimwengu wetu wa Kiislamu au hapo unapoishi kama unaelewa kinachosemwa basi utaona kuwa kunahitajika kusisitizwa hayo yote, kwani yanakosekana tena katika dunia nzima na ndio kukawa na matatzio hayawezi kutatuka wala kutatuliwa na mzizi wake ni kutokuwepo hayo mambo.

 

Je, ndugu yetu, haya yanayosisitizwa kila Ijumaa huyapendi au huyahitaji?! Huku tukidai kuwa twampenda aliyekuja nayo kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); ni kweli yalihitaji kupitishwa na kukubaliwa na Ulamaa au ni katika kuwakumbusha Waislamu kuwa wanatakiwa na Mola wao wawe tayari:

 

  1. Kufanya uadilifu,

  2. Kufanya hisani,

  3. Kuwapa jamaa;

  4. Kukataza uchafu,

  5. Kukataza uovu,

  6. Kukataza dhulma.

  7. Kuwaidhiwa ili mpate kukumbuka.

 

Ni kweli ndugu yetu, Waislamu wa zama hizi na wa hapo unapoishi wewe hawahitaji haya?! Swahaba za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakipewa ukumbusho wenye kwenda na wakati wao na waliokuja baada yao pia walikumbusha kulingana na wakati wao na watakaokuja baada yetu ndio hivyo hivyo, kazi ya kukumbushana baina ya Waislamu ni ya kuendelea mpaka kitaposimama Qiyaamah.

 

Hivyo ni vyema tuelewe kuwa hakuna kilichoongezwa wala kuchomolewa katika khutbah ya kipenzi chetu sote (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bali kinachojitokeza ni watu kujaribu kumuiga yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika khutbah zao kwa kutumia mbinu na njia mbali mbali zote zina lengo la kufika ujumbe aliokuja na kututaka tuufikishe yeye mbora wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio ukawa unawasikia mara husoma Aayah hii na mara husoma ile kuhakikisha kuwa zinakwenda sambamba na munasaba au zinatatua tatizo la jamii wakati huo inaposomwa khutbah.

 

Ulivyosema ‘Mfano ni maneno ya mwisho katika khutba za ijumaa, INNA LLAHA YAAMURU BIL ADLI’ fahamu kuwa hivyo basi khatibu aliyewafikishwa na Allaah kuelewa kuwa dini ya kiislamu inasisitiza mambo hayo na Waislamu wanatakiwa wawe hivyo ndio alipoona kuwa ni munasaba katika jamii yake kwa kukosekana hayo na mengineyo kuweka katika kila khutbah yake Aayah hii:

 

“Hakika Allaah Anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka”. An-Nahl: 90.

 

Ndugu yetu, ni vyema tuelewe kuwa khutbah ya Ijumaa haiwi khutbah bila ya kupatikana Qur-aan ndani yake, Hadiyth za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), dhikr, kuwakumbusha Waislamu, kuomba du’aa na kumswalia Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hii Aayah hapa:

 

“Hakika Allaah Anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka”. An-Nahl: 90.

 

Peke yake kama itakuwa ni khutbah basi itatosha kwa siku hiyo.

 

Ndugu yetu, katika Uislamu kwa kweli na hii ndio hakika hakuna anaeyewapinga hao Maulamaa uliosema ‘kwanini wapingwa ulamaa walo pasisha kumkumbuka Mtume (mawlid); kwani kilichopo na ndio hasa tunapenda tukielewe sisi na wewe na Waislamu wengine wenye kudai kuwa twampenda Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hiki:

 

Kama Mawlid ndio kumkumbuka Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi tuelewe kuwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tunatakiwa tumkumbuke kila siku na sio siku moja katika mwaka; ndio ikawa miongoni mwa ibada anazotakiwa kila Muislamu atekeleze kila siku ni kuswaliwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ukumbusho unakuwa ukumbusho kama tutakuwa tunaiga matendo yake katika maisha yetu ya kila siku na sio vyenginevyo.

 

Hivyo basi kilichopo si kuwapinga bali ni kuwataka hawa ulamaa walo pasisha kumkumbuka Mtume (mawlid) (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kushikamana na Qur-aan na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama kweli wanataka kivitendo katika maisha yao ya kila siku kumkumbuka Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share